Mkurugenzi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Agnes Kijazi akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana kutoa utabiri wa mvua kwa kipindi cha Machi hadi Mei. Picha na Silvan Kiwale |
Akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam jana, Mkurungezi wa TMA, Agnes Kijazi alisema hali ya juu ya joto kwa upande wa Somalia inatarajiwa kudhoofisha ukanda wa mvua kwa maeneo ya nchi yetu.
Kijazi alisema viwango vya mvua ya asilimia 75 ya wastani kwa kipindi kirefu hutafsiriwa kama chini ya wastani, wakati viwango vya kati ya asilimia 75 hadi 125 hutafsiriwa kama mvua za wastani na vile vya zaidi ya asilimia 125 hutafsiriwa kama juu ya wastani .
Septemba mwaka jana Mamlaka hiyo ilitabiri kuwapo kwa mvua kubwa ambayo ingeambatana na El-nino hafifu ziliyotarajiwa kuanza katika kipindi hicho, hata hivyo miezi michache baadaye TMA ilitoa taarifa kuwa mvua hizo zilitoweka kutokana na mabadiliko ya Tabianchi.
Kijazi alisema mwelekeo wa mvua kwa Machi hadi Mei umeonyesha maeneo ya Nyanda za Juu Kaskazini Mikoa ya Kilimanjaro ,Arusha na Manyara mvua zitaanza wiki ya kwanza ya Machi.
Kanda ya Ziwa Mikoa ya Kagera,Mwanza,Mara,Shinyanga na Simiyu mvua zinatarajiwa kuanza mwanzoni mwa Machi katika Mikoa ya Kagera na Geita na baadaye kusambaa katika maeneo mengine ya Mikoa ya Mwanza.
Ukanda wa Pwani Kaskazini mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Pwani huku maeneo ya Kaskazini mwa Mkoa wa Morogoro na Visiwa vya Unguja na Pemba mvua zinatarajiwa kuanza mwanzoni mwa Machi huku zikiwa za wastani.
Kanda ya Magharibi Mikoa ya Kigoma na, Tabora Rukwa na Katavi mvua zinatarajiwa kuanza wiki ya pili ya Machi na kuisha Aprili mwaka huu.
Kanda ya Kati Mikoa ya Singida na Dodoma inatarajiwa kuwa na mvua iliyo chini ya wastani pia Ukanda wa Pwani Mikoa ya Mtwara na Lindi itapata mvua iliyo chini ya wastani.
Hata hivyo Maeneo ya Kusini Mkoa wa Ruvuma mvua zinatarajiwa kuwa za wastani huku Nyanda za juu Kusini Magharibi Mikoa ya Mbeya, Iringa, Njombe na maeneo ya Kusini mwa Mkoa wa Morogoro mvua zinatarajiwa kuwa za wastani hadi chini ya wastani.
No comments:
Post a Comment