Thursday, February 28, 2013

Wanaharakati Waishukia Serikali mauaji ya albino.

BAADA ya kuibuka upya kwa matukio ya kuuawa na kukatwa viungo vya miili kwa watu wenye ulemavu wa ngozi (albino), wanaharakati nchini wameitaka Serikali kuchunguza kwa kina sababu za mauaji hayo, kuimarisha ulinzi hasa katika maeneo wanayoishi watu wa kundi hilo.

Wakati wanaharakati hao wakieleza hayo, Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Ummy Mwalimu amesema mauaji hayo yanatokana na baadhi ya watu kuwa na imani za kishirikina, kwamba wakipata viungo vya watu wenye ulemavu watapata utajiri.
 

Alisema tayari Serikali imemuagiza Ofisa Maendeleo ya Jamii Rukwa ambao ulikumbwa na mauaji hayo, kukutana na maofisa maendeleo wa wilaya zote za mkoa huo kwa ajili ya kuwapa elimu wananchi.

Katika miaka ya hivi karibuni, jumla ya albino 72 wameuawa, 34 wamenusurika, wengi wao kwa kukatwa viungo au kuumizwa. Makaburi 15 yamefukuliwa na viungo kuchukuliwa na kumekuwa na majaribio manne ya kufukua makaburi.

Katika matukio ya hivi karibuni, walemavu hao wakazi wa Tabora na Sumbawanga wamekatwa mikono ya kushoto, ikiwa ni tofauti na miaka mitatu iliyopita ambapo waliokumbwa na ukatili huo walikatwa mikono ya kulia.

Tangu Januari mwaka huu,mlemavu wa ngozi aliyeuawa ni Lugolola Bunzari (7) na waliojeruhiwa ni Mwigulu Matonange (10) na Maria Chambanenge (39).
 

Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti, Mwenyekiti wa Kituo cha Taarifa kwa Wananchi (TCIB), Deus Kibamba alisema Serikali inatakiwa kuchunguza kwa kina chanzo cha mauaji hayo kwa maelezo kuwa yanasababishwa na mambo mengi.

“Kwanza usalama wa nchi umekuwa mdogo, siku hizi ni kawaida kusikia askari kauawa na wananchi au watu wasiofahamika, ili kumaliza mauaji ya albino ni lazima waimarishiwe ulinzi” alisema Kibamba.

Alifafanua kwamba jambo lingile linalochangia kuibuka kwa matukio ya mauaji ni kuporomoka kwa maadili, kwamba watu wamefikia hatua ya kuamini kuwa wakipata mkono wa mtu mwenye ulemavu wa ngozi watatajirika.
“Pia umasikini ni tatizo kubwa, lakini pamoja na hayo Serikali inatakiwa kutambua makazi ya watu hawa na kuimarisha ulinzi kuanzia ngazi ya mtaa hadi taifa, ni wazi kuwa hali hii itasaidia kumaliza tatizo hili” alisema Kibamba.

Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Helen Kijo-Bisimba alisema miaka mitatu iliyopita nchi ilikumbwa na matukio ya mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi, kuitaka Serikali kutumia njia ilizotumia wakati huo hadi ikafanikiwa kumaliza tatizo hilo.

“Nadhani jambo la msingi ni kuimarisha ulinzi kwa watu hawa, polisi wakishirikiana na viongozi wa mkoa, wilaya, kata na vijiji tatizo hili litakwisha” alisema Kijo-Bisimba.
 

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Jinsia nchini (TGNP), Ussu Mallya alisema, “Ulinzi na usalama kwa watu wa kundi hili ni jambo la lazima, siku hizi kuna polisi jamii na kama watashirikiana na uongozi wa mtaa au vijiji wanavyoishi watu walemavu hawa ni wazi kuwa mauaji yatakwisha kabisa.”

Kwa upande wake,Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Ummy Mwalimu alisema Serikali inatekeleza mpango wake taifa wa kupambana na ukatili wa akinamama, na watoto na kwamba itahakikisha inamaliza mauaji hayo.

“Tumemuagiza Ofisa maendeleo ya Jamii wa mkoa wa Rukwa kukutana na maofisa maendeleo ya jamii wa wilaya ili kuwapa elimu wananchi juu ya mauaji haya kwa kutumia mikutano ya hadhara, wengi wanaamini kuwa wakipata viungo vya watu wenye ulemavu huu wa ngozi watakuwa matajiri” alisema Mwalimu na kuongeza;

“Baada ya wiki moja nitakwenda Shinyanga na Kishapu kuhudhuria mikutano hiyo kwa lengo la kuwaeleza wananchi ili waachane na imani hizi, watu wenye ulemavu wa ngozi hawana tofauti na watu wengine, hivyo kuwaua ni kuwakatisha haki yao ya kuishi.”

Mwigulu Matonange (10) akiwa na baba yake Gimbishi. 

No comments:

Post a Comment