Nchi
imeingia tena katika mgawo wa umeme kinyume na ahadi iliyotolewa na
Waziri wa Nishati na Madini Prof Sospeter Muhongo bungeni tarehe 28
Julai 2012. Hali hiyo ni matokeo ya Serikali kutozingatia tahadhari
niliyoitoa bungeni tarehe 27 Julai 2012 kwa niaba ya Kambi Rasmi ya
Upinzani na kwa nyakati mbalimbali kwa nafasi yangu ya Waziri Kivuli wa
Nishati na Madini juu ya hali tete iliyotarajiwa kuwepo na hatua
zinazopaswa kuchukuliwa katika utekelezaji wa mpango wa dharura wa
umeme.
Mbunge wa jimbo la Ubungo-Chadema Mh John Mnyika |
Ikiwa ni sehemu ya wajibu wa kibunge
wa kuisimamia Serikali nawataka viongozi na watendaji wa Wizara ya
Nishati na Madini na Shirika la Umeme Nchini (TANESCO) kuacha kuficha
hali ya mambo na kuwaeleza ukweli wananchi kuhusu mgawo wa umeme
uliojitokeza na hatua za haraka zinazochukuliwa kurekebisha hali hiyo.
Iwapo Wizara na TANESCO hawatatoa
matangazo ya ukweli kwa wananchi, kwa nafasi yangu ya Waziri Kivuli wa
Nishati na Madini nitaeleza vyanzo vya mgawo wa umeme uliojitokeza ili
hatua ziweze kuchukuliwa wakati huu ambapo wajumbe wa kamati ya nishati
na madini wenye wajibu wa kuisimamia Serikali kwa niaba ya Bunge katika
sekta hizo nyeti hawajateuliwa.
Aidha, pamoja na kutoa maelezo kuhusu
mgawo wa umeme, Wizara ya Nishati na Madini na TANESCO watumie nafasi
hiyo pia kueleza hatua zilizochukuliwa kuhusu ukaguzi wa awamu ya pili
kuhusu tuhuma za ufisadi katika ununuzi wa vifaa na uzalishaji wa umeme
wa dharura ikiwemo kuhusu mafuta mazito ya kuendeshea mitambo ya kufua
umeme.
Ikumbukwe kwamba mwanzoni mwezi Agosti
2012 Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (NAOT) iliunda timu ya
wakaguzi kufanya ukaguzi maalum wa hesabu za Shirika la Umeme (TANESCO)
kufuatia tuhuma za ubadhirifu wa fedha za umma zilitajwa bungeni na
Waziri Kivuli wa Nishati na Madini katika maoni ya Kambi Rasmi ya
Upinzani tarehe 27 Julai 2012 na Waziri wa Nishati na Madini wakati wa
majumuisho ya hoja ya Serikali tarehe 28 Julai 2012.
Wizara ya Nishati na Madini na TANESCO
waeleze pia hatua iliyofikiwa kuhusu uchunguzi mwingine uliofanywa na
Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) kuanzia mwezi Agosti 2012
wa mchakato wa ununuzi wa mafuta mazito ya kuendeshea mitambo ya kufua
umeme wa dharura kutokana na tuhuma mbalimbali zilizotolewa bungeni
kuhusu ununuzi huo suala ambalo Kambi Rasmi ya Upinzani ilitaka pia
tarehe 27 Julai 2012 liundiwe kamati teule ya Bunge ili uchunguzi wa
kina uweze kufanyika.
Wenu katika uwakilishi wa wananchi,
John Mnyika (Mb)
Waziri Kivuli wa Nishati na Madini
No comments:
Post a Comment