Thursday, February 28, 2013

Kim-poulsen-kushiriki-kili-marathon.

Kocha wa timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, KIM POULSEN.
KOCHA Mkuu wa timu ya taifa (Taifa Stars), Kim Poulsen amethibitisha kushiriki mbio za Kilimanjaro Marathon mwaka huu. Mbio hizo zimepangwa kufanyika mjini Moshi Jumapili ya Machi na atakimbia umbali wa kilomita 21.
 
Hii ni historia mpya kwa Tanzania kwa kocha wa timu ya taifa kushiriki mbio za Kilimanjaro Marathon ambazo zilianza rasmi zaidi ya miaka 10 iliyopita kwa udhamini wa Bia ya Kilimanjaro Premium Lager.
 
“Nataka kujaribu mbio hizo kwa sababu napenda changamoto na hii itanipa fursa nzuri ya kukimbia huku nikiuzunguka Mlima Kilimanjaro ambao ni maarufu,” alisema.
 
Poulsen aliongeza kuwa yupo tayari kwa mashindano baada ya kufanya mazoezi kwa miezi kadhaa. “Kwa kawaida kila siku nafanya mazoezi ya kukimbia, na sasa naweza kusema kuwa nipo tayari kwa ajili yam bio hizo,” alisema.
 
Aliongeza: “Nikiwa kocha timu ya taifa, nimeona umuhimu wa kuungana na watu wengine katika medani nyingine za michezo…sijawahi kushiriki Kilimanjaro marathon lakini nimesikia mengi mazuri kuhusu mbio hizo na ndiyo maana nikaamua kushiriki.”
 
Kwa ushiriki huo, kocha huyo atakutana na magwiji wa mbio hizo Tanzania na maelfu ya wakimbiaji kutoka nchi zaidi ya 40.
 
Meneja wa Bia ya Kilimanjaro, George Kavishe amesifu uamuzi wa wa kocha na  kusema kuwa hatua ya Poulsen itachangia kwa kiasi kikubwa kuhamasisha zaidi mbio hizo. 

“Kocha ameamua kwa dhati kushiriki na hali hiyo inaonyesha wazi kuwa hata katika timu ya taifa anatimiza vema majukumu yake,” alisema Kavishe.
 
Kampuni ya Executive Solutions ndio waratibu rasmi wa mashindano hayo hapa nchini huku wadhamini wengine wakiwa ni  Vodacom Tanzania (5km Fun Run), GAPCO (Mbio fupi kwa wenye ulemavu),  Tanga Cement, CFAO Motors, KK Security, Keys Hotel, TPC Sugar, TanzaniteOne, Hoteli ya New Arusha, Maji ya Kilimanjaro , FastJet, Clouds FM na Shirika la Mfuko wa Idadi ya Watu la Umoja wa Mataifa (UNFPA).

No comments:

Post a Comment