Saturday, December 29, 2012

Chadema, Serikali, katika vita sakata la gesi.

WAKATI Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo akiyalaani maandamano yaliyofanyika juzi mkoani Mtwara akisema kuwa walioyaandaa wamelenga kuigawa nchi vipandevipande, Chadema kimemtaka Rais Jakaya Kikwete kumbana waziri huyo ili aondoe udhaifu uliopo katika sekta ya nishati.

Juzi maelfu ya wakazi wa Mkoa wa Mtwara waliandamana wakipinga uamuzi wa Serikali kusafirisha gesi kwa njia ya bomba kutoka hapa kwenda Dar es Salaam.

Maandamano hayo yaliyoratibiwa na vyama vya Chadema, NCCR-Mageuzi, Sau, Tanzania Labour Party (TLP), APPT- Maendeleo, ADC, UDP na DP yakishirikisha wananchi wa wilaya za mkoa huo, zikiwamo Tandahimba na Newala, yalianzia katika Kijiji cha Mtawanya hadi Mtwara mjini kupitia barabara ya kwenda Msimbati eneo ambako gesi asilia inapatikana.

Akizungumza na gazeti hili jana, Profesa Muhongo alisema walioandaa maandamano hayo ni watu hatari kwa amani ya nchi.

“Walioratibu maandamano hayo ni watu hatari kwelikweli kwa amani na usalama wa Tanzania, wanataka kuigawa nchi vipandevipande, hawaitakii mema nchi yetu kwa utulivu na amani tuliyonayo,” alisema Profesa Muhongo.

Hata hivyo taarifa ya Chadema iliyotumwa kwenye gazeti hili na Katibu Mwenezi wa chama hicho, John Mnyika ilisema maandamano yanatokana na uzembe wa Serikali kushindwa kurekebisha kwa wakati upungufu uliopo katika sekta hiyo.

Kadhalika, Chadema kimeitaka Serikali ieleze hatua ilizochukua dhidi ya baadhi ya viongozi waliosababisha nchi kupoteza mapato katika miradi ya gesi iliyotangulia.

“Serikali ieleze imefikia wapi kurejesha kiasi cha Dola 20.1 milioni (zaidi ya Sh30 Bilioni) zilizopunjwa kifisadi katika mauzo ya gesi asilia huku miradi ya maendeleo katika maeneo ambayo gesi hiyo imetoka kama Songosongo ikiwa na upungufu wa fedha,” alisisitiza Mnyika katika taarifa yake.

Kwa upande wao, baadhi ya wasomi wamesema hakuna kosa gesi kusafirishwa kwenda Dar es Salaam, lakini wakaitaka Serikali kuchukua hatua za kuwaelimisha wananchi hao na kuweka wazi kile watakachonufaika nacho katika mradi huo.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Profesa Prosper Ngowi alisema wananchi wanatakiwa kutambua
kuwa gesi kusafirishwa kwenda jijini Dar es Salaam hakutawanyima fursa ya kunufaika na nishati hiyo, lakini akasema Serikali ichukue hatua za kuwaelimisha.

Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Bashiru Ali alisema kitendo walichokifanya wakazi wa Mtwara ni ujumbe kwa Serikali kuwa makini katika mgawanyo wa rasilimali za nchi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo Cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Helen Kijo-Bisimba alisema uamuzi wa wananchi kuandamana unatokana na kutoshirikishwa kikamilifu katika mchakato wa uvunaji wa rasilimali hiyo.
Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo akijibu hoja Bungeni siku za hivi karibuni.

No comments:

Post a Comment