Sunday, December 30, 2012

Matokeo ya Sensa hadharani kesho.

MATOKEO ya Sensa ya Watu na Makazi iliyofanyika Agosti 26, mwaka huu yanatarajiwa kutangazwa kesho na Rais Jakaya Kikwete, katika hotuba yake ya mwisho wa mwaka kwa Taifa.

Kazi hiyo ya maandalizi ya matokeo hayo ya Sensa iliyofanyika kwa zaidi ya miaka saba, inatarajiwa kufanyika jijini Dar es Salaam, katika viwanja vya Mnazi Mmoja, ambapo utafanyika uzinduzi wake.

Akizungumza na MTANZANIA Jumapili, Kamishna wa Sensa ya Watu na Makazi, Hajat Amina Mrisho, alisema kazi ya kuingiza takwimu imekamilika mapema mwezi huu, ambapo pamoja na mambo mengine ripoti hiyo ya matokeo wanatarajiwa kuikabidhi kwa Rais Kikwete kesho.

“Ofisi ya Taifa ya Takwimu, imejipanga kikamilifu katika hili na ratiba yetu tuliyoitoa hadi sasa imekwenda vizuri kwani kazi kubwa ilikuwa ni kuingiza Data, katika vifaa maalum na hivi sasa tumekamilisha na kesho Mungu akipenda ripoti tutaikabidhi kwa Rais Kikwete.

“Sensa ya mwaka huu imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kwa zaidi ya asilimia 95, kwa upande wa Tanzania bara, hasa baada ya zoezi hili tulilazimika kuongeza muda wa wiki moja zaidi kwa lengo la kufanya kazi nzuri kwa maslahi ya Taifa letu.

“Uzinduzi wa ripoti hii ya Sensa tutaufanya kesho Desemba 31, katika viwanja vya Mnazi Mmoja kama tulivyopanga na hivi sasa tupo katika maandalizi ya mwisho kuweza kukamilisha jambo hili liwe na ufanisi wa hali ya juu kuliko Sensa zilizotangulia.

“Kama unavyofahamu Ofisi ya Taifa ya Takwimu Tanzania (NBS), awali tulitangaza kuongeza wiki moja kutoka Agosti 30 hadi Septemba 8, kwani hata siku tulizoongeza zilikuwa na mafanikio ambapo kila aliyekuwa na haki ya kuhesabiwa alifikiwa na makarani wetu,” alisema Hajat Amina.

Akizungumzia kuchelewa kwa matokeo ya Sensa, Kamishna huyo wa Sensa, alisema NBS ilipanga ratiba tofauti na wananchi walivyokuwa wanafikiria, kwani tangu awali walitangaza matokeo yangetangazwa Desemba 31, na Rais Kikwete, katika hotuba yake ya kufunga mwaka 2012.

“Nataka niwaeleze Watanzania kuwa, Sensa ya mwaka huu imefanyika katika kipindi kifupi hadi kufikia hatua ya kutangazwa kwa matokeo.

“Sensa zilizopita tulikuwa tunakaa zaidi ya mwaka mmoja hadi kutoka matokeo yake. Safari hii NBS tulijipanga kikamilifu na tulihakikisha tunakuwa na vifaa vya kisasa ambavyo vimesaidia kazi hii kufanyika kwa miezi minne tu.

“Tunawaomba Watanzania waondoe hofu katika hili na kadri tutakavyokuwa tunafanya Sensa zetu tunaweza tukawa tunakwenda kwa muda mchache zaidi.

“Huenda katika Sensa ijayo ya mwaka 2022 itakuwa ni nzuri zaidi hasa kutokana na kila siku kuzaliwa kwa teknolojia mpya na za kisasa,” alisema.

Kutokana na hali hiyo alisema kuwa, zoezi hilo litakuwa na mchakato, ambapo baada ya kutangazwa matokeo hayo na Rais Kikwete, NBS itaanza kuchambua takwimu za kila mkoa, wilaya hadi kata na vijiji na kuzisambaza kwa wadau wa maeneo husika kwa ajili ya kuzifanyia kazi katika shughuli zao za kila siku.

“Awali tulianza na kazi ya kutenga maeneo ya kuhesabia watu kwenye kila kijiji na wilaya kwa nchi nzima, na hata kulazimika kurudi tena pale ambapo tulipohisi ramani zetu zimeharibika hasa mvua kubwa zinapoharibu miundombinu ya eneo husika.

Hajat Amina, alisema pamoja na kazi hiyo kukumbana na changamoto kadhaa, Sensa imefanyika kwa umakini wa hali ya juu na kwamba iligharimu Sh bilioni 140, hadi kukamilika kwake.

“Malengo ya Maendeleo ya Milenia, ambayo pia yanatekelezwa na Serikali yanahitajika yafanyiwe tathmini hapo ifikapo mwaka 2015. Bila ya shaka mnafahamu kuwa tathmini ya mikakati hiyo, malengo hayo ya milenia na mipango mingine ya kuimarisha hali ya maisha, haiwezi kufanyika bila ya kuwepo taarifa za uhakika na zilizo sahihi. Huo ndio ukweli,” alisema Hajat Amina.

Kwa upande wake Ofisa Uhamasishaji wa Sensa, Said Ameir, alisema pamoja na maandalizi hayo Sensa ya mwaka huu ilikumbana na changamoto kadhaa ikiwemo matishio ya baadhi ya jamii kutangaza kugomea Sensa, lakini baada ya kupatiwa elimu ya muhimu wa kazi hiyo waliweza kushiriki kikamilifu.

“NBS tulikabiliwa na kadhaa katika kazi hii hasa katika siku ya kilele cha Sensa Agosti 26, mwaka huu ambapo kuna baadhi ya maeneo yalikumbwa na changamoto za kuchelewa vifaa kwa makarani wetu.

“Mbali na hilo pia hata sare kwa ajili ya maafisa wa sensa na upungufu wa fomu za sensa ambazo zilichelewa, lakini baada ya muda katika maeneo yote nchi nzima vifaa vyote viliweza kukamilika.

“Hata hapa makao makuu, tuliweka pamoja mfumo mzuri wa usambazaji, lakini baadhi hawakuufuata. Hivyo, vifaa kwa ajili ya mahali fulani vilipelekwa mahali pengine hii nayo ilikuwa ni sababu ya kukosa fomu za kutosha kwa wakati huo,” alisema Ameir.

No comments:

Post a Comment