Sunday, December 30, 2012

WANA-TANGA WAAOMBWA KUCHANGIA UJENZI WA BARABARA YA KWEMATINDI-GARE.

WAKAZI wa Kijiji cha Gare, Kata ya Magoroto, Wilaya ya Muheza, mkoani Tanga, wanaomba wadau na wananchi wenye mapenzi mema kuchangia ujenzi wa barabara ya Kijiji cha Kwematindi hadi Gare, kwa kuwa inachangia kuzorotesha uchumi wao.

Mkakati wa kuomba msaada wa ujezni wa barabara hiyo umeanza baada ya kuona Serikali ya Kijiji na Kata hawana mpango wa kuendeleza kijiji hicho ambacho hakina barabara tangu uhuru.

Barabara hiyo imekuwa kikwazo cha shughuli nyingi za kiuchumi, hasa kipindi cha masika, hali inayohitaji jitihada za haraka kuijenga kwa maslahi ya wananchi wa kijiji hicho na Taifa kwa ujumla.

Lakini kutokuwepo kwa barabara hiyo imekuwa ni chanzo cha umasikini kwa wakazi wa kijiji hicho ambao wengi wao ni wakulima na wanashindwa kufanya shughuli zao za kuinua uchumi kutokana na miundombinu ya barabara ambayo imekuwa ikiwakwamisha kusafirisha bidhaa zao na wananchi kushindwa kufika kijijini kwa urahisi.
 
Ni moja ya mabasi mkoani Tanga linalotumia barabara hiyo.
Kukosekana kwa barabara hiyo kumewanyima wanakijiji fursa ya kupata huduma za jamii kama vile shule na hospitali hali inayochangia kurudi nyuma kimaendeleo.

Barabara hiyo korofi na isiyopitika kwa magari wala pikipiki, inahitaji kuchongwa kwa gharama ya Sh Mil 13,120,000 hali ambayo imekuwa ngumu kwa kuwa wanakijiji wengi hawana uwezo huo kutokana na kukosa kipato na hivyo ni muda muafaka kwa wananchi, hasa wanaoishi Dar es Salam watokao mkoani Tanga, kusaidia harakati za ujenzi wa barabara hii, kwa kuwa baada ya mambo yote nyumbani ni muhimu.

No comments:

Post a Comment