Monday, December 31, 2012

Mhasibu Simba aporwa mamilioni ya mechi kati ya Simba na Tusker.

Zaidi ya Sh. milioni 10 za klabu ya Simba zimeporwa baada ya Mhasibu wa klabu hiyo, Erick Sekiete (28) kudai kuvamiwa na majambazi sita katika mtaa wa Sinza kwa Remmy na kuporwa kiasi hicho cha pesa juzi saa 3:20 usiku.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Charles Kenyela alisema kuwa Sh. milioni 7.59 na dola za Marekani 2,000 ambazo Simba walizipata baada ya makato ya mapato ya mechi yao dhidi ya Tusker FC ya Kenya iliyomalizika kwa wenyeji Simba kuchapwa 3-0 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

 
Alisema kuwa baada ya kukabidhiwa fedha hizo, Sekiete na mwenzake Stanley Phillipo (23) ambaye alidaiwa kuwa ni mwanafunzi, walipanda kwenye gari aina ya Toyota Premio yenye namba za usajili T869 BKS lililokuwa likiendeshwa na Said Pamba na kwamba walipofika eneo hilo, dereva aliwashusha na kwamba wakaanza kutafuta teksi.

Aliendelea kueleza kuwa muda mfupi baada ya kushushwa, Sekiete na Philipo waliamua kuvuka upande wa pili wa barabara iendayo Kijitonyama ili wachukue teksi lakini ghafla  walitekwa na watu sita walioshuka kutoka kwenye pikipiki tatu.

Aliendelea kufafanua kuwa wakati watu hao wakimnyang’anya begi Sekiete walikuwa wakitamka maneno ya kejeli kwa uongozi wa Simba.

Kamanda Kenyela alisema kuwa baada ya watu hao kupora fedha hizo, walitokomea kusikojulikana na hadi sasa, Jeshi la Polisi linawashikilia watu watatu akiwamo Sekiete kuhusiana na tukio hilo.

Watu wengine wanaoshikiliwa na jeshi hilo katika Kituo cha Polisi Magomeni ni Pamba na Philipo ambao walikuwa pamoja na Sekiete kwenye gari.

 
Mwenyekiti wa Simba, Aden Rage amesema hapo jana kuwa amesikitishwa na taarifa za kuporwa kwa fedha za klabu yao.
Kamanda mkoa wa Temeke, Charles Kenyela.
 

No comments:

Post a Comment