Saturday, December 29, 2012

KUMALIZIKA KWA KESI YA LEMA, KWAIBUA MENGI.


MBUNGE wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema, akihojiwa na vyombo mbalimbali vya hbarai mara baada ya hukumu iliyomrejeshea ubunge wake.
MWANAZUONI aliyebobea katika sheria, Profesa Issa Shivji na Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Francis Stolla wamekosoa hukumu ya Mahakama ya Rufani, iliyomrejesha bungeni, Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti juzi, wanasheria hao walisema hukumu hiyo iliyotolewa na majaji watatu wakiongozwa na Nathalia Kimaro, Salum Massati na Bernard Luanda, inapingana na sheria.

Hata hivyo, mmoja wa mawakili wa Lema, Method Kimomogoro amepinga madai hayo akisema wanaoipinga pengine hawajapata nafasi ya kuliangalia kwa undani suala la haki ya mpiga kura kupinga matokeo mahakamani.

Profesa Shivji kwa upande wake alieleza kushangazwa na maelezo ya Mahakama ya Rufani kuwa mpiga kura hana haki ya kufungua kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi na kusema hiyo ni sawa na kutunga sheria mpya na si kutafsiri zilizopo.
Alisema Sheria ya Bunge ya Uchaguzi, Katiba ya nchi na Mahakama, vinampa haki mpiga kura kufungua kesi kupinga matokeo ya uchaguzi.

“Sheria ya Bunge na Mahakama Kuu katika kesi ya Mgonja (Chediel ya mwaka 1980), vinampa haki mpiga kura kufungua kesi mahakamani kupinga matokeo. Sijaona hoja nzito ya Mahakama ya kufuta haki hiyo ya mpiga kura,” alisema Profesa Shivji.

Katika shauri hilo namba 84 la mwaka 1980 lililofunguliwa na William Bakari na mwenzake dhidi ya Mgonja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Mahakama Kuu Tanzania iliamua kuwa, mpiga kura ana haki kufungua kesi mahakamani kupinga matokeo. Walalamikaji walishinda.

Hata hivyo, Mahakama ya Rufani katika kesi ya Lema, iliamua kwamba hukumu katika kesi ya Mgonja ilikosewa kwani si sahihi kwamba mtu yeyote bila kujali mahali alipojiandikisha na kupiga kura anaweza kupinga matokeo katika jimbo lolote nchini hata kama haki zake hazijakiukwa kwa namna yoyote.

Lakini Profesa Shivji aliitetea hukumu hiyo ya Mgonja akisema imekuwapo kwa zaidi ya miaka 30 sasa na kwamba kwa muda wote huo imekuwa ikifuatwa katika uamuzi wa mashauri mbalimbali, huku akisisitiza kuwa Mahakama haiwezi kuifuta kirahisi tu.

Profesa Shivji alisema mpiga kura ni mwananchi na kwa vyovyote ana masilahi katika uchaguzi husika na hivyo anatarajia kuona uchaguzi ambao ni huru na wa haki.
“Hivyo huwezi kusema hahusiki na nani kashinda au kashindwa kwa kuwa uchaguzi ni muhimu katika kujenga na kukuza demokrasia,” alisema Profesa Shivji.

Chama cha Wanasheria
Kwa upande wake, Stolla alisema: “Nimesikiliza hata maoni ya wanasheria mbalimbali wakizungumzia kutofurahishwa na tafsiri ya Mahakama ya Rufani kuhusu haki ya mpiga kura ‘ku-challenge’ (kupinga) matokeo ya uchaguzi mahakamani,” alisema na kuongeza:
“Katika uamuzi wa kisheria, inaonekana Mahakama imetunga sheria mpya na wengi tunajiuliza kama siyo, sababu ya kuwa mpiga kura ni ipi nyingine inampa haki mpiga kura kupinga matokeo?”

Stolla alisema Sheria ya Bunge ya Uchaguzi ya tangu mwaka 1985, ambayo ilifanyiwa marekebisho mwaka 2002, kabla ya kutungwa upya mwaka 2005, inampa haki mpiga kura kupinga matokeo ya uchaguzi mahakamani.

“Mwaka 2002, sheria zote zilifanyiwa marekebisho na baadaye mwaka 2005, Bunge likatunga sheria mpya inayoitwa Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, ikafuta ya mwaka 1985. Sheria hiyo na marekebisho yake, ndiyo inayotawala uchaguzi hadi sasa,” alisema.

Alisema hata kabla ya kutungwa kwa sheria hiyo ya Uchaguzi ya mwaka 1985, tayari kulikuwa na uamuzi wa Mahakama Kuu katika kesi ya Mgonja ambayo iliamua kuwa mpiga kura ana haki ya kupinga matokeo ya uchaguzi mahakamani.

No comments:

Post a Comment