Sunday, December 30, 2012

KLABU ZASUBIRI FEDHA ZAO TRA ZICHEZE LIGI KUU.

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Desemba 28, 2012

Klabu 14 ambazo timu zao zinashiriki Ligi Kuu ya Vodacom zimesema hazitacheza hatua ya pili ya Ligi hiyo inayotarajiwa kuanza Januari 26 mwakani hadi zitakaporejeshewa fedha zao zilizochukuliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kutoka kwenye moja ya akaunti za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

Novemba 23 mwaka huu, TRA kwa uwezo ilionao kisheria iliielekeza benki ya NMB kuilipa fedha hizo (sh. 157,407,968) kutoka kwenye moja ya akaunti za TFF ikiwa ni Kodi ya Lipa Kama Unavyopata (PAYE) kutoka kwenye mishahara ya waliokuwa makocha wa timu za Taifa.

Serikali ndiyo inayolipa mishahara ya makocha hao moja kwa moja kwenye akaunti zao, lakini ilikuwa haikati PAYE kutoka kwenye mishahara hiyo, hivyo malimbikizo kufikia sh. 157,407,968.

TFF bado inaendelea na mazungumzo na pande husika (Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kwa upande mmoja na TRA kwa upande mwingine) ili fedha hizo zirejeshwe kwani zilitolewa na mdhamini wa Ligi Kuu (kampuni ya Vodacom) kwa ajili ya maandalizi ya timu hizo tayari kwa mzunguko wa pili wa Ligi hiyo.

OFISA WA CAF KUTUA MWAKANI KUKAGUA VIWANJA
Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) litamtuma nchini ofisa wake Abbas Sendyowa kukagua viwanja na hoteli ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa utaratibu wa klabu kupata leseni zitakazoziwezesha kushiriki michuano inayoandaliwa na Shirikisho hilo.

Ofisa huyo kutoka Uganda atawasili nchini Januari 7 mwakani ambapo anatarajiwa kukamilisha kazi hiyo Januari 14 mwakani na baadaye kupeleka ripoti yake CAF.

Utekelezaji wa kazi yake nchini utahusisha mwakilishi kutoka TFF, mwakilishi kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, mameneja wa viwanja husika na Ofisa Usalama wa TFF.

NAZARIUS KILUNGEJA AONDOLEWA UCHAGUZI RUREFA
Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imekubaliana na uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi ya Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Rukwa (RUREFA) kumuondoa Nazarius Kilungeja kugombea uenyekiti katika uchaguzi wa chama hicho.

Kutokana na uamuzi huo, Kamati ya Uchaguzi ya TFF imeiagiza Kamati ya Uchaguzi ya RUREFA kuendelea na mchakato wa uchaguzi huo kama ilivyopangwa awali.

Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

No comments:

Post a Comment