Sunday, December 30, 2012

MADAKTARI 30 WASIMAMISHWA KAZI KWA MUDA.

BARAZA la madaktari Tanganyika limewasimamisha kwa muda madaktari 30, kutoa onyo kwa madakari 289 na kuwafutia mashtaka madaktari 49 baada ya kupitia malamamiko ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kufuatia mgomo wa madaktari uliotokea Juni 23 hadi 28 mwaka huu.

Taarifa iliyotolewa jana na Msemaji wa Wizara hiyo, Nsachris Mwamwaja imeeleza kuwa Baraza lilipitia malalamiko yote na limetoa adhabu stahiki kwa kila daktari aliyethibitishwa kushiriki katika mgomo huo.

Madaktari wakiwa katika chumba cha upasuaji.
Alisema mashtaka yaliyoahirishwa kutokana na wahusika kuhitaji ushauri wa kisheria ni madaktari wanne na mashtaka yasiyosikilizwa kutokana na wahusika kutofika walipoitwa na Baraza ni madaktari 22.

“Wizara inakamilisha taratibu za kinidhamu kwa mujibu wa Kanuni za  Utumishi wa Umma kwa Madaktari wote waajiriwa ambao walipatikana na hatia mbele ya Baraza la Madaktari,”aliseleza Mwamaja na kuongeza
“Wizara pia imeridhia kuwapa madaktari waliokuwa katika mafunzo kwa vitendo fursa nyingine ya kuendelea na mafunzo hayo katika hospitali za Umma walizokuwepo kabla ya kuondolewa.”

Hata hivyo alisema fursa hiyo haitawahusu madaktari wote waliopewa adhabu za kusimamishwa na Baraza la Madaktari, hadi hapo watakapomaliza kutumikia adhabu zao.

Alisema kwa taarifa hiyo madaktari wote waliofutiwa mashtaka na wale waliopewa onyo na onyo kali wanatakiwa kuwasilisha kwa Katibu Mkuu Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii barua kutoka kwa msajili wa Baraza la Madaktari ikithibitisha kurejeshewa usajili  na kuruhusiwa kuendelea na mafunzo kwa vitendo.

Vile vile madaktari waajiriwa(Registrar) wanatakiwa pia kuripoti kwa Katibu Mkuu ili kupewa
barua zao kulingana na Adhabu walizopewa.

No comments:

Post a Comment