Sunday, December 30, 2012

MBUNGE MURJI ATETEA WANANCHI WAKE, GESI KUBAKI MTWARA.

BAADA ya kutoonekana kwenye maandamano ya wakazi wa Mkoa wa Mtwara ya kupinga gesi kupelekwa Dar es Salaam yaliyofanyika Desemba 27 mwaka huu, Mbunge wa Mtwara Mjini, Hasnain Murji ameibuka na kusema anaunga mkono wananchi hao kutetea maslahi yao na kuwa tamko lililotolewa lilikuwa dhaifu.

“Hoja ya msingi ni kwa namna gani bomba la gesi litanufaisha Wana-Mtwara. Mimi kwa kiwango fulani sikubaliani na hoja ya gesi isiende Dar es Salaam lakini naungana na wananchi kudai tutafaidikaje na bomba hilo,” alisema Murji katika mahojiano maalumu na mwandishi wa habari hizi jana.

Alisisitiza kuwa, “Ninakubali gesi iende Dar es Salaam kwa sharti la kuzalisha umeme tu, si kwa matumizi mengine, wakianza kuitumia kwenye viwanda watakuwa wametuua kabisa.”
Alibainisha kuwa kitendo cha wananchi kuandamana ni haki yao ya msingi na hakipaswi kubezwa na mtu yeyote kwa sababu wanateteta haki yao ya msingi ya kufaidika na rasilimali yao.

Mbunge wa jimbo la Mtwara Mjini, Mhe.Asnaain Murji.
“Leo hii waziri ananipigia simu kuniuliza mahitaji yetu ni yapi, hilo ni jambo la msingi ndiyo maana nasema tamko lililotolewa wakati wa maandamano ni dhaifu kwa sababu halielezi mahitaji yetu ni yapi. Lazima tuwape conditions (masharti) kwamba gesi ikienda Dar es Salaam sisi tunahitaji hiki na kile,” alifafanua Murji.

Aliongeza kuwa, “Nimeandaa kikao na viongozi wa umoja wa vyama vya siasa vilivyoratibu maandamano hayo ili tukae tuainishe mahitaji yetu ni yapi iwapo gesi itakwenda Dar es Salaam, lazima tuwe na mkataba, tusikatae tu, tueleze tunahitaji nini gesi ikienda Dar es Salaam.

Akizungumzia kauli ya mkuu wa mkoa huo, Joseph Simbakalia ya kuwaita wanaopinga gesi kupelekwa Dar es Salaam wapuuzi na baadaye wahaini, Murji alisema “Hakupaswa kufanya hivyo, si busara kuwaita watu wanaodai haki yao wapuuzi au wahaini.”

Alieleza kuwa ni vyema angekwenda kupokea maandamano na baadaye angewaelimisha wananchi waliokuwapo hapo kuwa Serikali imeamua hivyo kwa sababu kadhaa. Wapo ambao wangemwelewa, lakini kuwaita wapuuzi au wahaini sidhani kama itasaidia.”

Kauli hiyo ya mbunge imekuja wakati ambapo tayari Mkuu wa mkoa huo Simbakalia amesisistiza kuwa alikuwa sahihi kuwaita wapuuzi na pengine wahaini, huku Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo akikazia uzi kuwa walioandaa maandamano hayo ni watu hatari kwa usalama wa Taifa.

No comments:

Post a Comment