KOCHA mpya
wa mabingwa wa soka Tanzania Bara, Simba SC, Mfaransa Patrick Liewig anatarajiwa
kuwasili leo nchini na atakuwapo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuishuhudia
timu hiyo ikimenyana na mabingwa wa Kenya, Tusker FC.
Ofisa Habari
wa Simba SC, Ezekiel Kamwaga amesema kwamba, awali kocha huyo alitarajiwa kuawasili
nchini juzi, lakini ilishindikana baada ya kukosa nafasi kwenye ndege na sasa
mashabiki wa timu hiyo wamtarajie leo.
Alisema
kocha huyo ambaye anakuja kurithi mikoba ya Mserbia Profesa Milovan Cirkovick,
atakishuhudia kikosi cha Simba kikicheza mechi hiyo kabla ya kuendelea na
taratibu nyingine ikiwemo kusaini mkataba wa kazi na baadaye kuanza kutumikia
kibarua chake kipya.
Kocha mpya wa wekundu wa msimbazi simba, Mfaransa, Patrick Liewing. |
Kwa upande
wa uzoefu, Liewig alifanya kazi PSG kuanzia mwaka 1989 hadi 1999 kama Kocha
Mkuu wa akademi na kuna wakati alikuwa akishirikishwa pia katika programu za
timu A, ingawa majukumu yake zaidi yalikuwa ni kwa Under 20, Under 18 aliowawezesha
kutwaa Kombe la French Junior Gambardella na Under 16.
Kuanzia
mwaka 1989 hadi 1990: alikuwa Meneja
Mkuu wa Tomislav IVIC, 1990 hadi 1991 alikuwa Msaidizi wa Henri Michel, 1991 hadi
1994 alikuwa Msaidizi wa Artur Jorge, 1994 hadi 1996 alikuwa Msaidizi wa Luis Fernandez,
1996 hadi 1998: alikuwa Msaidizi wa Ricardo Gomez, 1998 hadi 1999 alikuwa
Msaidizi wa Alain Giresse.
Liewig pia
alifundisha Al Wahda FC ya Abu Dhabi kuanzia 1999 hadi 2001, ambayo aliipa
ubingwa wa Ligi Kuu ya nchi hiyo na Kombe la Ligi.
Januari
mwaka 2003 alikuwa Msimamizi wa Chama cha Soka UAE katika fainali za Afrika za
U20 nchini Burkina Faso.
Kuanzia
mwaka 2004 hadi 2009 alikuwa Kocha wa ASEC Mimosas ya Ivory Coast aliyoipa
mataji matatu ya Ligi Kuu ya nchini humo mfululizo, 2004, 2005 na 2006, Super
Cup ya nchini humo 2005, 2007, 2008 na 2009 na akaiwezesha kufuzu hatua ya
makundi ya Ligi ya Mabingwa mara tatu, mara moja akiifikisha Nusu Fainali.
Amekuwa
Kocha bora wa Ivory Coast miaka mitatu mfululizo, 2004, 2005 na 2006 na tangu Septemba
mwaka jana hadi Juni mwaka huu, alikuwa kocha wa Club Africain ya Tunisia
Kuelekea
mchezo wa leo, Simba itamenyana na Tusker FC ambayo ilianza vema ziara yake
nchini, baada ya kuichapa Yanga 1-0 katika mchezo ulipigwa kwenye Uwanja wa
Taifa Jumatano.
Simba SC na
Tusker zinatarajiwa kukutana pia kwenye Kundi la Mapinduzi visiwani Zanziabr
hivi karibuni, kwani zimepangwa kundi moja, A pamoja na Bandari ya Unguja na Jamhuri
ya Pemba.
Aidha,
katika Kundi B, washindi wa pili wa Ligi Kuu ya Bara, Azam FC ya Dar e Salaam
pia, imepangwa na Mtibwa Sugar ya Morogoro, Coastal Union ya Tanga na Miembeni ya Unguja.
Michuano ya Kombe
la Mapinduzi, ambayo ni maalum kwa ajili ya kuherehekea Mapinduzi matukufu ya
Zanzaibar, inatarajiwa kuanza kutimua vumbi Januari 2, hadi kilele cha miaka 49
ya Mapinduzi ya Zanzibar, Januari 12, mwakani, huku ikishirikisha timu kutoka
ndani na nje ya Tanzania.
Kwa mujibu
wa ratiba ya michuano hiyo iliyotolewa na Kamati Maalum ya Kusimamaia michuano
hiyo, inaonesha kuwa katika mchezo wa kwanza utakaochezwa siku ya ufunguzi
itakuwa ni kati ya Bandari kutoka Unguja ambayo itacheza na Jamhuri kutoka
kisiwani Pemba ambao ni wawakilishi wa Zanzibar katika Kombe la Shirikisho
Barani Afrika, pamabanolitakalochezwa katika uwanja wa Mao Tse Tung mjini
Unguja, huku usiku wa siku hiyo hiyo katika Uwanja wa Amaan kisiwani Unguja
pambano la ufunguzi rasmi katika mashindano hayo likiwakutanisha mabingwa wa
soka nchini Tanzania, Simba SC ambao watapambana na mabingwa wa soka nchini
Kenya, Tusker.
Kwa mujibu
wa ratiba hiyo jumla ya timu nane zitashiriki katika mashindano hayo ambayo
yamejipatia umaarufu mkubwa visiwani hapa, timu hizo zimegawanya katika makundi
mawili ambayo ni kama ifuatavyo:
Awali
michuano hiyo ilitarajiwa kuanza kisiwani Pemba tarehe 1 Januari, lakini
kutokana na kujitoa katika mashindano kwa klabu ya Al-Ahly ya Misri kutokana na
klie kilichoelezwa sababu za kiusalama, mechi zote sasa zitachezwa kisiwani
Unguja na ufunguzi ukipangwa kuanza tarehe 2 badala ya tarehe 1 januari.
Bingwa wa
michuano hiyo ataondoka na zawadi ya kombe na fedha taslim Tsh.Milioni kumi
(10,000,000), mshindi wa pili Milioni tano (5,000,000), pamoja na zawadi
nyengine ambazo zimegawanywa katika makundi tofauti ikiwemo zawadi ya mfungaji
bora, mchezaji bora, mwamuzi bora, kipa bora, mwandishi wa habari bora, timu
bora na zawadi nyinginezo.
No comments:
Post a Comment