Malalamiko hayo yametolewa mwishoni mwa wiki na Katibu wa Chama cha Wazalishaji Chumvi Tanzania (TASPA), Julius Mosha wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa kuhusiana na malalamiko yanayotolewa mara kwa mara na wadau wa sekta ya chumvi.
Mosha alisema kuwa mwaka 2008 Halmashauri hiyo ilipitisha sheria ndogo ya ongezeko la ushuru wa chumvi toka kutoka Sh.50 kwa mfuko wa kilo 50 sawa na Sh,1000 kwa tani, ikafikia Sh.200 kwa mfuko wa kilo 50 sawa na Sh.4000 kwa tani, hata hivyo ongezeko hilo lililalamikiwa sana na kudai kuwa inashangaza licha ya kuwa na malalamiko hayo kuna taarifa nyingine ya ongezeko la asilimia 50 zaidi.
Alisema licha ya kuwa na malalamiko hayo, Halmashauri hiyo imekuwa na tabia ya kufanya maamuzi ya kuongeza ushuru wa aina mbalimbali bila ya kushirikisha wadau kwa mujibu wa sheria hali inayosababisha kuongezeka kwa gharama ya uzalishaji kulinganisha na bei ya chumvi katika masoko.
Mmoja wa wadau ambaye pia ni mshindi wa Tuzo ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA ) kwa mwaka 2012 anayeongoza kwa kulipa Kodi ya Mapato katika Wilaya ya Bagamoyo Kampuni ya H.J.Stanley and Sons Ltd imelalamikia Wilaya hiyo kutoza ushuru mwingi katika sekta ya chumvi ikiwa ni pamoja na kuwa na urasimu katika baadhi ya mambo yanayohusu uwekezaji.
Imeelezwa kuwa licha ya wao kuwa na uzalendo wa kupenda kulipa kodi ya mapato kama sheria inavyowataka kufanya hivyo , lakini wamejikuta wakipambana na ushuru wa Wilaya ambao kimsingi ni mkubwa hali inayowatia wasiwasi katika kuendesha shughuli zao za chumvi.
Kauli hiyo ilitolewa na Msemaji wa Kampuni hiyo Richard Stanley wakati alipokuwa akizungumzia kuongeza kwa ushuru wa chumvi pamoja na changamoto anazokabiliana nazo katika sekta hiyo.
Aliongeza kuwa ushuru unaotozwa na Halmashauri ya Bagamoyo unapingana na sheria inayowataka wao walipie asilimia 0.3 tu ya faida wanayopata kutokana na uzalishaji wao, lakini wanatozwa karibu asilimia 6 ambapo kwa kila mfuko wa chumvi unaozalishwa katika Wilaya ya Bagamoyo anapaswa kulipia Sh.200.
Sambamba na hayo mwekezaji huyo amelalamikia baadhi ya tabia inayoashiria urasimu kwa baadhi ya watendaji pindi wanapofuatilia nyaraka mbalimbali za ardhi, kwani wamekuwa wakipigwa danadana mara kwa mara huku wakidai nyaraka hazionekani katika Idara ya ardhi licha ya wao kuzipeleka mara nyingi tangu mwaka 2010.
Aidha aliiomba Serikali kuingilia swala hili na kuangalia ni jinsi gani wanaweza kusaidia kupunguza ushuru unaotozwa na Halmashauri ya Bagamoyo kwa wazalishaji wa chumvi, ikiwa ni pamoja na kupunguza urasimu usio wa lazima pindi watu wanapofuatilia haki zao.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo Samuel Saliyanga alisema Hamashauri yake inatekeleza sheria ndogo za Halamshauri na zilizopitishwa na Waziri Mkuu na si vinginevyo na kwamba tayari imeshapitishwa sheria nyingine ya kuongeza ushuru huo kwa watu wa chumvi.
Saliyanga alisema tayari Waziri Mkuu ameshapitisha sheria ndogo katika Halmashauri yake kuanzia Novemba 8 mwaka 2012 na itatumika kuwatoza ushuru wa chumvi kwa kila mfuko wa kilo 50 sh.300 badala ya Sh.200 iliyokuwa ikitozwa awali kwa kila mfuko wa chumvi wa kilo 50 na kwamba ushuru huo si wa uzalishaji.
Baadhi ya wachimba chumvi ya mawe katika Halmashuri ya wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani wakiendelea na kazi yao ya kutunza na kukusanya chumvi hiyo. |
No comments:
Post a Comment