Saturday, December 29, 2012

MATAYARISHO YA ZANZIBAR KUHAMA ANALOGIA KWENDA DIJITALI YAENDELEA.

Waziri wa Habari,Utamaduni,Utalii na Michezo Saidi Ali Mbarouk akijibu maswali ya waandishi wa habari hawapo pichani kulia ni Naibu Waziri wa Habari,Utamaduni,Utalii na Michezo Bihindi Khamisi Hamadi.
 
Picha na Makame Mshenga-Maelezo Zanzibar
……………………………………………………….
Na Faki Mjaka-Maelezo Zanzibar

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema matangazo ya mfumo wa Analogia yatazimwa rasmi katika Mikoa yote ya Zanzibar ifikapo Februari 28 mwakani ili kupisha mfumo mpya wa matangazo kwa njia ya Dijitali.

 Waziri wa habari, utamaduni, utalii, na Michezo Said Ali Mbarouk ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na Waandishi wa habari katika ukumbi wa Habari maelezo kikwajuni mjini Zanzibar kuhusiana na matayarisho ya kuhamia katika mfumo mpya wa matangazo ya Dijitali.
 
Amesema Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na Kamisheni ya Utangazaji Zanzibar (ZBC) zimeshauriana na kukubaliana kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iingie katika mfumo mpya wa Dijitali kwa awamu ambapo kwa zoni ya ZanzĂ­bar imekubaliwa kuwa February 28 2013 ndio iwe mwisho rasmi wa matangazo ya Analogi.

Waziri Mbarouk amesema Wizara yake haitozima mitambo ya matangazo ya Analogi ifikapo Disemba 31 bali itakachofanya ni kutangaza kwa pamoja matangazo ya Analogi na Digitali kwa mfumo unaojulikana kitaalamu kama SIMU L CAST hadi itakapofika muda rasmi wa kuhama mfumo wa Analogy.

 Akizungumzia matayarisho ambayo yamefanywa na Wizara yake katika kuukabili mfumo mpya wa Matangazo ya Dijitali Waziri Mbarouk amesema tayari wamejenga kituo cha usambazaji ishara(signals) katika eneo la Rahaleo kitakachokuwa na kazi ya kupokea na kusambaza ishara na mitambo ya uendeshaji.

 Aidha Wizara imetayarisha maeneo matatu Unguja ambayo ni Kizimkazi,Masingini na Nungwi ambapo kwa upande wa Pemba ni Kichunjuu,Mkanjuni na Konde kwa ajili ya kurushia matangazo ya Dijitali.

Matayarisho mengine ni pamoja na kuandaa utaratibu mzuri wa upatikanaji wa Ving’amuzi na maudhui kwa bei nafuu ambapo amesema vitaanza kuuzwa mwishoni mwa mwezi wa Januari mwakani.

Amefahamisha kuwa bei ya Ving’amuzi hivyo itakuwa rahisi kuliko vingamuzi vingine ambapo mwananchi atatakiwa kukinunua kwa Shl.50,000 na kukilipia shl.8,000 kwa mwezi ili kupata huduma ya matangazo hayo.

Amevielezea Ving’amuzi hivyo ambavyo vitakuwa na huduma mbali mbali ikiwemo Mtandao, Video on demand, programme guide, exclusive service yaani mawasiliano ya makundi maalum ambapo pia jumla ya Chaneli 36 za ndani na nje ya nchi zitapatikana kwa uhakika.

Waziri Mbarouk amesema uzinduzi wa mitambo na matangazo ya Dijitali unatarajiwa kufanyika wakati wa sherehe za Mapinduzi Januari 8 mwakani katika maeneo ya Rahaleo mjini Zanzibar.
 Mabadiliko ya Mfumo wa matangazo kutoka Analogia kwenda Dijitali yamekuja kufuatia agizo lililotolewa na Shirikisho la Mawasiliano la Afrika Mashariki EACO kuwa Nchi wanachama wa Shirikisho hilo ziwe zimehamia katika mfumo mpya wa Dijitali ifikapo mwaka 2013.

No comments:

Post a Comment