Monday, December 31, 2012

BAADA YA KUPIGA PICHA NA LEMA, ASKARI JESHI ATOWEKA KAMBINI.

JESHI la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), limesema askari anayedaiwa kuwa jeshi hilo aliyepiga picha na Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema ametoroka.

Msemaji wa JWTZ, Kanali Kapambala Mgawe alisema jana kwamba pamoja na hatua yake ya kutoroka, jeshi litaendelea kumsaka kwa udi na uvumba ili kumhoji na kujiridhisha kama kweli ni mwanajeshi wake kabla ya kumchukulia hatua za kinidhamu kwa mujibu wa Kifungu cha 147 cha Katiba ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania ya 1977.

“Huyu kijana inasemekana alishawahi kupitia Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), lakini wakati tunaendelea na uchunguzi alitoroka katika nyumba aliyokuwa amepanga bila ya taarifa kwa baba mwenye nyumba,” alisema Kanali Mgawe na kuongeza:

“Askari huyo alikuwa anaishi katika nyumba ya kupanga mita chache karibu na Kituo cha Polisi cha Simanjiro, Arusha na alikuwa akijishirikisha na ulinzi shirikishi.”

Alipoulizwa jina la askari huyo, Kanali Mgawe alijibu: “Yeye alikuwa anafahamika mtaani hapo kwa jina la kamanda.”

Hata hivyo, Kanali Mgawe alisema jeshi hilo litahakikisha linatoa ripoti kamili kwa umma baada ya kumkamata na uchunguzi kukamilika ili kuondoa utata uliogubika suala hilo.

Alifafanua kuwa iwapo mwanajeshi atateuliwa kufanya kazi katika taasisi yeyote ya Serikali nje ya jeshi, atatakiwa kuvua magwanda ya jeshi na kufanya kazi hiyo mpaka atakapomaliza muda wake na baada ya hapo ataruhusiwa kurejea jeshini.

“Kuna kitu kinaitwa ‘secondment.’ Mwanajeshi anaruhusiwa kufanya shughuli zozote nje ya jeshi iwapo atahitajika kufanya hivyo. Ila kwa masharti ya kuvua magwanda, hivyo wananchi wasishangae kuwaona baadhi ya askari wetu ni wakuu wa wilaya na mikoa na baadaye kurudi jeshini kuendelea na majukumu yao,” alisema Kanali Mgawe na kuongeza:

“Askari akiwa katika majukumu yake mapya, atafanya kazi zote atakazopewa zikiwamo za kisiasa kama ilivyo kwa wakuu wa wilaya na mikoa, lakini akirudi jeshini, anarudi kuwa askari mwenye utii na kufuata kanuni za jeshi zisizofungamana na siasa.”
Mbunge wa jimbo la Arusha mjini, Godbless Lema akiwa na askari wa JWTZ anayedaiwa kutoroka, baada ya tukio la kupiga picha.

UZINDUA RASMI WA MATOKEO YA SENSA YA WATU NA MAKAZI.

Bango linaloonyesha Idadi ya watu wote Watanzania, baada ya kuhesabiwa katika zoezi la kuhesabu Sensa lililoanza mwezi Agosti mwaka huu na kufikia tamati hii leo wakati Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Kikwete, alipotangaza rasmi matokeo ya Senza ya watu na makazi na kutaja idadi kamili, wakati wa hafla hiyo iliyofanyika leo katika Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.

Rais Jakaya Kikwete, akizungumza na wananchi wakati akisoma hotuba yake ya kutangaza rasmi uzinduzi wa matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi, leo katika Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam. Rais Jakaya, alisema kuwa katika Sensa ya mwaka huu, watanzania wameongezeka kwa asilimia kubwa ukilinganisha na Sensa iliyofanyika kwa mara ya kwanza nchini ya mwaka 1967, ambapo Watanzania wote walikuwa ni Milioni 12, 313, 054, na Tanzania Bara walikuwa ni milioni 11, 958,654 na Visiwani Zanzibar, walikuwa ni 354, 400, ambapo baada ya mwaka huo, Sensa kama hiyo ilifanyika tena mwaka 1978, 1988,2002 na hii ya mwaka huu 2012, ambapo imetoa idadi ya Watanzania wote kuwa ni jumla ya Milioni 44, 929,002. 
Baadhi ya Madiwani na viongozi mbalimbali wa Serikali, waliohudhuria katika hafla hiyo leo.

Kikundi cha Uhamasishaji cha Temeke, akikiwa ni miongoni mwa wageni waalikwa kilichokuwa kikiendelea na kazi yake ya uhamasishaji uwanjani hapo.

Sehemu ya wananchi waliojitokeza kuhudhuria hafla hiyo.

Picha ya pamoja kwa kumbukumbu.

Rais Jakaya Kikwete, akiteta jambo na Mwenyekiti wa CUF, Ibrahim Lipumba, wakati akiondoka katika viwanja vya Mnazi Mmoja, baada ya kuzidua rasmi matokeo ya Sensa ya watu na makazi.

TUME YA MABADILIKO YA KATIBA, KATIKA PICHA.

NAIBU Katibu wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Bw. Casmir Kyuki (kushoto) akitoa ufafanuzi kuhusu kuhusu kazi na majukumu ya kitengo cha utafiti cha Tume hiyo kwa wajumbe wa kamati ya Katiba na Sheria ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati walipotembelea Ofisi za Makao ya Tume hiyo jijini Dar es Salaam Oktoba 16. Wa pili kushoto ni Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Bi. Angellah Kairuki na Katibu wa Tume Assaa Rashid (watatukulia).

Mjumbe wa Sekretarieti ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Bw. Ismail Ngayonga akitoa ufafanuzi kuhusu kaziza Tume hiyo kwa Sarah Houlihanna Anna Lingken kutokaTaasisi ya Kisheria ya Women’s Link Worldwide ya nchini Colombia wakati walipotembelea banda la Tume hiyo katika maadhimisho ya siku ya Haki za Binadamu duniani zilizofanyika katika Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.

Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Serikali, Bw. Mohammed Mtonga (wapili kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na Wajumbe wa Sekretarieti ya Tumeya Mabadiliko ya Katiba, wakiongozwa na Katibu waTume, Bw. Assaa Rashid (kushoto) na Naibu Katibu, Bw. Casmir Kyuki mara baada ya kufungua mafunzo ya kuwajengea uwezo wajumbe wakamati ya ukaguzi wa Tume hiyo kuhusu ukaguzi wa fedha za umma.

WAZIRI MKUU MIZENGO PINDA AMTEMBELEA BABA YAKE HOSPITALI YA MUHIMBILI MOI.

Waziri Mkuu Mizengo Pinda akimjulia hali Baba yake mzazi Mzee Savere Kayanza Pinda ambaye amelazwa katika hospitali ya Taifa Muhimbili  kitengo cha Moi Mzee Mizengo yupo hospitalini hapo baada ya kufanyiwa upasuaji kutokana na tatizo la nyonga kulia kwa Waziri Mkuu ni muguzi mkuu wa zamu wodi hiyo, Edna Mhina  na kushoto kwa waziri mkuu ni  Donatila Kwelukila ambaye ni ofisa muuguzi chumba cha wagonjwa mahututi.

Taarifa kwa Umma:USITISHAJI WA MATANGAZO YA ANALOJIA NA KWENDA KATIKA MFUMO WA DIJITALI.

TAARIFA YA MHE. JANUARY Y. MAKAMBA (MB), NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO, SAYANSI NA TEKNOLOJIA KUHUSU USITISHAJI WA MATANGAZO YA ANALOJIA NA KWENDA KATIKA MFUMO WA DIJITALI.
Ndugu Wananchi,



Mtakumbuka kuwa hapo tarehe 23 Februari 2012 tuliwatangazia kupitia vyombo vya habari juu ya usitishwaji wa matangazo ya televisheni kwa kutumia teknolojia ya analojia kwenda katika mfumo mpya unaotumia teknolojia ya dijitali.



Napenda kuwaleleza kuwa, maandalizi ya kuzima mitambo ya analojia kuanzia tarehe 31 Desemba 2012 yamekamilika kwa mujibu wa makubaliano ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.



Hata hivyo, napenda sasa kutoa taarifa kuwa uzimaji wa mitambo ya analojia utafanyika kwa awamu kama ifuatavyo:-



(1) Dar Es Salaam-31 Desemba, 2012;

(2) Dodoma & Tanga- 31 Januari, 2013;
(3) Mwanza-28 Februari, 2013;
(4) Moshi & Arusha-31 Machi, 2013;
(5) Mbeya-30 Aprili, 2013.

Tumeamua kuanza kuzima mitambo hiyo kwa Jiji la Dar es Salaam kwanza ili kutoa fursa kwa makampuni yenye leseni kusimika mitambo ya utangazaji wa dijitali katika mikoa mingine. Makampuni haya yamejipanga kukamilisha usimikaji wa mitambo hiyo katika mikoa minane katika miezi minane ijayo.



Mitambo ya analojia itakayozimwa kesho ni ile iliyopo Kisarawe na Makongo. Vituo ambavyo siku ya tarehe 1 Januari 2013, vitapaswa kuanza kutangaza matangazo kwa mfumo wa dijitali ni TBC1, ITV, EATV, Channel 10, StarTV, DTV, CapitalTV, TumainiTV, ATN, MlimaniTV, C2C, CTN, CloudsTV na Efatha.



Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) inafanya jitihada za kutosha kuhakikisha kwamba makampuni yenye leseni za kusambaza ving’amuzi yanakuwa na ving’amuzi vya kutosha na vingine vimeagizwa ili kukidhi mahitaji ya baadaye na vile vilivyopo sokoni vina ubora unaokubalika.



Vilevile, Serikali kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania itahakikisha kwamba zoezi la uhamaji linafanyika bila usumbufu na kero kwa wananchi. Makampuni yanayouza ving’amuzi yameagizwa yaimarishe huduma kwa wateja wakati wa kuuza ving’amuzi na hata baada ya ununuzi iwapo wananchi watakuwa na matatizo na ving’amuzi.



Zoezi hili la uhamaji ni muhimu sana kwa maendeleo ya nchi yetu. Tutakapokuwa tumekamilisha uhamaji, huduma za mawasiliano na utangazaji zitapanuka na kuwa bora zaidi. Kwa mfano, itawezekana sasa kuangalia televisheni kupitia simu zetu za mikononi. Vilevile, itawezekana, kwa bei nafuu kabisa, kwa mtu mwenye uwezo wa kutengeneza vipindi kukodisha chaneli yake na kutangaza vipindi vyake. Vilevile, bei za mawasiliano na utangazaji zitashuka, na tutakuwa tumepiga hatua kubwa kwenye mapinduzi ya teknolojia duniani, ambayo nchi yetu haiwezi kubaki nyuma.



Ndugu Wananchi,



Serikali kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania itaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu uhamaji huu. Serikali inatarajia kupata ushirikiano wa karibu kutoka kwa wadau wa sekta ya utangazaji na wananchi kwa ujumla katika kipindi cha uzimaji wa mitambo ya utangazaji wa televisheni ili kufanikisha zoezi la uzimaji wa mitambo ya utangazaji ya teknolojia ya analojia.



Uhamaji huu hautahusu televisheni za wananchi zinazopata matangazo kupitia madishi (nyungo) (satellite) au nyaya (cables). Hivyo, wananchi wanaopata matangazo kupitia DStv, Zuku, na nyinginezo wataendelea kupata matangazo yao kama kawaida.



Ndugu Wananchi



Kama kuna mwananchi yoyote ana kero, malalamiko, swali au anahitaji maelekezo kuhusu uhamaji, awasiliane na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kupitia namba 0784-558270; 0784558271 au barua pepe: malalamiko@tcra.go.tz



Ndugu Wananchi,



Nawashukuru kwa kunisikiliza

Mhasibu Simba aporwa mamilioni ya mechi kati ya Simba na Tusker.

Zaidi ya Sh. milioni 10 za klabu ya Simba zimeporwa baada ya Mhasibu wa klabu hiyo, Erick Sekiete (28) kudai kuvamiwa na majambazi sita katika mtaa wa Sinza kwa Remmy na kuporwa kiasi hicho cha pesa juzi saa 3:20 usiku.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Charles Kenyela alisema kuwa Sh. milioni 7.59 na dola za Marekani 2,000 ambazo Simba walizipata baada ya makato ya mapato ya mechi yao dhidi ya Tusker FC ya Kenya iliyomalizika kwa wenyeji Simba kuchapwa 3-0 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

 
Alisema kuwa baada ya kukabidhiwa fedha hizo, Sekiete na mwenzake Stanley Phillipo (23) ambaye alidaiwa kuwa ni mwanafunzi, walipanda kwenye gari aina ya Toyota Premio yenye namba za usajili T869 BKS lililokuwa likiendeshwa na Said Pamba na kwamba walipofika eneo hilo, dereva aliwashusha na kwamba wakaanza kutafuta teksi.

Aliendelea kueleza kuwa muda mfupi baada ya kushushwa, Sekiete na Philipo waliamua kuvuka upande wa pili wa barabara iendayo Kijitonyama ili wachukue teksi lakini ghafla  walitekwa na watu sita walioshuka kutoka kwenye pikipiki tatu.

Aliendelea kufafanua kuwa wakati watu hao wakimnyang’anya begi Sekiete walikuwa wakitamka maneno ya kejeli kwa uongozi wa Simba.

Kamanda Kenyela alisema kuwa baada ya watu hao kupora fedha hizo, walitokomea kusikojulikana na hadi sasa, Jeshi la Polisi linawashikilia watu watatu akiwamo Sekiete kuhusiana na tukio hilo.

Watu wengine wanaoshikiliwa na jeshi hilo katika Kituo cha Polisi Magomeni ni Pamba na Philipo ambao walikuwa pamoja na Sekiete kwenye gari.

 
Mwenyekiti wa Simba, Aden Rage amesema hapo jana kuwa amesikitishwa na taarifa za kuporwa kwa fedha za klabu yao.
Kamanda mkoa wa Temeke, Charles Kenyela.
 

KESI YA SHEIKH PONDA YAPIGWA TENA KALENDA KUTOKANA NA MASHAHIDI KUTOFIKA MAHAKAMANI LEO.


Katibu Mkuu  wa
Jumuiya
na Taasisi za Kiislamu nchini, Sheikh Ponda Issa Ponda akiingia katika
chumba cha Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam leo
pamoja na washtakiwa wenzake 49, hata hivyo kesi hiyo imeahirishwa
kutokana na mashahidi upande wa mashtaka kutofika mahakamani hapo.

Katibu Mkuu  wa  Jumuiya na Taasisi za Kiislamu nchini, Sheikh Ponda Issa Ponda akiwa na mshtakiwa mwenzake,  Mukadam Abdal Swalehe (kushoto).

Baadhi ya wafuasi wa Sheikh Ponda wakiwa katika viunga vya mahakama ya Kisutu.

Katibu Mkuu  wa  Jumuiya na Taasisi za Kiislamu nchini, Sheikh Ponda Issa Ponda na mshtakiwa mwenzake Mukadam Abdal Swalehe wakitoka mahakamani chini ya ulinzi wa askari magereza.



Ulinzi uliimarishwa katika eneo la Mahakama ya Kisutu leo.



 Katibu Mkuu  wa  Jumuiya na Taasisi za Kiislamu nchini, Sheikh Ponda Issa Ponda (kulia) akiwa na washtakiwa wenzake.

Salamu Za Kuukabirisha Mwaka Mpya Wa 2013 Kutoka Kwa Dk. Shein.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi. Dk Ali Mohamed Shein,akitoa salamu za kuukaribisha Mwaka mpya wa 2013,kwa wananchi wa Zanzibar na Watanzania wote kwa ujumla,pia aliwasihi wananchi kuendela kushirikiana   na Serikali yao katika kuendeleza mipando mbali mbali ya maendeleo,na kuwataka kuwa walinzi wa rasilimali pia kuzingatia   taratibu za kisheria, kwa kuwa na elimu bora ya rasilimali hizo. 
Rais wa zanzibar, Dk.Ali Mohammed Shein.
 

 [Picha na Ramadhan Othman,Ikulu.]

Sunday, December 30, 2012

WANA-TANGA WAAOMBWA KUCHANGIA UJENZI WA BARABARA YA KWEMATINDI-GARE.

WAKAZI wa Kijiji cha Gare, Kata ya Magoroto, Wilaya ya Muheza, mkoani Tanga, wanaomba wadau na wananchi wenye mapenzi mema kuchangia ujenzi wa barabara ya Kijiji cha Kwematindi hadi Gare, kwa kuwa inachangia kuzorotesha uchumi wao.

Mkakati wa kuomba msaada wa ujezni wa barabara hiyo umeanza baada ya kuona Serikali ya Kijiji na Kata hawana mpango wa kuendeleza kijiji hicho ambacho hakina barabara tangu uhuru.

Barabara hiyo imekuwa kikwazo cha shughuli nyingi za kiuchumi, hasa kipindi cha masika, hali inayohitaji jitihada za haraka kuijenga kwa maslahi ya wananchi wa kijiji hicho na Taifa kwa ujumla.

Lakini kutokuwepo kwa barabara hiyo imekuwa ni chanzo cha umasikini kwa wakazi wa kijiji hicho ambao wengi wao ni wakulima na wanashindwa kufanya shughuli zao za kuinua uchumi kutokana na miundombinu ya barabara ambayo imekuwa ikiwakwamisha kusafirisha bidhaa zao na wananchi kushindwa kufika kijijini kwa urahisi.
 
Ni moja ya mabasi mkoani Tanga linalotumia barabara hiyo.
Kukosekana kwa barabara hiyo kumewanyima wanakijiji fursa ya kupata huduma za jamii kama vile shule na hospitali hali inayochangia kurudi nyuma kimaendeleo.

Barabara hiyo korofi na isiyopitika kwa magari wala pikipiki, inahitaji kuchongwa kwa gharama ya Sh Mil 13,120,000 hali ambayo imekuwa ngumu kwa kuwa wanakijiji wengi hawana uwezo huo kutokana na kukosa kipato na hivyo ni muda muafaka kwa wananchi, hasa wanaoishi Dar es Salam watokao mkoani Tanga, kusaidia harakati za ujenzi wa barabara hii, kwa kuwa baada ya mambo yote nyumbani ni muhimu.

WAENDESHA PIKIPIKI WA MKOA WA MWANZA WAIOMBA SERIKALI IWAPE MAFUNZO NA MKOPO.

UMOJA wa waendesha pikipiki wa mkoa wa Mwanza wameiomba Serikali kuwapa mafunzo ya uongozi pamoja na mikopo yenye masharti naafuu ili waweze kununua pikipiki zao binafsi na kujiajiri wenyewe nahivyo kujiinua kiuchumi tofauti na ilivyo sasa kwani wengi wao wameajiriwa na hivyo kuwatajirisha waajiri wao.
Baadhi ya waendesha pikipiki wa jiji la mwanza, maarufu kama BodaBoda wakiwa ndani ya sare zao za kazi.
Waendesha pikipiki hao ambao wengi wao ni vijana wametoa ombi hilo hivi karibuni wakati wakiongea na Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Maendeleo ya Vijana James Kajugusi wakati alipowatembelea ofisini kwao maeneo ya Mlango mmoja jijini Mwanza ili kuona shughuli zinazofanywa na umoja huo.
Akiongea kwa niaba ya wenzake Mwenyekiti wa Umoja huo Makoye Bunoro alisema kuwa kuna makampuni yanayokopesha pikipiki kwa riba kubwa jambo linasababisha mkopaji kuchukua muda mrefu wa kulipa deni na kutokupata faida na kuyaomba makampuni hayo yakopeshe kwa riba ndogo ila nao wapate faida.

Aliendelea kusema kuwa chama hicho kinasimamia upatikanaji wa leseni, hadi sasa waendesha pikipiki 2034 ambao ni wanachama na siyo wanachama wameshapata leseni pamoja na mafunzo yaliyotolewa na Chuo cha ufundi VETA kwa gharama naafuu jambo ambalo limeweza kupunguza kwa kiasi kikubwa ajali za barabarani zinazotokana na waendesha pikipiki katika mkoa huo.
Wilaya ya Magu waliopata mafunzo na leseni ni 190, Sengerema 172, Misungwi 57, Ukerewe 106, Kwimba 28, Nyamagana na Ilemela 1484.
Kwa upande wake Mkurugenzi Kajugusi aliwataka vijana hao kuimarisha umoja wao na kutokubali kutumiwa na makundi ya watu kwa manufaa ya watu hao kwani vijana wananguvu za kutosha hivyo watu wengi wanapenda kuwatumia, bali wao watumie nguvu zao kutafuta ajira ambazo zitawainua kiuchumi na kuleta maendeleo ya nchi yao.
Alisema kuwa Serikali iliamua kuruhusu pikipiki kuwa chombo cha kuendesha abiria ili zisaidie katika masuala ya usafirishaji na kuongeza fursa ya upatikanaji wa ajira binafsi kwa vijana ili waweze kujiajiri wao wenyewe hivyo watambue kuwa biashara wanayoifanya ni halali jambo la muhimu ni kufuata sheria zilizopo.
Alimalizia kwa kusema kuwa Idara ya vijana kwa kupitia vituo vyake vya kuwajengea uwezo vijana itaangalia uwezekano wa kutoa mafunzo kwa viongozi wa wapanda pikipiki wa wilaya ili wakawafundishe wenzao.
Umoja huo ulianzishwa mwezi wa pili mwaka 2011 na unajumla ya wanachama waliosajiliwa 1034 kutoka wilaya za Nyamagana 484, Ilemela 204, Sengerema 87, Ukerewe 51, Magu 123, Misungwi 57 na Kwimba 28.

IBF YAMPONGEZA CHEKA KWA KUTWAA UBINGWA.

Shirilisho la Ngumi la Kimataifa (IBF) limepongeza bingwa mpya wa uzito wa Super Middle katika bara la Afrika, Ghuba ya Uajemi na Mashariki yaa Kati, Mtanzania Francis Cheka.

Katika barua yake aliyomtumia Francis Cheka ya tarehe 28/12/2012 Mwenyekiti wa kamati ya Ubingwa wa IBF/USBA Lindsey Tucker alisema "Tunachukua fursa hii kukutakia maisha na mafanikio mazuri kama bingwa wa IBF na kumhimiza kuishi kama bingwa". 
 
Cheka atatakiwa kutetea taji lake katika kipindi cha miezi sita kufikia mwezi wa 6 mwakani dhidi ya mpinzani ambaye ana rekodi ya mapambano yasiyopungua 15 na mengi awe ameyashinda hususan mapambano mawili ya mwisho.

Aidha IBF inampongeza bondia Chiotcha Chimwemwe kutoka Malawi kwa ushupavu wake na ushindani mzuri katika pambano hilo lililofanyika katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid katika jiji la Arusha tarehe 26 Desemba, 2012.
Bondia Francis Cheka baada ya ushindi.
 

SIMBA SC YAONDOKA KESHO DAR, KUELEKEA VISIWANI ZANZIBAR.

KIKOSI cha Simba SC kinaondoka kesho Dar es Salaam kwenda Zanzibar kwa ajili ya michuano ya Kombe la Mapinduzi, michuano inyaonza Jumanne.
Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ alisema jana kwamba timu hiyo itakuwa huko hadi baada ya mashindano, Januari 12 ndipo itaenda Oman kwa ziara ya wiki mbili.
Simba SC jana ilicheza mechi ya kujipima nguvu na kufungwa mabao 3-0 na Tusker ya Kenya kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Katika mchezo huo, uliochezeshwa vema na refa Hashim Abdallah, hadi mapumziko, tayari Tusker walikuwa mbele kwa mabao 2-0, yaliyotiwa kimiani na Jesse Were dakika ya 37 na 45.
Mabao yote yalitokana na udhaifu wa safu ya ulinzi ya Simba, ambayo hii leo iliongozwa na beki kutoka Mali, Komabil Keita kiasi cha kufikia mfungaji anafunga akiwa amebaki anatazamana na kipa.
Simba ilikuwa ikishambulia kutokea pembeni, lakini mipira mingi mirefu iliyokuwa inamiminwa langoni mwa Tusker ilikuwa inaokolewa na mabeki warefu wa klabu hiyo bingwa ya Kenya, wakiongozwa na beki wa zamani wa Yanga, Joseph Shikokoti.
Kipindi cha pili, Tusker walirudi kwa nguvu tena na kufanikiwa kupata bao la tatu dakika ya 54, mfungaji Frederick Onyango.
Simba pamoja na kufanya mabadiliko, ikiwatoa Haruna Shamte, Haruna Athumani, Paul Ngalema, Mussa Mudde, Abdallah Seseme, Abdallah Juma, Ramadhani Chombo na Kiggi Makassy na kuwaingiza Miraj Adam, Hassan Isihaka, Emily Ngeta, Jonas Mkude, Salim Kinje, Haruna Moshi, Ramadhani Singano, Nassor Masoud ‘Chollo’ na Edward Christopher, haikuweza kupata hata bao la kufutia machozi.
Nassor Masoud aliingia kuchukua nafasi ya Shamte, lakini naye akaumia na kutoka nafasi yake ikichukuliwa na kinda wa Simba, B, Masele Kaheza.
Baadhi ya wachezaji wa Simba SC.

KLABU ZASUBIRI FEDHA ZAO TRA ZICHEZE LIGI KUU.

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Desemba 28, 2012

Klabu 14 ambazo timu zao zinashiriki Ligi Kuu ya Vodacom zimesema hazitacheza hatua ya pili ya Ligi hiyo inayotarajiwa kuanza Januari 26 mwakani hadi zitakaporejeshewa fedha zao zilizochukuliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kutoka kwenye moja ya akaunti za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

Novemba 23 mwaka huu, TRA kwa uwezo ilionao kisheria iliielekeza benki ya NMB kuilipa fedha hizo (sh. 157,407,968) kutoka kwenye moja ya akaunti za TFF ikiwa ni Kodi ya Lipa Kama Unavyopata (PAYE) kutoka kwenye mishahara ya waliokuwa makocha wa timu za Taifa.

Serikali ndiyo inayolipa mishahara ya makocha hao moja kwa moja kwenye akaunti zao, lakini ilikuwa haikati PAYE kutoka kwenye mishahara hiyo, hivyo malimbikizo kufikia sh. 157,407,968.

TFF bado inaendelea na mazungumzo na pande husika (Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kwa upande mmoja na TRA kwa upande mwingine) ili fedha hizo zirejeshwe kwani zilitolewa na mdhamini wa Ligi Kuu (kampuni ya Vodacom) kwa ajili ya maandalizi ya timu hizo tayari kwa mzunguko wa pili wa Ligi hiyo.

OFISA WA CAF KUTUA MWAKANI KUKAGUA VIWANJA
Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) litamtuma nchini ofisa wake Abbas Sendyowa kukagua viwanja na hoteli ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa utaratibu wa klabu kupata leseni zitakazoziwezesha kushiriki michuano inayoandaliwa na Shirikisho hilo.

Ofisa huyo kutoka Uganda atawasili nchini Januari 7 mwakani ambapo anatarajiwa kukamilisha kazi hiyo Januari 14 mwakani na baadaye kupeleka ripoti yake CAF.

Utekelezaji wa kazi yake nchini utahusisha mwakilishi kutoka TFF, mwakilishi kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, mameneja wa viwanja husika na Ofisa Usalama wa TFF.

NAZARIUS KILUNGEJA AONDOLEWA UCHAGUZI RUREFA
Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imekubaliana na uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi ya Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Rukwa (RUREFA) kumuondoa Nazarius Kilungeja kugombea uenyekiti katika uchaguzi wa chama hicho.

Kutokana na uamuzi huo, Kamati ya Uchaguzi ya TFF imeiagiza Kamati ya Uchaguzi ya RUREFA kuendelea na mchakato wa uchaguzi huo kama ilivyopangwa awali.

Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

IBF YAMTANGAZA LUCAS RUTAINURWA WA KITWE GENERAL TRADERS KAMA PROMOTA WA MWAKA 2012.

Shirikisho la Ngumi la Kimataifa (IBF) katika bara la Afrika, Ghuba ya Uajemi na Mashariki ya Kati limemtamngaza bwana Lucas Rutainurwa wa kampuni ya Kitwe General Traders ya jijini Dar-Es-Salam kama Promota wa mwaka 2012.

Akitangaza habari hizi, Rais wa IBF katika bara la Afrika, Ghuba ya Uajemi na Mashariki ya Kati Mtanzania Onesmo Ngowi alisema kuwa bwana Lucas Rutainurwa alifanikisha Watanzania wawili kuwa mabingwa wa IBF katika bara la Afrika, Ghuba ya Uajemi an Mashariki ya Kati mwaka unaoishia Desemba 2012.

Katika harakati zake za kuipa Tanzania sura ya kimataifa katika tasnia ya ngumi za kulipwa Rutainurwa na kampuni yake ya Kitwe General Traders waliandaa mapambano makubwa mawili ambayo yalizidi maandalizi ya mapambano yote yaliyowahi kufanyika Tanzania kwa miaka ya karibuni.

Mwezi April mwaka 2012, Rutainurwa na Kitwe General Traders waliandaa pambano lililowakutanisha mabondia Francis Cheka na Mada Maugo wote wa Tanzania kugombea mkanda wa IBF bara la Afrika, Ghuba ya Uajemi na Mashariki ya Kati katika ukumbi wa PTA jijini Dar-Es-Salaam. Katika mpambano huo bondia Francis Cheka aliibuka kidedea baada ya kumsimamisha Maugo katika raundi ya nane.

Francis Cheka alitetea vyema mkanda wake huo tarehe 26 Desemba jijini Arusha alishinda kwwa points bondia Chimwemwe Chiotcha kutoka nchini Malawi katika pambano lao la raundi 12.
 Mwezi wa nane mwaka 2012, Rutainurwa na Kitwe General Traders waliandaa mpambano mwingine kati ya bondia Ramadhani Shauri wa Tanzania na Sunday Kizito kutoka Uganda kugombea mkanda wa IBF katika bara la Afrika, Ghuba ya Uajemi na Mashariki ya Kati katika uzito wa Unyoya (Featherweight).

Katika mpambano huo bondia Ramadhani Shauri wa Tanzania alimsimamisha Sunday Kizito kutoka Uganda katika raundi ya 9 na kutangazwa kuwa bingwa mpya wa IBF.

Kupatikana kwa mabingwa hao, kumeifanya Tanzania kuwa nyumbani kwa mabingwa wawili wa IBF na hivyo kuiweka nchi hii katika ngazi moja na chache duniani hususa katika bara la Afrika zikiwemo Afrika ya Kusini, Ghana, Morocco, Algeria na Cameron.

Shirikisho la Ngumi la Kimataifa lina makao yake makuu yanayoratibu bara la Afrika, Ghuba ya Uajemi na Mashariki ya Kati kutokea katika jiji la Dar-Es-Salaam, Tanzania.

Hii ni heshima ya kipekee kwa nchi ya Tanzania kwani nchi nyingi zinagombania kuwa makao makuu ya shirikisho hii kubwa kuliko yote duniani.

IBF imemshukuru sana bwana Lucas Rutainurwa na kampuni yake ya Kitwe General Traders kwa mafanikio haya mazuri.

Bwana Lucas atapewa tuzo
yake la kuwa promota wa mwaka wa IBF katika bara la Afrika mwaka 2012 rasmi wakati wa mkutano wa 30 wa IBF/USBA utakaofanyika katika jiji la Berlin, nchini Ujerumani Mai mwakani.

Branco Milenkovik wa kampuni ya  Branco Sports Productions  ya Johannesburg Afrika Kusini aliyeteuliwa na IBF kwa mwaka 2012.

Katika hatua nyingine:

Bwama Michael Tetteh na bwana Henry Many-Spain wa GoldMike Promotions and Golden Concept za jiji la Accra, Ghana wameteuliwa kama promota wa mwaka 2012 wa mapambano ya IBF ya mabara. Bwana Tetteh amepromoti mapambano mengi ya IBF ya mabara (Continental Titles) kuliko promota mwingine yeyote katika bara la Afrika.

Aidha, IBF imemteua bwana Branco Milenkovik wa kampuni ya Branco Sports Productions ya jiji la Johannesburg, nchini Afrika ya Kusini kama promota wake wa mwaka wa mapambano ya dunia mwaka 2012. Hii ni mara ya 3 mfululizo kwa Branco kuteuliwa kama promota wa mwaka kwa kuandaa mapambano mengi ya IBF ya ubingwa wa dunia.

Matokeo ya Sensa hadharani kesho.

MATOKEO ya Sensa ya Watu na Makazi iliyofanyika Agosti 26, mwaka huu yanatarajiwa kutangazwa kesho na Rais Jakaya Kikwete, katika hotuba yake ya mwisho wa mwaka kwa Taifa.

Kazi hiyo ya maandalizi ya matokeo hayo ya Sensa iliyofanyika kwa zaidi ya miaka saba, inatarajiwa kufanyika jijini Dar es Salaam, katika viwanja vya Mnazi Mmoja, ambapo utafanyika uzinduzi wake.

Akizungumza na MTANZANIA Jumapili, Kamishna wa Sensa ya Watu na Makazi, Hajat Amina Mrisho, alisema kazi ya kuingiza takwimu imekamilika mapema mwezi huu, ambapo pamoja na mambo mengine ripoti hiyo ya matokeo wanatarajiwa kuikabidhi kwa Rais Kikwete kesho.

“Ofisi ya Taifa ya Takwimu, imejipanga kikamilifu katika hili na ratiba yetu tuliyoitoa hadi sasa imekwenda vizuri kwani kazi kubwa ilikuwa ni kuingiza Data, katika vifaa maalum na hivi sasa tumekamilisha na kesho Mungu akipenda ripoti tutaikabidhi kwa Rais Kikwete.

“Sensa ya mwaka huu imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kwa zaidi ya asilimia 95, kwa upande wa Tanzania bara, hasa baada ya zoezi hili tulilazimika kuongeza muda wa wiki moja zaidi kwa lengo la kufanya kazi nzuri kwa maslahi ya Taifa letu.

“Uzinduzi wa ripoti hii ya Sensa tutaufanya kesho Desemba 31, katika viwanja vya Mnazi Mmoja kama tulivyopanga na hivi sasa tupo katika maandalizi ya mwisho kuweza kukamilisha jambo hili liwe na ufanisi wa hali ya juu kuliko Sensa zilizotangulia.

“Kama unavyofahamu Ofisi ya Taifa ya Takwimu Tanzania (NBS), awali tulitangaza kuongeza wiki moja kutoka Agosti 30 hadi Septemba 8, kwani hata siku tulizoongeza zilikuwa na mafanikio ambapo kila aliyekuwa na haki ya kuhesabiwa alifikiwa na makarani wetu,” alisema Hajat Amina.

Akizungumzia kuchelewa kwa matokeo ya Sensa, Kamishna huyo wa Sensa, alisema NBS ilipanga ratiba tofauti na wananchi walivyokuwa wanafikiria, kwani tangu awali walitangaza matokeo yangetangazwa Desemba 31, na Rais Kikwete, katika hotuba yake ya kufunga mwaka 2012.

“Nataka niwaeleze Watanzania kuwa, Sensa ya mwaka huu imefanyika katika kipindi kifupi hadi kufikia hatua ya kutangazwa kwa matokeo.

“Sensa zilizopita tulikuwa tunakaa zaidi ya mwaka mmoja hadi kutoka matokeo yake. Safari hii NBS tulijipanga kikamilifu na tulihakikisha tunakuwa na vifaa vya kisasa ambavyo vimesaidia kazi hii kufanyika kwa miezi minne tu.

“Tunawaomba Watanzania waondoe hofu katika hili na kadri tutakavyokuwa tunafanya Sensa zetu tunaweza tukawa tunakwenda kwa muda mchache zaidi.

“Huenda katika Sensa ijayo ya mwaka 2022 itakuwa ni nzuri zaidi hasa kutokana na kila siku kuzaliwa kwa teknolojia mpya na za kisasa,” alisema.

Kutokana na hali hiyo alisema kuwa, zoezi hilo litakuwa na mchakato, ambapo baada ya kutangazwa matokeo hayo na Rais Kikwete, NBS itaanza kuchambua takwimu za kila mkoa, wilaya hadi kata na vijiji na kuzisambaza kwa wadau wa maeneo husika kwa ajili ya kuzifanyia kazi katika shughuli zao za kila siku.

“Awali tulianza na kazi ya kutenga maeneo ya kuhesabia watu kwenye kila kijiji na wilaya kwa nchi nzima, na hata kulazimika kurudi tena pale ambapo tulipohisi ramani zetu zimeharibika hasa mvua kubwa zinapoharibu miundombinu ya eneo husika.

Hajat Amina, alisema pamoja na kazi hiyo kukumbana na changamoto kadhaa, Sensa imefanyika kwa umakini wa hali ya juu na kwamba iligharimu Sh bilioni 140, hadi kukamilika kwake.

“Malengo ya Maendeleo ya Milenia, ambayo pia yanatekelezwa na Serikali yanahitajika yafanyiwe tathmini hapo ifikapo mwaka 2015. Bila ya shaka mnafahamu kuwa tathmini ya mikakati hiyo, malengo hayo ya milenia na mipango mingine ya kuimarisha hali ya maisha, haiwezi kufanyika bila ya kuwepo taarifa za uhakika na zilizo sahihi. Huo ndio ukweli,” alisema Hajat Amina.

Kwa upande wake Ofisa Uhamasishaji wa Sensa, Said Ameir, alisema pamoja na maandalizi hayo Sensa ya mwaka huu ilikumbana na changamoto kadhaa ikiwemo matishio ya baadhi ya jamii kutangaza kugomea Sensa, lakini baada ya kupatiwa elimu ya muhimu wa kazi hiyo waliweza kushiriki kikamilifu.

“NBS tulikabiliwa na kadhaa katika kazi hii hasa katika siku ya kilele cha Sensa Agosti 26, mwaka huu ambapo kuna baadhi ya maeneo yalikumbwa na changamoto za kuchelewa vifaa kwa makarani wetu.

“Mbali na hilo pia hata sare kwa ajili ya maafisa wa sensa na upungufu wa fomu za sensa ambazo zilichelewa, lakini baada ya muda katika maeneo yote nchi nzima vifaa vyote viliweza kukamilika.

“Hata hapa makao makuu, tuliweka pamoja mfumo mzuri wa usambazaji, lakini baadhi hawakuufuata. Hivyo, vifaa kwa ajili ya mahali fulani vilipelekwa mahali pengine hii nayo ilikuwa ni sababu ya kukosa fomu za kutosha kwa wakati huo,” alisema Ameir.

Polisi wadaiwa kughushi nyaraka Ofisi ya AG.

POLISI wametajwa kuwa miongoni mwa taasisi za dola ambazo zimekuwa zikisaidia kukua kwa vitendo vya ujangili katika hifadhi za taifa, mapori ya akiba na maeneo mengine.
Katika tukio la karibuni, polisi katika Wilaya ya Serengeti mkoani Mara, wanadaiwa kwamba walighushi nyaraka za Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na kuziwasilisha mahakamani kwa lengo la kuwaachia huru watuhumiwa waliokuwa na kesi ya kukutwa na silaha kinyume cha sheria.

Watuhumiwa hao ni wale wanaodaiwa kutumia silaha hizo kwa kufanya uwindaji haramu kwenye mbuga za wanyama kinyume cha sheria, huku mtandao mkubwa walionao katika vyombo vya dola ukichangia vitendo hivyo kuendelea.

Uchunguzi wa Mwananchi Jumapili ulibaini kuwa baadhi ya watuhumiwa, ambao wamewahi kunaswa na
kufikishwa mahakamani kwa tuhuma za ujangili, wametoweka katika njia za kutatanisha na kuacha kesi zikiendelea huku taarifa zikifikishwa mahakamani kwamba watuhumiwa hao wamefariki dunia.

Hata hivyo, mmoja wa watuhumiwa hao Malango Dusara aliyeripotiwa kufariki, anayekabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 3 ya 2010, mkoani Shinyanga kwa kukutwa na risasi 548, amekamatwa tena na sasa yuko mahabusu, baada ya kukutwa akiishi mitaani.

Wakati hayo yakiendelea katika mkondo wa mahakama, baadhi ya polisi wanadaiwa kushiriki uovu huo kwa kuharibu ushahidi wa kesi za watuhumiwa.

Imebainika kwamba, kuharibiwa kwa kesi hizo huanzia kwa polisi, ambao wanaandaa mashtaka na
hatimaye mahakamani, ambako inadaiwa watuhumiwa huachiwa na wakati mwingine, hukamatwa tena kwa makosa yaleyale wakiwa nje ya dhamana, lakini bado huachiwa tena.

Watuhumiwa hao sita wakazi wa Kigoma, Geita na Tabora ambao walikamatwa katika Kijiji cha Mbirikiri, wilayani Serengeti, mkoani Mara, Mei 12 mwaka huu, wakiwa na  bunduki nne za kivita aina ya SMG  na risasi 436.

Watuhumiwa hao ambao baadaye walifikishwa mahakamani majina tumeyahifadhi, ambapo baada ya kukamatwa walikabidhi silaha ambazo ni SMG mbili walizokuwa wamezificha eneo la Usinge,

Tabora na nyingine mkoani Kigoma na kumtaja mfadhili wao, anayewapa silaha (jina tunalo) ambaye ni mfanyabiashara na mkazi wa Busunzu Kibondo waliyedai anasambaza vijana hifadhi zote za Taifa kwa ajili ya kuua tembo na faru.

Mchakato wa mashtaka
Hata hivyo, baada ya kukamatwa mfanyabiashara huyo, kuliibua mvutano baina ya polisi wa mkoani Kigoma na wale wa Mara, ambao walikuwa wakitaka afikishwe Serengeti alikotajwa kwamba anafadhili ujangili, huku wale wa Kigoma wakipinga kwa sababu zisizofahamika.
IGP Said Mwema.

MADAKTARI 30 WASIMAMISHWA KAZI KWA MUDA.

BARAZA la madaktari Tanganyika limewasimamisha kwa muda madaktari 30, kutoa onyo kwa madakari 289 na kuwafutia mashtaka madaktari 49 baada ya kupitia malamamiko ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kufuatia mgomo wa madaktari uliotokea Juni 23 hadi 28 mwaka huu.

Taarifa iliyotolewa jana na Msemaji wa Wizara hiyo, Nsachris Mwamwaja imeeleza kuwa Baraza lilipitia malalamiko yote na limetoa adhabu stahiki kwa kila daktari aliyethibitishwa kushiriki katika mgomo huo.

Madaktari wakiwa katika chumba cha upasuaji.
Alisema mashtaka yaliyoahirishwa kutokana na wahusika kuhitaji ushauri wa kisheria ni madaktari wanne na mashtaka yasiyosikilizwa kutokana na wahusika kutofika walipoitwa na Baraza ni madaktari 22.

“Wizara inakamilisha taratibu za kinidhamu kwa mujibu wa Kanuni za  Utumishi wa Umma kwa Madaktari wote waajiriwa ambao walipatikana na hatia mbele ya Baraza la Madaktari,”aliseleza Mwamaja na kuongeza
“Wizara pia imeridhia kuwapa madaktari waliokuwa katika mafunzo kwa vitendo fursa nyingine ya kuendelea na mafunzo hayo katika hospitali za Umma walizokuwepo kabla ya kuondolewa.”

Hata hivyo alisema fursa hiyo haitawahusu madaktari wote waliopewa adhabu za kusimamishwa na Baraza la Madaktari, hadi hapo watakapomaliza kutumikia adhabu zao.

Alisema kwa taarifa hiyo madaktari wote waliofutiwa mashtaka na wale waliopewa onyo na onyo kali wanatakiwa kuwasilisha kwa Katibu Mkuu Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii barua kutoka kwa msajili wa Baraza la Madaktari ikithibitisha kurejeshewa usajili  na kuruhusiwa kuendelea na mafunzo kwa vitendo.

Vile vile madaktari waajiriwa(Registrar) wanatakiwa pia kuripoti kwa Katibu Mkuu ili kupewa
barua zao kulingana na Adhabu walizopewa.