Monday, January 21, 2013

MUHULA WA PILI WA RAIS OBAMA WAANZA JANA NCHINI MAREKANI.

Rais Barack Obama aliapishwa rasmi  Jumapili kuongoza Marekani kwa muhula wa pili wa miaka minne. Makamu rais wake Joe Biden pia aliapishwa.

Tukio hilo muhimu litafanywa tena kwenye sherehe za leo Jumatatu ambazo zinategemewa kushuhudiwa na maelfu ya watu katika uwanja mkuu  wa kitaifa hapa jijini Washington DC.

Bwana Obama alikula kiapo saa chache kabla ya saa sita mchana Jumapili akiwa White House katika sherehe zilizochukua  nusu dakika akiwa katika chumba cha  Blu. 

Akiwa na mkewe Michele Obama na binti zake Malia na Sasha na kundi ndogo la waandishi habari, jaji mkuu John Roberts alimwapisha rais Obama kwa muhula wa pili.

Baada ya kula kiapo rais Obama alisalimiana na jaji huyo, na kuwapa  busu mkewe na binti zake, akiwaambia, “nimefanya hivyo”.

Hii ni mara ya saba katika historia ya Marekani kwa rais kula kiapo Jumapili kabla ya sherehe za umma Jumatatu inayofuata. Katiba ya Marekani inasema wazi kuwa muhula wa rais sharti uanze rasmi Januari 20 .

Bw. Obama alitumia Biblia iliyokuwa ya nyanya ya mkewe, LaVaughn Delores Robinson kula kiapo.Katika sherehe za umma baadaye leo Jumatatu nje ya majengo ya bunge, kwa mara nyingine tena atawekelea mikono yake kwenye Biblia iliyotumiwa na rais Abraham Lincoln alipoapishwa mwaka wa 1861. Bwana Obama atatumia Biblia ya pili, iliyomilikiwa na mtetezi wa haki za kiraia Martin Luther King Jr.

Sherehe za leo Jumatatu zitafanyika sambamba na siku kuu ya kitaifa ya Martin Luther King Jr. Mapema Jumapili, rais Obama na familia yake walihudhuria ibada katika kanisa la Metropolitan African Methodist Episcopal Church.

Naye makamu rais Joe Biden  alikula kiapo cha kuhudumu muhula wa pili  katika makao yake rasmi  ya Naval Observatory hapa jijini Washington akitumia Biblia ya familia. 

Aliapishwa na jaji wa mahakama kuu Sonia Sotomayor  na hii ni mara ya kwanza kwa jaji mwenye asili ya kihispania kumwapisha makamu rais wa Marekani.

Rais Obama anaanza muhula wake wa pili huku Wamarekani wakiwa na hisia mchanganyiko kuhusu hali ya kiuchumi, na uwezo wa viongozi wa vyama vyote viwili kuondoa tofauti zao za kisiasa na kutoa kipaumbele katika maswala ya kuongeza ajira na kutatua matatizo ya  kifedha.  Kauli mbiu ya  rais Obama anapoapishwa kwa muhula wa pili ni ; “watu wetu,hali yetu ya baadaye.”

Wiki jana Ikulu ya White House ilitoa video ikiwa na ujumbe wa rais Obama akisema “nchi hii imepitia kipindi kigumu, lakini hatimaye tunaibuka tukiwa na nguvu zaidi“  tunaendelea kuimarisha muungano wetu kuhakikisha kila mtu anapata haki yake endapo atafanya bidii bila kujali anakotokea.”

Wednesday, January 16, 2013

SIMBA KUMSAKA TARAATIIIBU MRIHTI WA OKWI.

Zacharia Hns Pope.
KLABU ya Simba imesema kwamba haitafanya haraka kuziba nafasi ya mshambuliaji wake wa kimataifa wa Uganda, Emannuel Okwi iliyemuuza Etoile du Sahel ya Tunisia jana.
 
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe amesema hapo jana kwamba kwa kuwa wamekwishakamilisha usajili wao wa Ligi ya Mabingwa Afrika na muda wa kusajili unaisha leo, hawatafanya haraka ya kusajili mchezaji mwingine.
 
“Daima sisi huwa tunasajili kwa makini na matunda yake ni kuuza wachezaji kwa bei nzuri, mfano Patrick Ochan, Mganda mwingine tuliyemuuza TP Mazembe (ya DRC), hivyo hatutafanya papara tena katika kusajili, ili tupate mkali kama au zaidi ya Okwi,”alisema Poppe.
 
Kapteni huyo wa zamani wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) alisema kwamba watasubiri kuona kama watafuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ndipo wasajili mchezaji mwingine, vinginevyo itakuwa hadi msimu ujao.
Kkikosi cha simba.
 Simba jana ilimuuza Okwi klabu ya Etoile du Sahel ya Tunisia kwa dau la dola za Kimarekani 300,000, zaidi ya Sh Milioni 450 za Tanzania.
 
Okwi, aliyezaliwa Desemba 25, mwaka 1992 aliisajiliwa Simba akitoea SC Villa ya Uganda mwaka 2010 akiwa kinda wa miaka 17, akisajiliwa kwa dau la dola za Kimarekani 40,000.
 
Baada ya kumaliza mkataba wake wa awali, Desemba mwaka jana aliongeza mkataba wa miaka miwili na Simba SC ambao kabla hajaanza kuutumikia, anahamia Sahel.
                                                                                                                          (CHANZO BIN ZUBEIRY)

SIMBA KILINGENI OMAN KESHO.

Mashabiki wa klabu ya simba ya jijini Dar es slaam.
  MABINGWA wa ligi kuu soka Tanzania Bara Simba Sc, kesho watashuka katika uwanja wa Qaboos Sports Complex nchini Oman kukwaana na timu ya Taifa ya huko iliyoshiriki michuano ya Olimpiki, imefahamika.
 
Simba ipo nchini Oman kwa kambi maalum ya kujiandaa na mzunguko wa pili wa ligi kuu soka Tanzania Bara  na michuano ya kimataifa.
 
Katibu Mkuu wa Simba Evodius Mtawala ameiambia Sports Lady leo kwamba mchezo huo utakuwa ni muhimu kwa timu hiyo kwani kocha atautumia katika harakati zake za kukisuka ipasavyo kikosi chake. 
 
“Kama mnavyojua tangu tumpate kocha mpya (Patrick Liewing) kikosi hajipata kukaa pamoja hivyo huo ndio mwanzo wa kocha kuanza kukiweka sawa kikosi chake,”alisema 
 
Mtawala aliongeza kuwa, kocha Liewing amefurahishwa na wachezaji wote kuwa pamoja kwa sasa ambapo anaamini kambi hiyo itakuwa na mafanikio zaidi. 
 
Mbali na mchezo huo, Simba inatarajiwa kucheza mechi nyingine za kirafiki na timu kama Fanja Fc na timu ya jeshi la huko kabla ya kurejea nchini Januari 23.
Wekundu wa msimbazi, kikosi cha timu ya simba cha jijini Dar es salaam.
 

KUMBUKUMBU YA REGIA MTEMA JIJINI DAR.

Baba mzazi wa aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Regia Mtema, Estaratus Mtemanyenza akitoa shukrani wakati wa kumbukumbu ya kuadhimisha mwaka mmoja tangu kifo cha mbunge huyo, iliyofanyika jijini Dar es Salaam juzi. Kulia ni Naibu Waziri wa Sheria na Katiba, Angella Kairuki.
Katibu wa Kamati ya Maandalizi na Msemaji wa Regia Foundation, Olivia Sanare akizungumza wakati wa maadhimisho ya kumbukumbu ya kifo cha aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Regia Mtema.
Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika (Kulia), akiwa katika hafla ya kumbukumbu ya mwaka mmoja wa kifo cha Regia Mtema.
  ALIYEKUWA Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Regia Mtema, ametimiza mwaka mmoja tangu kufariki kwake, ambapo Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba, alihudhuria maadhimisho hayo na kusema demokrasia ya kweli haigaiwi katika sahani ya dhahabu, bali kwa kuipigania.

Makamba alienda mbali zaidi na kuongeza kuwa, wanaopaswa kupigania haki hiyo ni vijana ambao wanayo nafasi kubwa katika safari ya kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani mwaka 2015.

Makamba alitoa kauli hiyo jana usiku katika hafla ya kumbukumbu ya kuadhimisha mwaka mmoja tangu kifo cha Regia, aliyefariki kwa ajali ya gari Januari 14, mwaka jana - hafla iliyofanyiola katika Hoteli ya Peacock jijini Dar es Salaam.

Akitoa mada iliyohusu vijana na namna anavyomfahamu Regia, Makamba alisema kama vijana watatumika vizuri katika demokrasia, watakuwa chachu ya maendeleo na kwamba ujana peke yake si sifa ya kuwa kiongozi.

Makamba ambaye ni Mbunge wa Bumbuli (CCM), alisema lazima uchaguzi wa mwaka 2015 uamuliwe na vijana kama alivyokuwa na uthubutu wa kufanya mambo makubwa Regia.

Naibu waziri huyo aliwataka vijana kutafakari ni kwa nini walijiandikisha kwa wingi bila ya kwenda kupiga kura katika chaguzi mbili za 2005 na 2010 na kwamba uchaguzi ujao ni lazima wabadilike na kufanya uamuzi mgumu.

Alitoa mfano kwamba, mwaka 2015, watajiandikisha vijana wapya  milioni 5 na kutimiza zaidi ya waliojiandikisha milioni 25, uchaguzi utakuwa umetendewa haki na vijana.

Hata hivyo alisema ili kusukuma gurudumu la maendeleo si lazima vijana wakagombea uongozi katika siasa tu bali hata katika sekta na shughuli zingine.

 “Sikugombea nafasi ya uongozi katika nchi hii kwa sababu ya kutaka ukubwa, bali nilifanya hivyo ili vijana waige kutoka kwangu na kama sasa wengine walivyoiga kwa Regia,” alisema Makamba.
Regia Mtema enzi za uhai wake.
 Akizungumzia alivyomfahamu Regia, Makamba alisema alimfahamu siku chache kabla ya kuanza kwa kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, katika midahalo iliyokuwa ikirushwa na televisheni nchini.

“Nikiwa naangalia mdahalo wabunge waliokwenda kugombea majimboni, nilimwona Zitto, Halima na dada mwingine ambaye sikumfahamu akiwa nao, naye akizungumza namna anavyokwenda jimboni huku akitoa maelezo mazuri,” alisema Makamba

Makamba alisema baadae alifahamiana zaidi kwa kuonana na kushirikiana naye katika mambo mbalimbali bungeni ambapo alikiri Regia alikuwa ni mtu mwenye uwezo na upeo mkubwa wa mambo.
Gari aliyokuwa akiiendesha marehemu Regia Mtema, na kuchukua uhai wake.

BONY YAYI ZIARANI NCHINI KWA SIKU MBILI.

Rais Dkt.Jakaya Mrisho kikwete akimkaribisha mgeni wake Mheshimiwa Dkt.Boni Yayi wakati alipowasili katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Mwalimu julius Nyerere usiku wa leo.
Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika na Rais wa Benin, Mheshimiwa Dkt. Boni Yayi amewasili nchini usiku wa leo, Jumanne, Januari 15, 2013, kwa ziara ya kikazi ya siku mbili nchini Tanzania.

Kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dar es Salaam, Rais Boni Yayi amepokelewa na mwenyeji wake, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete mara ndege yake ilipotua kiasi cha saa tano unusu usiku.


Kesho asubuhi, viongozi hao wawili watafanya mazungumzo rasmi kabla ya Rais Boni Yayi kuondoka nchini kuendelea na ziara yake Barani Afrika.
Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete na mgeni wake Rais Dkt.Boni Yayi wakifurahia jambo katika hoteli ya Kilimanjaro leo usiku.
                                                                                                

MAMA SALMA ASHUSHA PARTY NZITO KWA WAKE WA MABALOZI.

Baadhi ya wake wa Mabalozi wanaowakilisha nchi zaoTnzania wakisubiri kuanza kwa hafla ya kukaribisha mwaka mpya2013 katika viwanja vya Ikulu jjijini Dsm Jan 15,2013 iliyoandaliwa na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete (hayupo pichani).

Mke wa Rais Mama Salma Kikwete (kushoto) akisalimiana na Mdau Fauzia Aboud katika hafla hiyo katika viwanja vya Ikulu jijini Dar e Salaam Jan15,2013.

Mke wa Rais Mama Salma Kikwete(mwenye kilemba)akipongezana na Consulate wa Jamhuri ya Poland Bibi Grazyna Tairo kwenye hafla ya kuwakaribisha wenza wa Mabalozi nchini jan 15,2013 katika viwanja vya Ikulu jijini Dar es Salaam.

Pix no 7-Mke wa Makamu wa Rais Mama Asha Bilal (aliekaa) akisalimiana na Msaidizi Mwandamizi wa Rais masuala ya Diplomasia , Liberata Mulamula walipokutana katika halfa ya kusherehekea mwaka mpya 2013 kwaajili ya wake wa Mabalozi nchini iliyoandaliwa na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete katika viwanja vya Ikulu jijini Dar es Salaam Jan 15,2013,

Mke wa Rais Mama Salma Kikwete (mwenye kilemba) akipongezana na Kiongozi wa wenza wa Mabalozi nchini Celine Khalfan Juma Mpango katika hafla ya kusherehekea na kukaribisha mwaka mpya 2013 katika viwanja vya Ikulu jijini Dar es Salaam Jan 15,2013.

Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akiongea kwenye hafla maalumu ya kuwakaribisha wake wa Balozi nchini kwa mwaka mpya 2013, Hafla hiyo imefanyika katika viwanja vya Ikulu jijini Dar- es Salaam , Jan 15,2013.


ke wa Makamu wa Rais Mama Asha Bilal (kushoto) akibadilishana mawazo na Mke wa Waziri Mkuu Mama Tunu Pinda (kulia) katika hafla maalumu ya mwaka mpya 2013 kwaajili ya wake wa Mabalozi iliyoandaliwa na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete(hayupo pichani) kwenye viwanja vya Ikulu jijini Dar es Salaam Jan,15,2013.

Mke wa Rais Mama Salma Kikwete akisalimiana na Mke wa Rais Mstaafu Mama Sitti Mwinyi(kushoto) katika hafla mwaka mpya2013 ya kuwakaribisha (SPOUSE) wake wa Mabalozi nchini Jan 15,2013 katika viwanja vya Ikulu jijini Dar es Salaam.

Mke wa Rais Mama Salma Kikwete (mwenye kilemba) akibadilishana mawazo na baadhi ya wenza wa Mabalozi wanaowakilisha nchi zao nchini wakati wa sherehe ya hafla ya kuukaribisha miaka 2013 katika viwanja vya Ikulu jijini Dar es Salaam,jan 15,2013.

CHADEMA NDANI YA NJIRO, ARUSHA.

Katibu mkuu wa Chadema Dk Wilbroad Slaa akihutubia maelfu ya wananchi waliojitokeza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Reilway Njoro mjini Moshi .

Mbunge wa jimbo la Arusha mjini Godbless Lema akichangisha fedha kwa ajili ya kufanikisha mikutano ya chama hicho inayoendelea sasa maeneo mbalimbali nchini.

Mbunge wa jimbo la Arumeru Mashariki Joshua Nassari akihutubia maelfu ya wananchi katiika viwanja vya Railway Njoro wakati wa mkutano wa hadhara .

Maelfu ya wananchi waliojitokeza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Reilway Njoro mjini Moshi na kuhutubiwa na viongopzi mbalimbali wa chama cha demokrasia na maendeleoCHADEMA,wakiongozwa na Dk Wilbroad Slaa. .

Vijana wa sarakasi wakionesha umahiri wao mbele ya Dk Slaa wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Railway Njro mjini Moshi.



Moja ya wakazi wa mji wa Moshi ambaye jina lake halikuweza kufahamika mara moja akicheza wakati wa mkutano wa hadhara wa Chadema uliofanyika viwanja vya Railway Njoro mjini Moshi.

Mbunge wa jimbo la Arumeru Mashariki Joshua Nassari akiteta jambo na katibu wa chadema mkoa wa Kilimanjaro Basl Lema ,kulia kwake ni Dk Slaa.

PROFESSOR J AZUSHIWA KIFO.

Mwanamuziki Professor J.
 Kuna habari za uzushi zimesambaa leo kuwa rapper Joseph Haule aka Profesa Jay amefariki dunia ambazo kwa mujibu wake mwenyewe Profesa zimemshtua mama yake kwa kiasi kikubwa.

Taarifa hizo za uzushi zimedai kuwa Profesa Jay alianguka na kuzimia na wengine kudai amefariki.
Kupitia mtandao wa Twitter, Profesa Jay amezikanusha taarifa hizo kwa kuandika, “Jamani eeeh mimi ni mzima wa afya njema hao wanaozusha kuwa nimekufa wataanza wenyewe. Mi niko fresh mpaka natamani kujiteka.”
“Watu hawana kazi za kufanya kila siku kuwaombea wenzao mabaya tu maisha sijui yamewashinda wamekalia uzushi tu. Leo zamu yangu nimepigiwa simu mpaka nimeshangaa kumbe watu wanataka kuhakikisha mzee washindwe na walegee,” aliongeza.
“Imemshtua sana mama yangu maana alinisikia nilipokuwa nikioongea na moja ya simu zilizokuwa zinanipa ripoti hii.”

MKE WA KIGOGO NDANI YA SAKATA LAUCHANGUDOA DAR.

Katika hali isiyokuwa ya kawaida,mke wa kigogo mmoja ambae anacheo kikubwa hivi karibuni alibambwa kwenye danguro moja lilipo maeneo ya Sinza jijini Dar akijiuza.
Habari zaidi toka kwa watu wa karibu wanaomjua mwanamke huyo maarufu kwa jina la Mama Amina zinadai kuwa yeye ni mke wa pili wa kigogo mmoja anaefanya kazi kwenye Wizara moja nyeti ya Serikali ya Jamhuri ya Tanzania.

Aidha watu hao waliiambia xdjayz  Jijini Dar kuwa mwanamke huyo alifikwa na balaa hilo katika msako mkali unaoendelea wa Polisi Kanda ya Kinondoni wa kuwakamata machangudoa wote wanaojiuza.


Habari zaidi ziliendelea kusema kuwa kigogo huyo ana familia nyingine ambayo inaishi maeneo ya Mbezi Beach .
Huyu  Mama Amina amempangishia nyumba maeneo ya Sinza Mori na amekuwa akimpa huduma zote muhimu...
Cha  kushangaza ni kwamba  kila mumewe akiondoka nyuma huenda kujiuza.

Mwandishi wetu jana alifika kituo cha Polisi Oysterbay na kushuhudia kundi la machangudoa hao wakipelekwa Mahakamani kwa gari ya Manispaa pamoja na gari ya polisi akiwemo mwanamke huyo wa kigogo.
Machangudoa wakiwa wameziba nyuso zao zilisipigwe picha na mwandishi wetu.
Mke wa mtu akiwa ameziba uso wake kwa mikono ili kukwepa kamara
Mke wa mtu aliyesuka akiinamisha kichwa chini kukwepa kupigwa picha na kamera 
Mke wa mtu akiwa amejifunika uso kwa Khanga ili asipigwe picha.

Tuesday, January 15, 2013

DR.SHEIN ATEUA MWENYEKITI WA BODI.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Ali Mohamed Shein amemteuwa Mussa Msheba Suleiman kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Usafiri wa Barabarani katika Wizara ya Miundo Mbinu na Mawasiliano,Zanzibar.
 
Kwa mujibu wa Taarifa iliotolewa na Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi ,Dkt Abdulhamid Yahya Mzee imeeleza kuwa Rais amefanya uteuzi huo kwa mujibu ya uwezo aliopewa chini ya kifungu Namba 14((2)(a) cha sheria ya Usafiri wa Barabarani(THE ROAD TRANSPORT ACT)Namba 7ya mwaka 2003.
 
Uteuzi huo umeanza tarehe 06Januarri,2013.
 
IMETOLEWA NA IDARA YA HABARI MAELEZO ZANZIOBAR.
13/1/2013.
                                                                          

KAGASHEKI USO KWA USO NA WACHEZAJI WA SEATTLE SOUNDERS.

Waziri Balozi Kagasheki.
 Waziri wa Maliasili na Utalii Balozi Khamis Kagasheki akizungumza na ujumbe wa wachezaji na waandishi wa habari (PICHA CHINI),kutoka timu ya seattle Sounders ya Canada wakati wa chakula cha jioni kilichoandaliwa na Bodi ya Utalii ya Tanzania TTB kwenye hoteli ya serena jijini Dar es salaam hapo jana. 

Kwa ajili ya ugeni huo, Bodi ya Utalii ilisaini mkataba wa kutangaza utalii wa Tanzania katika kiwanja cha timu hiyo katika ziara iliyofanywa na Waziri wa Maliasili Balozi Khamis Kagasheki nchini humo.

Katika msafara huo unaoongozwa na mchezaji wa mpira wa American Football Kevin Griffin ambaye pia ni Fan Development Marketing wa Sunders FC, wachezaji hao walitembelea mbuga za Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro na Mbuga ya Tarangire ambapo walipata muda wa kujionea vivutio vilivyomo katika hifadhi hizo na kupiga picha.
Waziri wa maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, uso kwa uso na timu ya SEATTLE SOUNDERS na waandishi wa habari.
                                                                      

WAWILI WAZIKWA HAI MBEYA.

WAKAZI wawili wa Kijiji cha Karungu, Kata ya Ivuna, Wilaya ya Momba, mkoani Mbeya wamefariki dunia baada ya kufukiwa wakiwa hai katika kaburi moja na marehemu wanaodaiwa kumuua, tukio linalohusishwa na imani za kishirikina.

Watu hao, Ernest Molela anayekadiriwa kuwa na umri zaidi ya miaka 60 na Bibi Mizinala Nachela ambaye umri wake unakadiriwa kuwa zaidi ya miaka 50, walizikwa wakiwa hai pamoja na aliyekuwa mkazi wa kijiji hicho, marehemu Nongwa Hussein.

Kaimu Ofisa Mtendaji wa Kata ya Ivuna, Joseph Silwimba aliwaambia  wanahabari jana kuwa, tukio hilo lilitokea juzi kati ya saa tano na sita mchana, muda mfupi kabla ya maziko ya Hussein.

Kabla ya kufukiwa katika kaburi moja na marehemu, Molela na Nachela kwa nyakati tofauti walipigwa hadi kuzirai na watu wanaodaiwa kushiriki kuchimba kaburi kwa ajili ya kumzika marehemu Hussein.

Silwimba alisema Hussein alifariki dunia Jumamosi saa 10 jioni baada ya kuugua kwa muda mrefu, lakini inaonekana kuwa baadhi ya wakazi wa kijiji hicho walihusisha ugonjwa huo ambao ulisababisha kifo chake na ushirikina.

Jana mchana, Mkuu wa Polisi wa Wilaya (OCD), Momba aliyefahamika kwa jina la Wendo aliongoza operesheni ya kufukua kaburi walimozikwa watu hao, ambao walikutwa wakiwa wameshafariki dunia.

Silwimba alisema miili ya Molela na Nachela ilifanyiwa uchunguzi, kisha kukabidhiwa kwa ndugu na jamaa zao ambao waliifanyia mazishi jana mchana.

Mkasa wenyewe
Kundi la vijana tisa ambao wanadaiwa kuwa ndiyo waliokuwa wakichimba kaburi la marehemu Hussein walianza msako katika Kijiji cha Karungu wakiwatafuta wale waliowatuhumu kwamba ni wachawi na kwamba walihusika na kifo chake.

Silwimba alisema katika harakati zao, walikwenda nyumbani kwa George Hussein ambaye ni kaka wa marehemu lakini hawakumkuta, hivyo kuamua kuchoma moto nyumba yake kwa kuwa walikuwa wakimtuhumu kuhusika na kifo hicho.

“Baada ya kufanya uharibifu huo, walikwenda hadi nyumbani kwa Mzee Molela kisha wakamkamata na kumpiga sana hadi hali yake ikawa mbaya kisha wakambeba hadi eneo la maziko,” alisema na kuongeza:

“Waliporejea kwenye msiba walimkuta Mama Nachela naye wakamkamata na kuanza kumpiga hadi akazimia na yeye pamoja na Molela waliwavuta hadi kwenye kaburi ambako mazishi ya Nongwa (Hussein) yalifanyika.”

Alisema baada ya jeneza kushushwa kaburini, vijana hao wanaodaiwa kwamba walikuwa na hasira walimvuta Molela na kumwamuru kuweka udongo kaburini, lakini alishindwa kufanya hivyo kutokana na hali yake kuwa mbaya.

“Baada ya kushindwa walimsukumiza kaburini na baadaye walimvuta yule mama (Nachela) ambaye naye alikuwa hajitambui na kumtupa ndani ya kaburi halafu wakawafukia wote, kisha wakaondoka,” alisema Kaimu Ofisa Mtendaji huyo.
Kamanda wa polisi mkoani Mbeya Diwani Athuman.
                                                                            

Monday, January 14, 2013

MAKAMU WA RAIS DKT. BILAL AENDESHA KIKAO CHA MUUNGANO MJINI ZANZIBAR LEO.

Makamu wa rais Dk.Mohammed Gharib Bila.
WAKATI mjadala juu ya Muungano kati ya Zanzibar na Tanganyika ukishika kasi na kuzusha mtazamo tofauti Kamati ya Pamoja ya kutatua kero za Muungano imefanya kikao chake Zanzibar kujadili mambo kadhaa yanayoleta mgongano katika Muungano huo.

Mkutano huo uliofanyika Hoteli ya Zanzibar Beach Resort uliongozwa na Makamo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Mohammed Gharib Bilal, Waziri Mkuu Mizengo Pinda na Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ni mfululizo wa mikutano kama hiyo ambayo imewahi kufanyika mara ya mwisho Januari mwaka jana.

Baadhi ya Mawaziri kutoka Tanzania Bara na wa Zanzibar pamoja an wakurugenzi wa idara ambazo zinasimamia masuala yanayolalamikiwa ndani ya Muungano pia wameshiriki na kutoa maelezo yao kuhusiana na namna ya kuondosha kero zilizokuwepo ndani ya Muungano huo.

Kwa kuwa waandishi wa habari hawakuruhusiwa kuingia ndani ya vikao hivyo ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar imetoa taarifa ikielezea kuwa mkutano huo umepiga hatua katika kutatua kero za Muungano lugha ambayo imekuwa ikisikika kila baada ya mikutano kama hiyo.

Waziri wa Nchi Ofisi wa Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mohammed Aboud Mohammed ambaye ndio mwenye dhamana ya masuala ya Muungano kwa Zanzibar alisema miongoni mwa mambo amabyo yamepata ufumbuzi ni kuhusiana na suala la mgawanyo wa misaada kutoka nje pamoja na ajira kwa wazanzibari ndani ya taasisi za Muungano.

Alisema licha ya kuwepo na kasoro bado Muungano ni muhimu kuwepo kutokana na faida kuwa nyingi kwa pande zote mbili na kuahidi serikali zote mbili kuendelea kuwaelimisha wananchi juu ya faida ya kuendelea kwa Muungano huo wa Tanganyika na Zanzibar ambao umeshafikia miaka 49 tokea kuasisiwa kwake.

Hata hivyo kauli ya Mohammed Aboud haijaelezea kwa undani masuala ya uhusiano wa Zanzibar na nchi za nje pamoja na suala la mafuta na gesi asilia ambalo limechukua nafasi kubwa kujadiliwa hivi karibuni.

Kuhusu mafuta na gesi asilia Aboud amesema serikali zote mbili zimefikia hatua nzuri ya kuelekea kuondoa rasilimali hiyo katika orodha ya mambo ya Muungano ili Zanzibar kunufaika kiuchumi na rasilimali hiyo bila ya kuingiliwa na Tanzania Bara.

Wachunguzi wa kisiasa wanaeleza kwamba huu ni wakati mgumu kwa serikali ya Tanzania inapoelekea kuandika katiba mpya ambapo suala la Muungano limeibuka huku baadhi ya wananchi wakitaka uhuru zaidi kwa Zanzibar huku wengine wakipinga hilo.

Baadhi ya wazanzibari wakiongozwa na Maalim Seif Sharif Hamad wanashikilia msimamo wa kutaka mfumo mpya wa Muungano wa Mkataba kutokana na Muungano uliopo kuwa na kasoro nyingi ambazo zinainyima fursa Zanzibar kuendelea kiuchumi na kijamii.

Wajumbe wa Kamati ya pamoja kati Serikali ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wamekutana katika utaratibu wao wa kawaida wa kujadili masuala yanayohusu Muungano ambapo walipitia na kuridhia kumbukumbu za Kikao cha Kamati hiyo kilichofanyika Tarehe 28 Januari mwaka 2012 Mjini Dar es salaam pamoja na kupokea Taarifa ya utekelezaji wa masuala ya Muungano.
 

Aidha wajumbe hao walipitia na kuridhia mapendekezo kuhusu utaratibu wa muda wa mgao wa ajira kwa Taasisi za Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na kupitia makubaliano ya hoja zilizopatiwa ufumbuzi.

Wakichangia Hoja mbali mbali zilizowasilishwa kwenye Mkutano huo baadhi ya Wajumbe wa Kikao hicho wameelezea kuridhika kwao na hatua zinazochukuliwa na Ofisi ya Waziri Mkuu na ile ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar chini ya usimamizi wa Wanasheria Wakuu wa Pande zote mbili katika kulishughulikia suala la mafuta na gesi kuondolewa katika mambo ya Muungano.

Walisema hatua ya kuridhiwa na kukubaliwa na Maraisi wa Serikali zote mbili Nchini limewawezesha na kuwapa nguvu wataalamu wa sheria wa pande zote mbili kuangalia namna ya kuandaa utaratibu utakachokidhi mahitaji ya kisheria ya kila upande kuhusu suala hilo.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan alisema mwenendo mzima wa utekelezaji wa masuala yanayoleta kero ndani ya Muungano unakwenda vyema kufuatia mfumo wa vikao vinavyohusisha watendaji wa pande zote mbili.

Waziri Samia alisema hata hivyo yapo baadhi ya masuala ambayo huchukuwa muda mrefu kuyapatia ufumbuzi kutokana na mfumo wa sheria unaohitaji mabadiliko ili kwenda sambamba na makubaliano yaliyoridhiwa.
Waziri mkuu Mhe.Mizengo Kayanza Peter Pinda.
Waziri Mkuu wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Mizengo Pinda akitoa shukrani zake aliipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa maadhimisho mazuri ya sherehe za Mapinduzi ya Zanzibar za Mwaka huu zilizokuwa za mfano wa aina yake.

Pinda alisema jamii ingependa kuona sherehe za Mapinduzi za Mwakani kutimia nusu karne zikawa za mafanikio makubwa zaidi na Serikali ya Muungano wa Tanzania inaandaa fikra ya namna ya kuongeza nguvu za ushiriki na mchango wake katika kufanikisha sherehe hizo.

Kwa upande wake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema umahiri wa Mawaziri wa Pande zote mbili katika kikao chao cha sekreterieti umewezesha kamati ya pamoja ya SMT na SMZ kufanikiwa kwa hali ya juu.

Balozi Seif alifahamisha kwamba wajumbe wa kikao hicho wameweza kupokea na kuridhia masuala mbali mbali waliyoyaagiza katika kikao cha mwaka jana ambayo yalikuwa yakileta kero katika masuala ya Muungano.

Akikifunga kIkao Hicho Mwenyekiti wa Kamati ya pamoja na Serikali ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Dr. Mohd Gharib Bilal alishauri Viongozi wa Wizara za Serikali zote mbili kuendelea kushirikiana ili kuleta ufanisi zaidi.

Dr. Bilal alisema ushirikiano huo utakaoshirikisha pia watendaji na wataalamu wa sekta husika ndani ya taasisi zao utasaidia kupunguza na hatimae kuondosha kabisa kero zinazosababisha hitilafu ndani ya mfumo wa Muungano.

Masuala yaliyowasilisha katika kikao hicho cha Kamati ya pamoja ya SMT na SMZ na kupokewa na kuridhiwa na wajumbe hao ni pamoja na uwezo wa SMZ kukopa nje ya Nchi, malalamiko ya wafanyabiashara wa Zanzibar kutozwa kodi mara mbili, kodi ya mapato-pay as you earn { PAYE} pamoja na suala la Mafuta la kutaka kutolewa katika mambo ya Muungano.

Kikao kijacho cha Kamati ya Pamoja ya Serikali ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kinatarajiwa kufanyika mara baada ya Sherehe za mwaka huu za Muungano wa Tanganyika na Zanzibar na kufanyika pahali zitakapofanyika Sherehe hizo.
Makamu wa rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, dk.Mohammed Gharib Bilal, akiteta jambo na makamu wa pili wa rais wa Zanzibar Mhe.Seif Ali Idd.
                                                                           

UFAFANUZI WA MAONI BINAFSI YA MAALIM SEIF KWA TUME YA MABADILIKO YA KATIBA.

HOTUBA YA MAKAMU WA KWANZA WA RAIS WA ZANZIBAR, MHESHIMIWA MAALIM SEIF SHARIF HAMAD KWA WAANDISHI WA HABARI HUKO HOTELI YA BWAWANI TAREHE 14 JANUARI 2013, KUHUSU MAONI YAKE BINAFSI ALIYOYATOA MBELE YA WAJUMBE WA TUME YA MABADILIKO YA KATIBA ILIYOFIKA NYUMBANI KWAKE MBWENI ZANZIBAR, SIKU YA TAREHE 13 JANUARI, 2013.
Makamu wa kwanza wa rais wa serikali ya mapinduzi ya zanzibar, Maalim Seif Sharrif Hamad.
Waheshimiwa Waandishi wa Habari
Kwanza kabisa hatuna budi kumshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa kutujaalia uhai na uzima na kutuwezesha kukutana tena leo hapa hoteli ya Bwawani, ikiwa ni mara ya kwanza kwangu kufanya mkutano kama huu kwa waandishi wa habari tokea kuanza kwa mwaka huu mpya wa 2013. Naomba nichukue nafasi hii kukutakieni kheri na Baraka tele katika mwaka huu wa 2013. Aidha, sina budi kutoa shukurani zangu nyingi na za dhati kabisa kwenu nyote waandishi mlioweza kuhudhuria hapa kwa wingi, licha ya kupewa taarifa kwa muda mfupi, juu ya kuwepo kwa mkutano huu, lakini mkaukubali na mkasema muje kusikiliza wito wetu.
Waheshimiwa waandishi wa habari
Kama ambavyo mnaelewa hivi sasa nchi yetu imo katika mchakato muhimu wa mabadiliko ya katiba. Mchakato huo ni jambo muhimu sana kwa sababu hii ni mara ya kwanza kabisa wananchi wa Tanzania wanashirikishwa kikamilifu katika kuamua aina ya katiba wanayoitaka, tokea katiba hiyo ilipotungwa mwaka 1977.
Tume ya mabadiliko ya Katiba katika kufanikisha kazi yake tayari imemaliza kazi ya kukusanya maoni ya wananchi, katika maeneo mbali mbali hapa Zanzibar na Tanzania Bara, na baada ya kumaliza hatua hiyo ya kukusanya maoni ya wananchi, tume hiyo ilianza kazi ya kukutana na makundi maalum, kwa ajili ya kuyasikiliza na kuchukua maoni ya makundi hayo, ambapo vyama tafauti vya siasa makundi mengine muhimu ya kijamii, zikiwemo taasisi za kidini yaliweza kupata fursa kama hiyo.

Waheshimiwa Waandishi wa Habari
Baada ya tume hiyo ya mabadiliko ya Katiba kumaliza kuchukua maoni ya makundi maalum, jana tarehe 13 Januari, 2013 ilianza kukutana na viongozi mashuhuri kwa ajili ya kupata maoni.
Waheshimiwa waandishi wa habari na furaha kukujuilisheni kuwa kwa mujubu wa Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Mstaafu Joseph Sinde Warioba, mimi ndiye niliyepata bahati ya kuwa wa kwanza katika kundi la viongozi mashuhuri kupewa nafasi ya kutoa maoni yangu mbele ya Tume hiyo.
Baadhi ya wajumbe wa Tume hiyo wakiongozwa na Mwenyekiti wake, Jaji Warioba na Makamu wake, Jaji Augostino Ramadhan jana asubuhi walifika nyumbani kwangu Mbweni, kwa ajili ya kuja kunisikiliza kuchukua maoni yangu kuhusu katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hivyo nimeona ni jambo la busara wananchi nao wafahamu japo kwa uchache ni kitu gani nilichokizungumza katika maoni yangu binafsi, kama Seif Sharif Hamad.
Waheshimiwa Waandishi wa Habari
Kama ilivyojitokeza kwa Wazanzibari walio wengi, nami nimeona ni jambo la busara kabisa katika maoni yangu nizungumzie moja kwa moja suala la Muungano wa Tanzania, kwa vile nikiwa kama Mzanzibari niliwaeleza wajumbe wa Tume hiyo kuwa, hilo ndilo jambo linalonigusa zaidi katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano.
Nukta muhimu nilizozizungumzia katika maoni yangu ni kama ifuatavyo:
1. Asili na Sababu za Muungano
2. Misukosuko katika Muungano
3. Kiini cha matatizo katika Muungano
4. Uvunjwaji wa mkataba wa Muungano
5. Matatizo yatokanayo na kiini cha tatizo
6. Nafasi ya Zanzibar katika Muungano
7. Vipi tutoke hapa tulipo
8. Mfumo mpya wa Muungano wa Mkataba
ASILI NA SABABU ZA MUUNGANO
Waheshimiwa Waandishi wa Habari
Maoni yanayotolewa kuhusu asili na sababu za Muungano yamekuwa yakitofautiana mno. Wapo wanaouleza Muungano huu kuwa ni wa pekee katika bara la Afrika, kwani ndiyo pekee ulioweza kudumu katika kutimiza azma na malengo ya kuleta umoja wa Afrika (Pan-Africanism), na pia wapo wanauona kuwa ni “jaribio la kusisimua la ukoloni mdogo wa nchi moja ya Kiafrika kuiteka na kuitawala nchi nyengine ya Kiafrika”.
Hivyo basi, si rahisi kusema moja kwa moja kuwa maelezo yepi au hoja ipi ni sahihi. Utangulizi (Preamble) wa Mkataba wa Muungano wa 1964 wenyewe unataja sababu kuu ya kuunganisha nchi za Zanzibar na Tanganyika kuwa ni “maingiliano ya muda mrefu ya watu wa nchi mbili hizi na mahusiano yao ya kidugu na kirafiki na kuendeleza umoja wa watu wa Afrika. Lakini miaka 49 sasa baada ya uzoefu wa Muungano huu, Wazanzibari wanajiuliza kweli haya yalikuwa ndiyo madhumuni ya Muungano huu?
Tukiangalia kwa undani tutaona kuwa wakati ule wa miaka ya 1950 na 1960 waasisi na wakuu wa harakati za kupigania Uhuru waliiona mipaka ya nchi zao iliyowekwa na wakoloni kuwa ni ‘mbinu za kibeberu’zilizotekelezwa kwa ajili ya manufaa na maslahi yao. Kutokana na hisia hizo, mazungumzo ya kuanzisha aina fulani ya umoja miongoni mwa nchi huru za Afrika yalitawala duru za siasa.
Nadharia mbili zilijichomoza. Ya kwanza, ikishadidiwa na Kwame Nkrumah wa Ghana, ilikuwa ikitaka kuasisiwa kwa nchi moja tu ya Afrika nzima iliyoungana ikiwa na Serikali moja kwa bara zima. Nadharia hii ilipingwa na baadhi ya viongozi, wakiongozwa na Mwalimu Julius Nyerere wa Tanganyika, ambao walisisitiza haja ya kuanza na miungano ya maeneo (regional unions) chini ya mfumo wa Shirikisho badala ya kuwa na mpango wa Serikali moja.[1]
Katika kulifikia lengo hilo, viongozi wa kisiasa wa nchi tatu za Afrika Mashariki – Kenya, Uganda na Tanganyika – walikuwa wakifanya mikutano ya mara kwa mara kipindi chote cha kati ya mwaka 1961 na 1963 kuona jinsi gani wanaweza kutimiza ndoto hiyo. Mfumo wa Muungano uliokuwa ukiandaliwa ulikuwa ni ule wa Shirikisho.
Ijapokuwa Zanzibar haikuwakilishwa katika mkutano wa kuanzishwa umoja wa Afrika Mashariki, viongozi wan chi tatu hizo walisema kuwa“tunapaaswa kuweka bayana kwamba nchi hiyo inakaribishwa kushiriki kikamilifu katika mikutano yetu kwa ajili ya uundwaji wa Shirikisho.
Wakati juhudi za kuanzisha Shirikisho la Afrika Mashariki zikiwa zinafifia, Mwalimu Nyerere aliona Zanzibar kama fursa ambayo hakutaka kuipoteza. Katika mazungumzo ya siri kati yake na Rais Abeid Amani Karume wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, wakakubaliana kuziunganisha nchi mbili hizi. Hakukuwa na ushirikishwaji wa aina yoyote ule wa wananchi wa nchi hizi mbili katika maamuzi haya makubwa. Usiri uliogubika hatua hii kubwa unafichuliwa na Mwalimu Nyerere mwenyewe pale aliposema:
“Tanganyika tulipeleka Polisi wetu Zanzibar. Baada ya kuyashinda matatizo kadhaa tukaungana. Sisi wenyewe kwa khiyari zetu tulikubaliana kuungana. Karume na mimi tulikutana. Peke yetu wawili tu tulikutana. Nilipomtajia wazo la Muungano, Karume hakufikiri hata mara mbili. Pale pale alinitaka kuita mkutano wa waandishi wa habari kutangaza azma yetu. Nilimshauri asubiri kidogo kwani ilikuwa bado ni mapema mno kuweza kuviarifu vyombo vya habari.
Taarifa hizi ziliendelea kubaki kuwa siri hadi tarehe 26 Aprili, 1964 pale Redio ya Tanganyika ilipotangaza kwamba siku hiyo Marais wawili hao watakutana katika Bunge la Tanganyika kubadilishana Hati za Muungano ambazo zimeunganisha Zanzibar na Tanganyika kuwa Jamhuri moja.
MISUKOSUKO KATIKA MUUNGANO
Waheshimiwa Waandishi wa Habari
Muungano wa Zanzibar na Tanganyika umepita katika masaiba kadhaa tokea kuasisiwa kwake takriban miaka 49 iliyopita lakini mtikisiko ulioukumba katika siku za karibuni ni mkubwa sana. Ni mkubwa kwa sababu umegusa kiini cha Muungano huu ambapo suala linaloulizwa ni iwapo kwa kule kukubali kushirikiana katika baadhi ya mambo, je, Zanzibar na Tanganyika zimejifuta na hivyo kupoteza hadhi zake kama nchi? Hilo limekuwa ndiyo suala kubwa linaloulizwa na Wazanzibari hasa baada ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda kutamka Bungeni kwamba Zanzibar si nchi.
Muungano huu umekuwa gumzo kuu katika takriban kila mjadala wa katiba na siasa katika nchi yetu. Umejitokeza na kujionyesha hivyo katika mwaka wa mwanzo wa Muungano kuhusiana na sakata la kuwa na Ubalozi wa iliyokuwa Ujerumani Magharibi kwa upande wa Tanganyika na Ubalozi wa iliyokuwa Ujerumani Mashariki kwa upande wa Zanzibar, kuhusiana na uwakilishi wa Zanzibar katika Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki na uanzishwaji wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT) mwaka 1964 – 1966.
Mengine ni wakati wa kuunganisha vyama vya ASP na TANU kuunda Chama Cha Mapinduzi (CCM) mwaka 1977, katika mjadala wa marekebisho ya Katiba wa 1983/84 na hatimaye kujiuzulu kwa Rais wa pili wa Zanzibar Sheikh Aboud Jumbe, wakati wa kuondolewa katika Uwaziri Kiongozi kwa mwandishi wa maoni haya na hatimaye kufukuzwa katika CCM na wenzake 6 mwaka 1988, katika harakati za madai ya kutaka kura ya maoni kuhusiana na Muungano huo mwaka 1989/90, wakati wa mjadala wa kuanzishwa vyama vingi mwaka 1991.
Kama hayo hayatoshi misuko suko mingine mikubwa ilijitokeza katika sakata la Zanzibar kujiunga na Umoja wa Nchi za Kiislamu (OIC) mwaka 1993, wakati wa mjadala wa G-55 kudai kuanzishwa kwa Serikali ya Tanganyika ndani ya Muungano mwaka 1994, katika mjadala wa marekebisho ya 11 na 14 ya Katiba ya Muungano mwaka 1994/95, wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa 1995 na ule wa 2000 na karibuni kabisa kuhusiana na suala la matarajio ya ugunduzi wa mafuta visiwani Zanzibar, harakati za kuanzisha Shirikisho la Afrika Mashariki na pia baada ya kupitishwa kwa Marekebisho ya Kumi ya Katiba ya Zanzibar ya 1984 yaliyofanywa mwaka 2010.
Tume na Kamati kadhaa zimeundwa kuainisha matatizo ya Muungano na kupendekeza njia za kuyatatua. Serikali ya Jamhuri ya Muungano imeunda Tume na Kamati zifuatazo, miongoni mwa nyingi, kuhusiana na masuala haya:
1. Kamati ya Mtei
2. Tume ya Jaji Francis Nyalali (1991)
3. Kamati ya Shellukindo (1994)
4. Kamati ya Shellukindo 2 ya kuandaa Muafaka juu ya Mambo ya Muungano baina ya SMZ na SMT.
5. Kamati ya Jaji Mark Bomani (1995)
6. Kamati ya Jaji Robert Kisanga (1998)
7. Kamati ya ‘Harmonization’
8. Kamati ya Masuala ya Simu (Kamati ya Kusila)
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) nayo kwa upande wake iliunda Kamati zifuatazo kwa madhumuni hayo hayo:
1. Kamati ya Baraza la Mapinduzi (Kamati ya Amina) ya 1992
2. Kamati ya Rais ya Kupambana na Kasoro za Muungano (Kamati ya Shamuhuna) ya 1997
3. Kamati ya Rais Kuchambua Ripoti ya Jaji Kisanga (Kamati ya Salim Juma Othman)
4. Kamati ya Kuandaa Mapendekezo ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar juu ya Kero za Muungano (Kamati ya Ramia) ya 2000
5. Kamati ya Baraza la Mapinduzi juu ya Sera ya Mambo ya Nje
6. Kamati ya Rais ya Wataalamu juu ya Kero za Muungano ya 2001
7. Kamati ya Baraza la Mapinduzi ya Jumuiya ya Afrika Mashariki
8. Kamati ya Mafuta
9. Kamati ya Madeni baina ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Muungano wa Tanzania
10. Kamati ya Suala la Exclusive Economic Zone (EEZ)
11. Kamati ya Masuala ya Fedha na Benki Kuu
12. Kamati ya Rais ya Masuala ya Simu (1996 –1999)
13. Kamati ya Baraza la Mapinduzi juu ya matatizo na kero za Muungano na taratibu za kuyaondoa (2004)
Ukiacha Tume, Kamati na Ripoti hizo, kuanzia mwaka 1985 kulianzishwa utaratibu wa Kamati ya Pamoja ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano na Waziri Kiongozi wa Zanzibar pamoja na Mawaziri wa Serikali zetu mbili ambao ulitarajiwa uwe ndiyo jukwaa la kuzungumzia matatizo kutoka kwa washiriki wakuu wa Muungano huu na kuyapatia ufumbuzi unaofaa.
Utaratibu huu uliachwa kwa muda mrefu lakini sasa umerejeshwa upya kufuatia agizo la Rais Jakaya Kikwete alilolitoa katika mkutano na mawaziri na watendaji wakuu wa Serikali yake huko Ngurdoto, Arusha mwezi Februari, 2006. Mikutano hiyo sasa imebadilishwa utaratibu wake na inaongozwa na kusimamiwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano na timu za pande mbili zikiongozwa na Waziri Mkuu kwa upande wa Serikali ya Muungano na Makamu wa Pili wa Rais kwa upande wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
                                                                     
KIINI CHA MATATIZO YA MUUNGANO
Waheshimiwa Waandishi wa Habari
Kama tulivyokwisha kuona kwamba Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uliundwa kupitia Mkataba wa Muungano wa 1964 (Articles of Union). Mkataba huu, kwa kutumia ushahidi wa picha, ulitiwa saini na Rais wa Jamhuri ya Tanganyika, Mwalimu Julius Nyerere, na Rais wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, Sheikh Abeid Amani Karume, kwa niaba ya nchi zao mbili katika Ikulu ya Zanzibar, tarehe 22 Aprili, 1964.
Mkataba wa Muungano wa 1964 ni Mkataba wa Kimataifa na ndiyo maana kwa kuzingatia matakwa ya sheria za kiingereza zilizokuwa zikifuatwa na Zanzibar na Tanganyika wakati huo na hadi leo uliweka sharti katika kifungu cha (viii) kwamba unapaswa kuthibitishwa na Bunge la Tanganyika na Baraza la Mapinduzi la Jamhuri ya Watu wa Zanzibar likishirikiana na Baraza lake la Mawaziri ili kuupa nguvu za kisheria ndani ya nchi mbili hizo.
Hoja ya kwanza inayojitokeza hapa na ambayo imeshindwa kupatiwa majibu hadi leo ni kushindwa kupatikana kwa nakala halisi ya Mkataba huo ikiwa na saini za Rais Nyerere wa Jamhuri ya Tanganyika na Rais Karume wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar.
Hoja hii imeibuliwa ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano na pia katika Mahkama Kuu ya Zanzibar ambako Serikali zote mbili, Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, zimeshindwa kutoa nakala hiyo licha ya kuahidi kufanya hivyo.
Nusura pekee iliyobaki ni kutegemea nakala halisi (iwapo ipo) inayoelezwa kwamba ilikabidhiwa kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kumbukumbu za Umoja huo kujiridhisha kwamba nchi mbili hizi zimeungana. Kuonekanwa kwa nakala halisi ya Mkataba huo ni muhimu sana katika kujiridhisha uhalisia wa kile kilichokubaliwa baina ya nchi zetu mbili.
Hoja ya pili ni ile inayohusu utekelezwaji wa matakwa ya uthibitishaji (the want of ratification) wa Mkataba huo kwa upande wa Zanzibar. Upo ushahidi wa kutosha kwamba Bunge la Tanganyika lilikutana na kuuridhia Mkataba huo tarehe 25 Aprili, 1964. Kwa upande mwengine, hakuna ushahidi wowote kwamba Baraza la Mapinduzi likishirikiana na Baraza la Mawaziri la Zanzibar lilikaa kuuridhia Mkataba huo kwa kupitisha Sheria ya Kuthibitisha (Ratification Decree) kama ilivyotakiwa na Mkataba wenyewe. Kwa hakika ushahidi ulioibuliwa na Prof. Issa Shivji katika kitabu chake cha karibuni kabisa, Pan-Africanism or Pragmatism? Lesssons of Tanganyika-Zanzibar Union umeweka wazi pasina chembe ya wasiwasi kwamba Mkataba huo haujaridhiwa na upande wa Zanzibar hadi hii leo.
Ukiachilia mbali hoja hizo, na kwa msingi wa hoja tukichukulia kwamba Mkataba huo ni halali, bado ukitazama kwa jicho la sheria, utaona kiini cha matatizo ya Muungano kinatokana na tafsiri ya Mkataba wa Muungano (Articles of Union) wa 1964.
Mfumo uliopo sasa ambao ulianza kutekelezwa 1964 ni ule wa serikali mbili – ile ya Jamhuri ya Muungano na ile ya Zanzibar. Tanganyika haikuwekewa serikali yake tofauti; madaraka yake kwa yale mambo yasiyo ya Muungano yalielezwa kwamba yatasimamiwa na kuendeshwa na Serikali hiyo hiyo ya Jamhuri ya Muungano. Hata hivyo, uhalali wa kisheria wa muundo huu umeendelea kuhojiwa na hata kupingwa kwamba hauwakilishi ipasavyo makusudio yaliyomo katika Mkataba ulioanzisha Muungano wenyewe.
UVUNJWAJI WA MKATABA WA MUUNGANO
Waheshimiwa Waandishi wa Habari
Mbali na suala la muundo wa Muungano, maeneo mengine mengi yanayogusa msingi wa Mkataba wa Muungano yaliendelea kuvunjwa na Tanganyika ikivaa joho la Serikali ya Muungano.
Kifungu cha (iv) cha Mkataba wa Muungano kiliorodhesha mambo 11 tu ambayo ndiyo yaliyokubaliwa na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na Jamhuri ya Tanganyika kuwa mambo ya Muungano. Hata hivyo, kipindi cha miaka 49 ya Muungano kimeshuhudia mambo hayo yakiongezwa isivyo halali kwa kutumia chombo kisicho na mamlaka ya kufanya hivyo yaani Bunge la Muungano na sasa kufikia 22 lakini ukiyanyumbua yanafikia 37.
Mfano unakuta kifungu kimoja cha 11 kinayaweka pamoja mambo manne ambayo ni Bandari, Usafiri wa Anga, Posta na Simu. Kwa lugha ya Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Mhe. Othman Masoud Othman, anasema ni makontena 22 yenye mambo 37 ya Muungano. Ikumbukwe kwamba kila hatua ya kuongeza mambo ya Muungano maana yake ni kuchukua mamlaka ya Zanzibar na kuyahaulisha kwa Serikali ya Muungano ambayo kama tulivyokwisha onyesha kwa hakika hasa ni Serikali ya Tanganyika iliyojivika joho la Muungano.
Mambo hayo yaliyoongezwa juu ya Makubaliano ya Muungano ya asili, yaani, yale kumi na moja (11) ni haya, kama yanavyoelezwa katika Nyongeza ya Kwanza ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano:-
1.Mambo yote yanayohusika na Sarafu na Fedha kwa ajili ya malipo yote halali (pamoja na noti); mabenki; fedha za kigeni na usimamizi juu ya mambo yanayohusika na fedha za kigeni.
2.Leseni za Viwanda na Takwimu.
3.Elimu ya Juu.
4.Maliasili ya Mafuta, pamoja na mafuta yasiyochujwa ya motokaa na mafuta aina ya petroli na aina nyinginezo za mafuta au bidhaa za mafuta, na gesi asilia. 5. Baraza la Taifa la Mitihani Tanzania na mambo yanayohusika na kazi za Baraza hilo.
6.Usafiri na Usafirishaji wa Anga.
7.Utafiti.
8.Utabiri wa Hali ya Hewa.
9.Takwimu.
10.Mahkama ya Rufaa ya Jamhuri ya Muungano.
11.Uandikishaji wa vyama vya siasa na mambo mengine yanayohusiana nayo.
Ukiondoa mambo hayo, yapo pia mambo mengine ya ziada ambayo yameingizwa katika Muungano kwa Bunge tu kutunga sheria na kutangaza kwamba zitatumika hadi Zanzibar.
Mfano wa masuala kama hayo ni Uvuvi wa Bahari Kuu na Tume ya Utawala Bora na Haki za Bianadamu. Yapo baadhi yake kwa mfano Usafiri wa Baharini ambapo Zanzibar ilikataa kutekeleza sheria iliyopitishwa na Bunge na hatimaye ikatunga sheria yake yenyewe kuhusiana na suala hilo.
Aidha, kuunganishwa kwa vyama vya TANU na ASP na kuzaliwa CCM huku chama hicho kipya kikijipa madaraka juu ya vyombo vyengine vyote vya maamuzi katika nchi ikiwemo Serikali na Bunge na Baraza la Wawakilishi ilikuwa ni mtihani mkubwa na ukiukwaji wa mkataba wa Muungano. Dhana hiyo ya Chama kushika hatamu iliyoasisiwa na Mwalimu Nyerere, lengo lake lilikuwa ni kujilimbikizia madaraka yeye na Chama alichokuwa akikiongoza kama milki yake binafsi.
Chini ya mfumo huo, CCM iliweza kutoa maagizo na maamuru mazito bila ya kujali madaraka ya Serikali ya Zanzibar yaliyotolewa kupitia Mkataba wa Muungano na hivyo kujinyakulia uwezo wote wa kuitawala Zanzibar ipendavyo huku viongozi wa Zanzibar wanaohoji wakituhumiwa kwamba wanapinga nidhamu ya Chama.
                                                                        
MATATIZO YATOKANAYO NA KIINI CHA TATIZO
Waheshimiwa Waandishi wa Habari
Kiini cha tatizo la msingi la Muungano ambalo kwa mtazamo wangu ni muundo wake unaotokana na tafsiri potofu ya Mkataba wa Muungano ndicho kimepelekea kujitokeza kwa matatizo mengine katika miaka 49 hii na ambayo yanaongezeka kila uchao.
Mtu anapoangalia matatizo au hizi zinazoitwa kero, atagundua kuwa karibu yote yanatokana ama na mshirika mmoja (mara nyingi Zanzibar) kutokuuamini au kuutilia shaka upande mwengine, au mshirika wa pili (mara nyingi Tanganyika ikivaa joho la Muungano), huku ikiamini kwamba ina haki ya moja kwa moja kuamua na kutekeleza mambo fulani bila ya kulazimika kupata ridhaa ya upande wa pili ambao inahisi kama imeubeba tu. Ukiangalia kwa undani utagundua kuwa tatizo linarudi kwenye muundo.
Zanzibar haifahamu mamlaka ya Muungano katika Serikali ya Muungano yanaishia wapi ambapo mamlaka kwa mambo yasiyo ya Muungano kwa ajili ya Tanganyika yanaanza.
Tanganyika nayo kwa kuwemo kwake katika Serikali ya Muungano kunaifanya ishindwe kufahamu ni vipi na wapi Zanzibar inapata mamlaka ya kuhoji mambo ambayo yameshatamkwa kwamba ni ya Muungano hata kama hayakuwemo katika Mkataba wa asili wa Muungano. Hali hii inaonekana katika kila kile kinachoitwa “kero”za Muungano.
Mifano inaweza kutolewa kwa takriban mambo yote, lakini kwa madhumuni ya mkutano huu na waandishi wa habari tuchukue mifano ya mambo matatu yafuatayo yanayozusha malalamiko nayo ni:
1. Umilikaji wa Mafuta na Gesi Asilia.
2. Uchangiaji katika gharama za Muungano na mgawanyo wa mapato yanayotokana na Muungano.
3. Uwakilishi wa Zanzibar katika Bunge la Muungano.
NAFASI YA ZANZIBAR KATIKA MUUNGANO
Waheshimiwa Waandishi wa Habari
Kwa kuendelea, ni vyema sasa tuangalie nafasi ya Zanzibar katika Muungano huu, hasa kufuatia kauli za kuidhalilisha Zanzibar zilizotolewa na wanasiasa wa Tanganyika hivi karibuni wakiongozwa na Waziri Mkuu, Mizengo Kayanza Peter Pinda.
Kutokana na kule kule kujaribu kujisahaulisha kuwepo kwa Mkataba wa Muungano ambao ndio sheria kuu (grundnorm) ya Muungano na kuifanya Katiba inayoitwa ya Jamhuri ya Muungano ionekane kuwa ndiyo Katiba mama na hivyo kuikweza kwamba eti iko juu ya Katiba ya Zanzibar, zimetolewa kauli kwamba kufuatia hatua ya kuungana na Tanganyika, Zanzibar imepoteza hadhi na sifa ya kuwa nchi.
Waliosema hivi wanasahau kwamba Zanzibar ina Katiba yake ambayo ina hadhi sawa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano, na kwamba zote mbili zinapaswa kutafsiri kisawa sawa Makubaliano ya Muungano.
Katiba ya Zanzibar inatamka wazi wazi kwamba Zanzibar ni nchi. Utangulizi wa Katiba hiyo ambao unaeleza dhamira ya Wazanzibari wakiwa ndiyo wenye Katiba hiyo unabainisha wazi wazi dhamira ya Wazanzibari kulinda na kudumisha nchi yao na yale yote yanayoitambulisha Zanzibar kama nchi.
Huko nyuma kabla ya Marekebisho ya Kumi ya Katiba ya Zanzibar ya 1984 yaliyopitishwa mwaka 2010, ni bahati mbaya kwamba baadhi ya watu walikuwa wakinukuu vibaya kifungu cha (1) cha Katiba ya Zanzibar kilichokuwa kikisomeka kwamba, “Zanzibar ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania” kumaanisha kwamba kwa kuwa kwake sehemu ya Jamhuri ya Muungano kunaiondolea na kuipotezea Zanzibar hadhi yake ya kubakia kuwa nchi.
Tafsiri hiyo haikuwa sahihi kama ilivyofafanuliwa na Jaji Abdullahi D. Zuru kutoka Nigeria, ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Tume ya Kupitia Sheria (Law Review Commission) Zanzibar.
Jaji Zuru katika maelezo yake alisema kuwa anaamini kwamba waanzilishi wa hatua ya kuzileta pamoja Zanzibar na Tanganyika kuwa Jamhuri moja, hawajakusudia kuwa hatua hiyo ipoteze (erode) uhuru wa nchi yoyote kati ya nchi mbili kamili zilizohusika.
Kinyume na hayo, maoni yake ni kwamba nia ilikuwa kuimarisha uhuru wa kila moja ya nchi hizo mbili sambamba na ule wa Muungano utakaozaliwa. Mtaalamu huyo anafahamisha kwamba kisheria, “Haki mbili zikikutana ndani ya mtu mmoja, ni sawa na kusema kwamba ziko ndani ya watu wawili.”
Aidha, alisema ni imani ya Tume yake kabisa kuwa ulipoundwa Muungano, Zanzibar ilikusudia na ilisisitiza juu ya kuendeleza mamlaka yake ndani ya utaratibu wa Muungano. Na hapa namnukuu:
“Kutokana na haya, tunaamini kwamba hadhi ya Zanzibar kama inavyoelezwa katika kifungu cha (1) imepotoshwa kwa sababu (kifungu) hakielezi nia ya wenye katiba (sponsors of this constitution) na madaraka yaliyotolewa na watu wa Zanzibar…”
VIPI TUTOKE HAPA TULIPO?
Waheshimiwa Waandishi wa Habari
Inakaribia miaka 49 sasa tangu uundwe Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Kulikuwa na wakati wa kutosha kurekebisha kasoro zilizopo. Hilo halikuwezekana kutokana na ubabe wa Mwalimu Nyerere ambaye aliamua kuwatia shemere Wazanzibari na kuhakikisha Muungano unakwenda kama alivyotaka yeye hata baada ya “kuondoka madarakani”.
Si jambo la kuficha kwamba wananchi wa pande zote mbili za Muungano wamechoshwa na unafiki uliopo na wanadai mfumo na muundo mpya wa Muungano utakaoweka misingi mipya ya ushirikiano.
Katika mijadala mbali mbali inayoendelea katika ukusanyaji wa maoni ya wananchi, vyama vya siasa na taasisi nyengine za kijamii kumetolewa hoja kwamba suluhisho la matatizo niliyoyafafanua hapo juu na mengine mengi yanayoukabili Muungano huu, kumejitokeza mapendekezo yanayoelekeza kwamba ufumbuzi wake ni muundo wa Serikali Moja, Serikali Mbili zilizopo sasa pamoja na marekebisho kadhaa au Serikali Tatu.
Kwa upande wa Zanzibar, wananchi walio wengi wamependekeza kuwepo kwa Muungano wa Mkataba (Treaty based Union) kama njia bora ya kudumisha mahusiano makongwe kati ya Zanzibar na Tanganyika.
Kwa upande wangu, siamini kama Serikali Moja, Mbili au Tatu zitaweza kumaliza matatizo yaliyopo ya Muungano na hasa kule kutokuaminiana kukubwa kulikojengeka kutokana na matatizo hayo kuachwa muda mrefu bila ya kushughulikiwa au kushughulikiwa kwa njia za hotuba za kisiasa zaidi zisizofuatiwa na utekelezaji wowote. Sababu zangu za kutoiona mifumo hiyo kama njia sahihi ya ufumbuzi wa matatizo yanayotukabili ni hizi zifuatazo.
Serikali Moja:
Mfumo wa Serikali moja umekuwa ukitajwa kuwa utaondoa manung’uniko na kelele zote kuhusu matatizo ya Muungano lakini bado unaonekana kuwa na matatizo yafuatayo:
1. Mfumo huu utazifuta kabisa nchi za Tanganyika na Zanzibar na kuwa na nchi moja yenye mamlaka moja inayosimamiwa na Serikali moja.
2. Ingawa mfumo huu unaweza kuungwa mkono na Watanganyika walio wengi, Wazanzibari hawawezi kuukubali kabisa mfumo huu kwa sababu utafuta utambulisho wao na historia yao.
3. Katika mfumo huu wa kuwa na nchi moja yenye mamlaka moja, Zanzibar itachukuliwa kama eneo jengine lolote la Tanzania na hivyo kutokuwa na uwezo wa kujiletea maendeleo yake na badala yake itategemea maendeleo yatakayopangwa na Serikali kuu kulingana na rasilimali zitakazotengwa kwa ajili ya eneo la Zanzibar kama inavyopangwa kwa maeneo mengine.
Serikali Mbili:
Mfumo wa serikali mbili uliopo hivi sasa una mkanganyiko wa mambo kadhaa kwa mfano:
1. Kutokuwepo kwa mshirika mmoja wa asili wa Muungano yaani Tanganyika. Hivyo linapotokea tatizo la Muungano badala ya kukutana pande mbili za Muungano na kujadiliana kwa misingi ya usawa sasa majadiliano yanakuwa baina ya Serikali ya Muungano na Serikali ya Zanzibar. Majadiliano ya namna hii yanakosa misingi ya haki na usawa.
2. Mabadiliko ya Katiba yaliyomuondoa Rais wa Zanzibar kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano yalikwenda kinyume kabisa na makubaliano ya awali ya Muungano. Mabadiliko haya yanamuondoa mmoja wa washirika wakuu katika Serikali ya Muungano ambaye ni Rais wa Zanzibar.
3. Kumekuwa na mkanganyiko vile vile kwa mambo ya Zanzibar ambayo siyo ya Muungano lakini mambo hayo yanashughulikiwa na Serikali ya Muungano katika ngazi zote za kimataifa. Kwa mfumo huu, Tanganyika inatumia jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kujifaidisha kwa mambo yote yasiyo mambo ya Muungano katika nyanja za kimataifa. Kama vile elimu, afya, kilimo, mazingira, michezo, utamaduni, mawasiliano, miundombinu, usafiri baharini na angani.
4. Aidha, mfumo uliopo wa Serikali mbili hautoi fursa ya wazi kwa upande mmoja wa Muungano (Tanganyika) kutetea maslahi yake ndani ya Muungano.
5. Wabunge wa Zanzibar wanashiriki katika Bunge la Muungano kujadili mambo ambayo siyo ya Muungano.
6. Mfumo uliopo unaochanganya mamlaka mbili (ile ya Serikali ya Muungano kwa mambo yote ya Muungano na ile ya Tanganyika kwa mambo yake yasiyokuwa ya Muungano) unaleta mkanganyiko mkubwa katika suala la kujua mipaka ya gharama za uendeshaji wa Muungano na mapato yanayotokana na taasisi za Muungano.
Ushahidi mwengine wa wazi wa kwamba mfumo uliopo umeshindwa kufanya kazi na wala hauwezi kurekebishika ni kwamba katika miaka 20 iliopita kumeundwa Tume na Kamati 8 kwa upande wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Tume na Kamati 13 kwa upande wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar mbali na kuwepo kwa Kamati ya Kudumu ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano ikiwajumuisha Waziri Mkuu wa Serikali ya Muungano na Makamu wa Pili wa Rais (zamani Waziri Kiongozi) wa SMZ lakini zote zimeshindwa kutatua matatizo ya Muungano na badala yake yamekuwa yakizidi kila uchao.
Serikali Tatu:
Baadhi ya vyama vya siasa na hata wasomi wa sheria wamekuwa wakipendekeza mfumo wa Serikali tatu (Serikali ya Muungano, Serikali ya Tanganyika na Serikali ya Zanzibar) kama suluhisho la matatizo ya Muungano. Hata hivyo, mfumo huu nao kwa sasa unaonekana bado hautaondoa manung’uniko kwa upande wa Zanzibar kwa sababu:
1. Mfumo wa Shirikisho la Serikali Tatu utatoa mamlaka ya ndani kwa nchi mbili zinazounda Muungano huu na kuwa na Serikali zake za kusimamia mamlaka hayo lakini bado mamlaka ya kidola yatabaki katika Serikali ya Muungano.
Madai makubwa yanayotolewa na Zanzibar hivi sasa yanahusu kurejesha ‘sovereignty’ ili kuifanya Zanzibar, serikali yake na viongozi wake wawe na hadhi ya kutambuliwa kitaifa na kimataifa. Hilo halitapatikana katika mfumo wa Serikali tatu kwa sababu:
2. Mamlaka yanayoshikiliwa na Serikali ya Muungano ambayo ndiyo itakayoziwakilisha nchi mbili kimataifa bado ina nafasi kubwa ya kuweza kutumika kumfaidisha mshirika mkubwa zaidi katika Muungano huo (Tanganyika) kuliko kwa mshirika mdogo (Zanzibar) kwa kule tu kujiona kwake ni mkubwa (big brother attitude).
3. Upo uwezekano wa kuendelea kuwepo kwa kutoaminiana kutokana na kila nchi kuwa na Serikali yake na hivyo kuwa na chombo cha kupanga mambo yake, hali inayoweza kuifanya Serikali ya Muungano ijikute haina uwezo wa kuzisimamia Serikali hizo za mamlaka ya ndani na hivyo kupoteza uhalali wake wa kisiasa.
4. Iwapo mambo ya Muungano yatabaki kama yalivyo au yatarekebishwa kwa uchache, kuwepo kwa mfumo wa Serikali tatu hakutorudisha mamlaka ya Zanzibar kupanga na kusimamia uchumi wake.
MFUMO MPYA WA MUUNGANO WA MKATABA:
Waheshimiwa Waandishi wa Habari
Kama nilivyotangulia kueleza, tumedumu na Muungano wa Katiba kwa miaka 49 ambao pamoja na mafanikio ya kuziweka nchi zetu mbili pamoja katika kipindi chote hicho, bado umeshindwa kutujengea kuaminiana kwa dhati na zaidi umeshindwa kuyatatua matatizo ya msingi yanayotokana na maumbile ya mfumo huo.
Ulimwengu wa sasa umeshuhudia aina mpya ya mahusiano kati ya nchi huru ambao hutoa nafasi ya mashirikiano kwa maeneo yanakayokubaliwa na nchi husika huku kila nchi ikibaki na mamlaka yake kama nchi kamili. Mfumo huu kisheria unaitwa‘CONFEDERATION’ ambao kimsingi ni Muungano wa Mkataba (Treaty based Union).
Katika mfumo huu, yale maeneo ya ushirikiano huwekwa katika mkataba au mikataba baina ya nchi zilizoamua kushirikiana na hutoa fursa ya kurekebishwa kila mahitaji yanapojitokeza kwa kadiri na kwa mujibu wa makubaliano yaliyomo kwenye mkataba au mikataba hiyo.
Umoja wa Ulaya (European Union – EU) ni mfano mzuri wa muungano wa aina hii ambapo nchi wanachama zinashirikiana katika maeneo mengi yaliyomo katika Mikataba tofauti lakini kila nchi mwanachama imebaki kuwa na hadhi yake kama nchi na kubaki na uanachama wake katika Umoja wa Mataifa (UN) na hata katika mashirika mengine ya kimataifa.
Waheshimiwa Waandishi wa Habari
Kwa kumalizia, nasema kuwa kutokana na hoja nilizozieleza hapo juu, mimi nimependekeza katika maoni yangu kwa Tume ya Maoni ya Katiba kuwa, baada ya uzoefu wa miaka 49 wa Muungano wa Katiba (Constitutional Union) kati ya Zanzibar na Tanganyika ambao baadhi ya matatizo yake ya kimaumbile nimeyaeleza na kuyafanua hapo juu, sasa Zanzibar na Tanganyika ziingie katika mfumo wa “CONFEDERATION”kupitia Muungano wa Mkataba (Treaty based Union).
Chini ya mfumo huo wa Muungano wa Mkataba, kuwe na Serikali mbili ambapo Jamhuri ya Tanganyika itakuwa na Serikali yake na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar itakuwa na Serikali yake, zote mbili zikiwa na mamlaka kamili Kitaifa na Kimataifa. Kisha Serikali hizo mbili zitafunga mkataba wa mashirikiano baina yao ambao unaweza ukapewa jina la ‘Tanzanian Union Treaty’. Yale maeneo yatakayokubaliwa kuwa chini ya ushirikiano wa nchi mbili huru yatasimamiwa na Kamisheni ya Muungano (Tanzanian Commission), kama ilivyo kwa Kamisheni ya Ulaya (European Commission) au jina jengine lolote litakalokubaliwa na nchi mbili hizo.
Ahsanteni sana kwa kunisikiliza
________________________________________
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amesema kuwa, uchumi wa nchi hiyo utaendelea kukua maradufu kutokana na mifumo bora ya uwekezaji iliyopo, hali itakayosaidia pia kushindana katika soko la Afrika Mashariki. Mizengo Pinda amesema, fursa muhimu ndizo zinazovutia wawekezaji kwenda nchini humo na pato la nchi kuendelea kukua maradufu. Pinda amesema hayo wakati wa uzinduzi wa duka la kusambaza bidhaa za Beko kutoka Uturuki, zikiwemo televisheni, friji na majiko ya umeme. Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amesisitiza kuwa, serikali ya nchi hiyo imeweka mikakati madhubuti kuhakikisha kwamba, mwenendo wa ukuaji uchumi unaendelea. Ameongeza kuwa, mara zote Tanzania imekuwa katika kutafuta masoko na wawekezaji, hivyo kuzinduliwa kwa duka hilo ni ishara kuwa nchi imepiga hatua kwenye maendeleo. Licha ya Mizengo Pinda kuelezea mwenendo wa ukuaji uchumi nchini Tanzania, lakini kupanda kwa gharama za maisha kunaendelea kuripotiwa katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki na kuyafanya maisha ya Mtanzania wa kawaida kuwa magumu.
Jeshi la Nigeria limemtia mbaroni Muhammad Zangina mmoja wa viongozi wa kundi la Boko Haram. Taarifa ya jeshi la Nigeria imesema, Zangina ametiwa mbaroni karibu na mji wa Maiduguri. Jeshi la Nigeria limesema kuwa, Zangina anatuhumiwa kuhusika ana mashambulio kadhaa ya kigaidi dhidi ya raia na vikosi vya polisi katika mji wa Maiduguri na kwamba, ametiwa mbaroni masaa machache kabla ya kutekeleza mpango wa mashambulio mengine katika mji huo. itakumbukwa kuwa, serikali ya Nigeria ilikuwa imetenga kitita cha dola laki moja na sitini elfu kama zawadi kwa atakayetoa taarifa za uhakika za kutiwa mbaroni Muhammad Zangina.
Kundi la Boko Haram linatuhumiwa kuhusika na mauaji mengi yaliyofanyika nchini Nigeria, na wanachama wake wamekuwa wakisakwa kwa udi na uvumba na jeshi la nchi hiyo. Hadi sasa mamia ya watu wameshapoteza maisha yao na majengo kadhaa ya serikali na makanisa kuchomwa moto kutokana na mashambulio yanayofanywa na kundi hilo kaskazini mwa Nigeria.
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Russia amesema kuwa, takwa la waasi wa Syria la kutaka kuachia ngazi Rais Bashar al-Assad wa nchi hiyo kama sharti la kufanya mazungumzo, halitekelezeki. Sergey Lavrov amesema kuwa, sharti hilo la waasi la kushiriki katika mazungumzo ya kitaifa halitekelezeki. Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Russia amewataka waasi hao kutoa mapendekezo yenye lengo la kuupatia ufumbuzi wa kisiasa mgogoro wa Syria.
Wakati huo huo, kwa mara nyingine tena Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Russia imetoa taarifa na kusisitiza kwamba, kuna udharura wa mgogoro wa Syria kutatuliwa kwa njia za amani na kwamba, njia za kijeshi hazipaswi kutumika. Hayo yanaripotiwa huku, Qatar, Saudia, Uturuki zikishirikiana na Marekani zimeendelea kuchochea machafuko nchini Syria na hivyo kukwamisha jitihada za kuutafutia ufumbuzi mgogoro wa nchi hiyo kwa njia za amani.