Monday, January 14, 2013

WABUNGE NCCR MAGEUZI, WAKIONGOZWA NA MWENYEKITI TAIFA JAMES MBATIA WANUSURIKA KIPIGO, MTWARA.

Mwenyekiti Taifa wa chama cha NCCR MAGEUZI, James Mbatia, wa tatu kutoka kushoto kabla hajawahutubia wananchi wa manispaa ya mtwara mikindani, katika uwanja wa mashujaa mjini Mtwara.
MWENYEKITI wa NCCR Mageuzi, James Mbatia jana alijikuta katika wakati mgumu baada ya kulazimika kufungiwa katika ofisi ya NCCR-Mageuzi wilaya ya Mtwara Mjini kutokana na baadhi wa wananchi walioudhuria mkutano wake wa hadhara uliofanyika uwanja wa Mashujaa, kutaka kumdhuru kwa madai kwamba hawakuridhishwa na hotuba yake.


Mbatia alianza kurushiwa chupa tupu za maji alipokuwa akitoka uwanjani hapo baada ya kukatisha hotuba yake kutokana na baadhi ya wananchi kupinga kauli zake kwa madai hawamuelewi.


Kauli inayodaiwa kumgharimu Mbatia ni ile ya ‘Iwapo gesi itatoka Mtwara’ ndipo wananchi hao walipoanza kupaza sauti wakisema “Hatukuelewi…hatukuelewi” hata hivyo Mbatia aliendelea kuhutubia hali iliyosababisha wananchi hao wapaze sauti zao kwa kuimba nyimbo.
Mbunge Machalli akiuhutubia umati uliojaa.

                                                                           
“Haitoki… Hatoki…Haitoki…” sauti za wananchi zilisikika na hata Mbatia alipojaribu kuwatuliza wananchi hao kwa kusema ‘gesi kwanza…. Gesi kwanza” baadhi waliitikia na wengine waliendelea kusema hawamuelewi.


Hali hiyo ilimlazimisha Mbatia kukatisha hotuba yake saa 11.25 jioni na aliondoka uwanjani hapo kwa kutembea kwa miguu hali iliyotoa mwanya kwa wananchi kumrushia chupa tupu za maji. 

Mwenyekiti huyo akiwa ameambatana na wabunge wa chama hicho, Moses Machali (Kasulu Mjini) na Agripina Buyogela (Kasulu Vijijini) mkoani Kigoma, walielekea kituo cha polisi kilichopi karibu na uwanja huo na baadaye alielekea ofisi za NCCR Mageuzi wilaya.


Alipotafutwa jana kuzungumzia suala hilo, Mbatia hakupatikana kupitia simu zake zote za mkononi hata wabunge Buyogela na Machali pia simu zao zilikuwa zimefungwa.


Kamanda wa Polisi mkoa wa Mtwara, Mary Nzuki alisema hakuwa na taarifa za Mbatia kunusurika kupigwa ila aliahidi kufuatilia suala hilo. 

“Ninachojua Mbatia yuko hapa kweli na amefanya mkutano wake, baada ya mkutano ule akiwa anatoka eneo la mkutano alikuwa anasindikizwa na wafuasi wake ambao walikuwa wanamshangilia. Sasa kama walipofika huko mbele walimgeuka hilo sijui”, alisema Nzuki.

Pinda afunguka.
Waziri Mkuu Mizengo Pinda.
Wakati huohuo, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda amewasihi wakazi wa mikoa ya Kusini kuwa wavumilivu na kuruhusu mradi wa kusafirisha gesi kutoka mikoa hiyo kwenda Dar es Salaam ufanikiwe kwa kuwa una faida kubwa kwao.


Pinda alitaja manufaa hayo kuwa ni pamoja na ajira kwa vijana watakaoshiriki katika ujenzi huo, ujenzi wa viwanda na miundombinu na upanuzi wa Bandari ya Mtwara.


“Nilishangaa kuona wananchi wa Mtwara wanaandamana kupinga ujenzi wa bomba la gesi asilia kutoka huko kwenda Dar es Salaam. Mradi huo ndiyo utakuwa suluhisho la tatizo la umeme nchini, ”alisema Pinda na kuongeza:


“Wananchi wa Mtwara wawe wavumilivu, watanufaika sana na mradi huo. Mradi utajumuisha upanuzi wa Bandari ya Mtwara pamoja na ujenzi wa Viwanda mbalimbali vitakavyosaidia kukuza uchumi wa maeneo yao kwa kutoa ajira na kukuza biashara zao.”
Mb.Moses Machali, na James Mbatia kulia.




Mhe.James Mbatia akiwahutuba wananchi wa manispaa ya mtwara mikndani.
                                                                              

No comments:

Post a Comment