Sakata la gesi asilia inayopatikana katika kijiji cha
Msimbati kilichopo wilaya ya Mtwara Vijijini mkoani Mtwara, limeendelea
kuchukua sura kila leo baada ya wabunge wake kurushiana madongo kupitia radio
zilizopo mkoani humo huku kila mmoja akimshambulia mwenzake kwa kudai siyo
mwajibikaji kwa wananchi.
Madongo hayo yanafuatia baada ya mbunge wa jimbo la
Mtwara mjini Asnein Murji (CCM), kuweka wazi msimamo wake wa kuungana na
wananchi wa mkoa wa Mtwara wanaopinga kuhamishwa gesi asilia kupelekwa jijini
Dar es Salaam.
Akizungumza katika kipindi cha Powerful Voice
kinachorushwa na Safari radio mjini Mtwara jana Jumapili, Waziri wa TAMISEMI na
mbunge wa Mtwara vijijini Hawa Abdul rahmaan Ghasia amesema kuwa, kitendo cha
Murji kuungana na wananchi kupinga gesi kuhamishwa kwenda jijini Dar es Salaam
ni unafiki kwani hakuna jambo lolote alilolifanywa kwa manufaa ya wananchi.
Waziri wa nchi ofisi ya waziri mkuu (TAMISEMI), na mbunge wa Mtwara Vijijini. |
Waziri Ghasia amesema kuwa, Murji hana cha kujivunia
kwa kuwa ameshindwa kuwasemea wananchi waliompa dhamana ya kuwawakilisha na
kuwasemea matatizo yao bungeni.
Ameeleza kuwa, kama suala la kupinga gesi
kuhamishiwa jijini Dar es Salaam halikupaswa kutokea wakati huu lilipaswa
kupingwa tangu bungeni, lakini mbunge huyo hakufanya hivyo kwani tangu
amechaguliwa na wananchi kuwawakilisha bungeni hajawahi kuuliza swali ama kutoa
hoja yoyote kuhusiana na gesi.
Pia amesema kuwa, Murji hajawahi kufanya mikutano
kuongea na wananchi wake ili kutoa elimu juu ya suala la gesi kwani yeye kama
kiongozi alitakiwa afanye hivyo kwa wananchi waliompa dhamana huku akisema kuwa
mbunge huyo ana siasa za majitaka.
Kwa upande wake mbunge wa jimbo la Mtwara mjini Asnein
Murji (CCM), amesema kuwa, suala la gesi bado wananchi hawajashirikishwa, hivyo
ni lazima chombo husika kifanye hivyo kabla ya kuihamisha gesi kuelekea jijini
Dae es Salaam.
Mbunge wa Mtwara Mjini, Mhe.Asnain Murji. |
Akizungumza akizungumza katika kipindi cha Amka na
Pride kinachorushwa na kituo cha Pride fm radio mapema hii leo, Murji amesema
kuwa, wananchi wa Mtwara hawapingi uhamishwaji wa gesi hiyo kwenda jijini Dar
es Salaam, bali wanachotaka kufahamu ni namna gani watanufaika na gesi hiyo
kwani wananchi hao walikuwa na matumaini makubwa na rasilimali hiyo.
Murji amesema kuwa, suala la kutoa elimu juu ya
masuala ya gesi, hayakupaswa kufanywa na yeye kama ambavyo waziri Ghasia
anavyodai ila lilitakiwa kufanywa na TPDC ambao ndiyo wana dhamana ya na gesi.
Aidha Murji amesema kuwa, suala la kuongea na
wananchi analifanya sana na hata sasa yupo katika kuzungumza na wananchi hivyo
msimamo wake ni kupinga gesi kupelekwa jijini Dar es Salaam huku akimshangaa
waziri Ghasia kwa kusema kuwa hakuna kitu alichokifanya katika jimbo lake
wakati hata yeye hana cha kujivunia jimboni mwake.
Amesema kuwa, anamshangaa waziri Ghasia kujisifia
kujenga barabara Mtwara mjini wakati katika jimbo lake hakuna barabara ya lami
yenye kueleweka.
John Samwel Malecela, waziri mkuu mstaafu. |
Wakati huo huo Waziri Mkuu Mstaafu na Mwanasiasa Mkongwe nchini,
John Malecela, ametoa wosia kuhusu mgogoro wa gesi akiiomba Serikali kufanya
kila iwezalo ili kuhakikisha kuwa wakazi wa Mtwara wananufaika kwanza na
rasilimali hiyo.
Malecela ametoa kauli hiyo alipotakiwa kutoa
maoni yake kuhusu mgogoro wa kusafirisha gesi kutoka mkoani Mtwara kwenda
jijini Dar es Salaam unaoendelea kushika kasi katika siku za hivi karibuni
ambapo amesema kuwa, “Ukiwa karibu na waridi unatakiwa kunukia waridi. Wakazi
wa Mtwara nao wanatakiwa wanukie waridi,” amesema Malecela.
Aidha Malecela amesema, pamoja na ukweli kwamba rasilimali
inayopatikana nchini ni kwa ajili ya watanzania wote, ukweli kwamba wakazi wa
eneo inakopatikana rasiliamali hiyo wanapaswa kunufaika nayo, haukwepeki huku
akisema kuwa, licha ya gesi hiyo kuwa ya watanzania wote, Serikali inatakiwa
kuandaa utaratibu ili kuhakikisha kuwa wananchi wa Mtwara wananufaika zaidi na
rasilimali hiyo.
Ameongeza kuwa, umaskini uliokithiri katika baadhi ya mikoa
nchini ukiwamo mkoa wa Mtwara, ndio unaosababisha watu waanze kudai rasilimali
zinazotoka katika maeneo yao wakiamini kuwa ndio mwanzo wa ukombozi wao.
Katika hatua nyingine Kikongwe Somoe Issa (90) ambaye ni mkuu wa
kaya ya Msimbati, kijiji ambacho gesi asilia inavunwa ameionya Serikali
kutoendelea na mpango wake wa kusafirisha gesi kwenda jijini Dar es Salaam na kuwa
iwapo itapinga bomba hilo litasafirisha maji badala ya gesi.
Kikongwe huyo ambaye haoni wala kusikia amesema kuwa, hayupo
tayari kuona gesi hiyo ambayo imepatikana katika kijiji hicho ikiondoka mkoani
Mtwara.
No comments:
Post a Comment