Friday, January 4, 2013

VIONGOZI MAARUFU WALIOFARIKI DUNIA 2012.

Marehemu Regia Mtema.
 MWAKA 2012 unayoyoma na tumeshuhudia ndani ya miezi 12 iliyopita tukipoteza baadhi ya viongozi maarufu serikalini, kanisani na katika tasnia ya habari waliofariki dunia,  baadhi yao ni hawa wafuatao:

Regia Mtema: Alifariki Januari 14, 2012 kwa ajali ya gari eneo la Ruvu Darajani, Pwani. Alikuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema na  Mbunge wa Viti Maalum wa chama hicho lakini pia alikuwa Waziri Kivuli wa Kazi na Ajira.
Jeremia Sumari: Alikuwa Mbunge wa Arumeru Mashariki kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM). Alifariki dunia usiku wa Januari 19, mwaka huu, aliwahi kuwa Naibu Waziri wa Fedha na Uchumi, alikuwa akisumbuliwa na uvimbe kwenye ubongo kwa muda mrefu.
Jenerali Ernest Mwita Kyaro: Alifariki Aprili 10, mwaka huu, aliwahi kuwa Mkuu wa Majeshi Tanzania kati ya mwaka 1988 - 1994 na aliwahi kuongoza majeshi yetu katika Vita ya Kagera kupambana Nduli Iddi Amini wa Uganda mwaka 1979.
Mohammed “Bob” Makani: Huyu alikuwa muasisi wa Chadema, alifariki dunia Juni 6, mwaka huu jijini Dar kwenye Hospitali ya Aga Khan. Aliugua kwa muda mrefu.
Hawa Ngulume: Aliwahi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Bagamoyo na Mbarali, alifariki dunia Agosti 30, mwaka huu katika Hospitali ya Jeshi ya Lugalo, jijini Dar es Salaam baada ya kusumbuliwa na maradhi ya kansa kwa kipindi kirefu.
Daud Mwangosi: Alikuwa mwandishi wa habari wa Channel Ten mkoani Iringa na Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari mkoani humo. Aliuawa kwa bomu Septemba 2, mwaka huu wakati wa vurugu kati ya polisi na wafuasi wa Chadema katika Kijiji cha Nyololo wilayani Mufindi mkoani humo.
Liberatus Barlow: Huyu alikuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, aliuawa kwa kupigwa risasi na watu wanaodhaniwa kuwa majambazi usiku wa kuamkia Oktoba 13, mwaka huu katika eneo la Kitangiri, Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza. Ni RPC wa kwanza nchini kuuawa kwa risasi.
Mhashamu Askofu Aloysius Balina: Alikuwa Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Shinyanga, alifariki dunia Novemba 6, mwaka huu akiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando jijini Mwanza alipokuwa akitibiwa.
Jackson Makwetta: Huyu alikuwa waziri wa zamani wa sayansi, teknolojia na elimu ya juu na Mbunge wa Njombe, alifariki dunia Novemba 18, mwaka huu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, jijini Dar es Salaam, alikuwa akisumbuliwa na maradhi ya moyo.
Marehemu Jackson Makwetta.

No comments:

Post a Comment