Mbunge wa jimbo la Kilindi, mkoani Tanga (CCM), Beatrice Shelukindo |
MBUNGE
wa Kilindi (CCM), Beatrice Shelukindo ametangaza kuchukua kile
alichokiita uamuzi mgumu ili kuhakikisha kuwa Mbunge wa Monduli (CCM),
Edward Lowassa anamrithi Rais Jakaya Kikwete katika Uchaguzi Mkuu wa
mwaka 2015.Shelukindo alitoa kauli hiyo Jumapili wakati akiwasalimia
wakazi wa Monduli baada ya kukaribishwa kuchangia ujenzi wa Hosteli ya
KKKT katika sherehe za kukaribisha Mwaka Mpya zilizofanyika nyumbani kwa
Lowassa ambazo pia zilihudhuriwa na makada kadhaa wa CCM.
Jana alipoulizwa kuhusu kauli hiyo, Shelukindo alisema: “Ni kweli
mimi ni muumini wa Lowassa, ila pale (mkutanoni) sikumtaja kwa sababu
najua chama kina taratibu zake na muda wa mchakato wa kumpata Rais
haujafika.”
“Niliposimama niliwaeleza kuwa nisingeweza kuchangia fedha nyingi kwa
sababu watu wangu wana njaa huko Kilindi. Pia kule (Kilindi)
tunaendesha harambee ya aina hiyohiyo. Ila nikawaambia zawadi yangu kwa
Wanamonduli ni kufanya uamuzi mgumu ili mwaka 2015 apatikane Rais
mzalendo na anayeweza kufanya uamuzi mgumu na kwa wakati.”
Shelukindo aliendelea: “Niliposema hivyo, umati uliibuka kwa shangwe
na kunitaka nimtaje nitakayeshirikiana naye, lakini nikawaambia kuwa huu
si wakati mwafaka ila baadaye nilichangia Sh500,000.”
Shelukindo alisema harambee hiyo ilitarajiwa kuchangishwa Sh100 milioni lakini zikapatikana Sh70 milioni.
Mbali na Shelukindo, makada wengine wa CCM waliohudhuria sherehe hizo
ni Mbunge wa Bariadi Mashariki, Andrew Chenge, Mbunge wa Kigoma Mjini,
Peter Serukamba na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Hamis Mngeja.
Awali, akizungumza katika sherehe hizo, Lowassa aliwataka Watanzania
kutumia mwaka huu wa 2013 kufanya uamuzi mgumu katika kila changamoto
inayowakabili.
“Salamu zangu za Mwaka Mpya kwa Watanzania: Nawaomba wapitishe uamuzi
mgumu kwa kila changamoto watakazokabiliana nazo,” alisema.
Alisema
hatua hiyo ni muhimu katika kukabiliana na umaskini na kuongeza kuwa mtu
akiamua inawezekana.
Lowassa aliwahi kusema bungeni akiitaka Serikali kuwa na tabia ya
kupitisha ‘uamuzi mgumu’ katika kuwaondolea wananchi kero akisema bila
kuthubutu ni vigumu kukabiliana na changamoto.
Katika sherehe hizo, Lowassa pia alizungumzia taarifa zilizozagaa
mitandaoni kuwa sherehe yake hiyo ilikuwa ni ya kisiasa akisema:
“Wameandika katika mitandao ya kijamii kuwa kuna sherehe kubwa ya
kisiasa. Mimi nawaambia wa waache porojo hizo. Nimekuwa nikiandaa
sherehe hizi tangu mwaka 1995, wao wakitaka waige mfano huu.”
Chanzo MWANANCHI
No comments:
Post a Comment