TFF. |
Raisi anayemaliza muda wake TFF, Sir Leordiger Chillaer Tenga. |
KAMATI ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) imesema
kwamba wadau wote wanaweza kupata fomu za maombi ya uongozi wa TFF na Bodi ya
Ligi Kuu (TPL Board) kupitia kwenye tovuti ya shirikisho hilo.
Taarifa ya TFF imesema wote wanaopenda kugombea uongozi
katika vyombo hivyo wanaarifiwa kuwa wanaweza kupata fomu hizo kwenye tovuti ya
TFF (www.tff.or.tz) na wanatakiwa kulipia fomu hizo katika akaunti ya TFF namba
01J1019956700 iliyoko CRDB tawi la Holland House.
Taarifa imesema fomu zinatakiwa kuambatanishwa na risiti ya
malipo au karatasi za malipo ya benki na zirejeshwe kwa Katibu Mkuu wa TFF kwa
mkono au kwa barua pepe, tfftz@yahoo.com kabla ya saa 10 kamili alasiri ya
Januari 18 mwaka huu.
Taarifa imesema kwa wagombea wanaorejesha fomu kwa mkono,
watatakiwa kujiorodhesha na kusaini kwenye fomu ya orodha ya wagombea.
Katika taarifa nyingine, TFF imetoa pongezi kwa uongozi mpya
wa Chama cha Soka Rukwa (RUREFA) uliochaguliwa katika uchaguzi uliofanyika
Januari 10 mwaka huu.
Taarifa imesema ushindi waliopata viongozi waliochaguliwa
kuongoza chama hicho unaonyesha jinsi wajumbe wa Mkutano Mkuu wa RUREFA walivyo
na imani kubwa kwao katika kusimamia mchezo huo mkoani Rukwa.
TFF imeahidi kuendeleza ushirikiano wake kwa Kamati ya
Utendaji ya RUREFA chini ya Uenyekiti wa Blassy Kiondo aliyeibuka mshindi
katika uchaguzi huo uliofanyika mjini Sumbawanga.
“Uongozi huo mpya una changamoto nyingi, kubwa ikiwa ni
kuhakikisha unaendesha shughuli za mpira wa miguu mkoani Rukwa kwa kuzingatia
katiba ya RUREFA pamoja na vyombo vya mpira wa miguu vilivyo juu yake,”imesema
taarifa.
Viongozi waliochaguliwa katika uchaguzi huo ni Blassy Kiondo (Mwenyekiti), Gregory Seko (Katibu), John Maholani (Mjumbe wa Mkutano Mkuu TFF), Ayoub Nyaulingo (Mwakilishi wa Klabu TFF) na Gloria Ndawa (Mweka Hazina). Nafasi nyingine zitajazwa katika uchaguzi mdogo.
No comments:
Post a Comment