TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI.
TAREHE 07-01-2013.
Bw.Joel Nannauka akizungumza na waandishi wa habari wa Mtwara Press Club hawapo pichani, kuhusiana na usafirishaji wa gesi gafi kuelekea jijini Dar es salaam. |
Ndugu waandishi wa Habari kwanza
ningependa kuwashukuru sana kwa kuitikia wito wenu kuja hapa leo kuyasikiliza
yale ambayo nimekusudia kuyaongea.
Pili ningependa kuwapongeza sana
kwa namna mnavyoripoti habari hizi kila wakati bila kuchoka na kuyafuatilia
matukio na kueleza hoja na hisia za wananchi wa Mtwara kila kunapokucha.
Najua ziko shutuma zilizotolewa
na viongozi wa serikali kwamba wanaozungumzia jambo hili wanatafuta umaarufu wa
kisiasa,nadhani hiyo ilikuwa mbinu ya kuziba mdomo tusizungumze.Swala hili ni
nyeti na lina sura ya kitaifa ni wajibu wa kila mpenda maendeleo ya nchi hii
kulizungumzia kwa ustawi wa watu wetu,ndicho ninachofanya leo,uzalendo
unanitaka kufanya hivyo.
Nikinukuu maneno ya mpigania haki za wanawake nchini
Afghanistan Mama Malalai Joya aliyewahi kusema”The silence of Good people is
worse than the actions of Bad people ” Hivyo kukaa kwangu kimya ni
kubaya zaidi kuleta matendo mabaya ya mtu yeyote yule,ili nisiwe kwenye kundi
hilo naomba nivunje ukimya huo.
Nianze kwa kusema kuwa
ningependa kutoa maoni yangu kama mwananchi wa kawaida ninayeguswa na jambo
hili na ninatumia haki yangu ya kikatiba kwa mujibu ya ibara ya 18 kipengele
(A).
Ingawa ukweli utabaki kuwa mimi ni mwanachama wa chama cha mapinduzi na
historia inajieleza kuwa nimeshawahi
kuwa katibu msaidizi wa CCM wilaya na
mgombea wa ubunge katika kura za maoni mwaka 2010 katika uchaguzi wa ndani ya
chama kwa jimbo la Mtwara Mjini.
Tangu kuanza kwa vuguvugu la
mradi wa ujenzi wa bomba la gesi nimetumia muda mwingi kuwa Mtwara kuliko Dar es Salaam
ambako hasa ndiko ninakofanya shughuli zangu.
Kabla vuguvugu hili halijachukua
sura kubwa ya kitaifa yalikuwepo manun’guniko mengi kwa wananchi yaliyoonyesha
kutoridhishwa na kufanyika kwa mradi huu.
Ikumbukwe kuwa ingawa mkataba wa
kupata mkopo wa ujenzi wa bomba kutoka benki ya Exim china(Takribani usd 1Bill)
ulisainiwa nchini china tarehe 26 september 2011 na ujumbe uliiongozwa na
waziri wa wakati huo wa Nishati na Madini William ngeleja,kujulikana kwa
utekelezwaji wa mradi huu kwa watu wengi ulikuwa ni pale mheshimiwa Rais
alipozindua mradi wa kujenga mtambo wa kufua umeme kinyerezi tarehe
8/November/2012 ambao ungetokana na gesi kutoka Mtwara ikiungana na bomba la
songosongo,hapa ikiwa ni takribani mwaka mmoja kupita tangu kusainiwa.
Kwa kulitazama jambo hili
kutokea mbali na kwa kutoridhishwa na ukimya uliotawala kwa viongozi wa
serikali na wawakilishi wa wananchi,nilichukua hatua za makusudi kufanya
ufuatiliaji mbalimbali.
Hatua yangu ya kwanza ilikuwa kwenda TPDC ofisi ya
mkurugenzi tarehe12 december 2012 ikiwa ndiyo mwakilishi wa serikali
anayesimamia mradi huu ili kuhoji mambo kadhaa na kutoa mtazamo wangu wa
umuhimu wa kusimamishwa kwa mradi huu ili kusikiiliza kilio cha wananchi.
Ingawa
sikufanikiwa kuonana na mkurugenzi nilifanikiwa kukutanishwa na wakuu wa
kitengo cha malalamiko yanayohusu mradi huu ambao kwa ukweli ni kwamba
walisisitiza tatizo kubwa ni kutokuelewa kwa wananchi na kupuuza hoja yangu ya
msingi ya kutaka ujenzi wa bomba hili usimamishwe ili kusikiliza hoja za msingi
za wananchi.
Baada ya hapo nilichukua hatua
ya kuomba msaada wakisheria kutoka kituo cha sheria na haki za binadamu ili
kusitisha mradi huu kwa kuwasiliana na mkurugenzi wa kituo hicho Bi hellen Kijo
bisimba mnamo tarehe 17dec 2012 ambaye alinieleza kuwa alishatuma ujumbe wake
Mtwara na wako katika hatua za kuandika ripoti hivyo niisubirie.Kwa bahati
mbaya sana bado sijafanikiwa kuipata ripoti yao.
Sikuishia hapo,niliamua kuandika
barua kwa ngazi za manispaa ya Mtwara mnamo tarehe 18 dec 2012 ikiwa na madai
kadhaa na mapendekezo ya nini kifanyike kuhusiana na mradi huu.
Kati ya madai
yangu ilikuwa kumtaka meya wa manispaa kuitisha kikao cha haraka cha baraza la
madiwani kulijadili jambo hili kama la dharura wakiwa ndio wawakilishi wa
wananchi na kutoa msimamo wao kwa serikali kuitaka kusitisha mradi huu na
kusikiliza kilio cha wananchi.
Juhudi hii nayo haikuzaa matunda kwani sikupata
jibu lolote la barua yangu wala utekelezaji wake hadi hii leo.
Baada ya hapo nilishiriki
kikamilifu katika mijadala ya sera na vipindi mbalimbali vya redio nikihimiza
kusitishwa kwa ujenzi wa bomba hili hadi pale hoja za wananchi zitakapojibiwa
kama vile nilivyonukuliwa katika gazeti la mwananchi la tarehe 26 december 2012
ukurasa wa kumi ikiwa ni siku moja kabla ya kufanyika maandamano makubwa siku
ya tarehe 27.
Nimeeleza haya yote ili
kuonyesha kuwa kwa mtu yeyote anayeona mbali ni lazima alijua kuwa bila ya
kusikilizwa kwa kilio hiki cha wananchi ni lazima tungefika hapa tulipo na kuna
uwezekano wa kwenda mbali zaidi kuliko hapa kama hatua stahiki hazitachukuliwa.
Baada ya kusema hayo ningependa kutoa
masikitiko yangu kwa kauli za kejeli,dharau na kukatisha tamaa zilizotolewa na
viongozi waandamizi wa serikali Mh.Waziri Sospeter Muhongo na mkuu wa mkoa wa Mtwara(Joseph
Simbakalia) mara baada ya maandamano ya
tarehe 27 dec.
Pia napenda kueleza kusikitishwa na Rais Jakaya Kikwete kwa kauli
yake aliyoitoa kuhusu ujenzi wa bomba hili katika salamu zake za mwaka mpya,napenda
kutumia nafasi hii kumshauri Mh.Rais,Waziri wa Nishati na Madini na Mkuu wa
mkoa kupitia upya madai 9 yalisomwa siku ya maandamano ili kutoupotosha mjadala
na madai ya watu wa Mtwara.
Nimetoa rai hiyo kwasababu
ukipitia hotuba za viongozi hawa wote utagundua kuwa aidha wamepewa taarifa
zisizo sahihi kuhusu madai ya wanamtwara ama wamefanya haraka kujibu au
hawajaelewa kabisa madai ya wanamtwara.
Kwani kilichofanyika si kujibu madai yao
bali kuonyesha jinsi ambavyo hawako tayari kuwasikiliza,nadhani mtazamo huu
ndio unaochochea jambo hili kuwa kubwa kila siku na kuwapa mtazamo wananchi
kuwa kuna ajenda ya siri katika hili.
Naomba kuchukua nafasi hii
kueleza kuwa WANANCHI WA MKOA WA MTWARA HAWAPINGI WANANCHI WA MIKOA MINGINE
KUNUFAIKA NA FAIDA ZA GESI BALI KINACHOPINGWA NI KUSAFIRISHA GESI GAFI TOFAUTI
NA AHADI YA SERIKALI YA KUJENGA MTAMBO WA KUZALISHA UMEME MKOANI MTWARA UTAKAOVUTIA
WAWEKEZAJI WA VIWANDA.UMEME HUU UNAWEZA KUSAFIRISHWA KWENDA MAHALI POPOTE
TANZANIA/NJE YA NCHI BAADA YA MTAMBO KUJENGWA MTWARA.
Baadhi ya waandishi wa habari kutoka Mtwara Press Club, wakimsikiliza bw.Joel Nannauka. |
Naomba kukumbusha kuwa madai
haya hayajotoka hewani,bali yametokana na sababu kadhaa:
1. Ni ahadi
za mara kwa mara zilizokuwa zilizotolewa na Mh.Rais na mawaziri wa Nishati na
Madini katika nyakati tofauti.Tangu mara ya kwanza Mh.Rais alipohojiwa clouds(kipindi
cha power breakfast) tarehe 29 october katika
kampeni ya mwaka 2010,pia alipokuja kwenye kampeni Mtwara na hata
alipokuja kushukuru baada ya kuwa Rais aliendelea kuahidi kuufanya Mtwara kuwa
mji wa viwanda kwa kuupatia umeme wa uhakika kupitia ugunduzi wa gesi hii,pia
alieleza katika kipindi hicho cha radio kusudio la serikali yake kujenga mtambo
wa 300MW.
Hii yote ilitengeneza matumaini makubwa kwa wananchi wa Mtwara wa
kufaidika na gesi hii.Leo tunaposikia gesi ghafi inahamishwa na bado hakuna mtambo
huo wala kiwanda sawa na ahadi zilivyotolewa,kuna kosa gani wananchi wakihoji?
2. Mpango
wa Mtwara power project uliolenga kuufanya mradi huu kuwa sehemu ya National
power Development plan(3920MW) ukilenga kuwa na mtambo wa kuzalisha 300MW
Mtwara zitakazoingizwa katika gridi ya Taifa na kuondoa tatizo la umeme nchini
uliokuwa umelenga kukamilika mwaka 2012.Ingawa ni wazi kuwa kampuni iliyokuwa
itekeleze mradi huu Artumas ilishindwa kutokana na mtikisiko wa kiuchumi wa
mwaka 2008,iliweka bayana kuwa ingepata dola za kimarekani milioni 7 ingeweza
kuutekeleza.
Kwa nini serikali haikuweka kama sharti mojawapo kwa kampuni ya
Wentworthy resource Limited iliyoinunua artumas kuutekeleza mradi huu uliokuwa
umekubalika kuingia katika mpango wa kitaifa?kwa nini uliachwa?Hili nalo hatuna
majibu kama ilivyo kwa mipango mingine kama vile Mtwara Corridor.
3. Ikumbukwe
kuwa kisiwa cha songosongo ndio eneo la kwanza kugunduliwa kwa gesi asilia
mwaka 1974 na kampuni ya AGIP kukiwa na takriban cubic feet 783 billion.
Kati ya
mipango mingi iliyowekwa kwa wakati huo kuhusiana na kubadilisha maisha ya
wanasongosongo na kilwa kwa ujumla ni kujenga kiwanda cha mbolea KILWA AMMONIUM
COMPANY,kilicholenga kutatua tatizo la ajira na kutosheleza uzalishaji wa
mbolea nchini.
Waliambiwa wasiwe na hofu gesi kwenda Dar es Salaam kwani viwanda
vitajengwa kilwa,Ingawa eneo lilitengwa kwa ujenzi wa kiwanda hicho na
wataalamu kusomeshwa,hadi hivi leo kiwanda hakijajengwa. Hivi hali kama hii
haitoshi kuleta wasiwasi kwa wananchi?kuna tatizo gani wakihoji jambo
hili?Waswahili husema ukiona mwenzako ananyolewa,wewe tia maji.
Kama
viwanda hivi vitafanikiwa vitaleta tija na ulazima wa kuifufua bandari ya
Mtwara ambayo tangu mwaka 2006/2007 imekuwa ikitumika kwa 31% ya uwezo wake(Tani
122,862 kwa mwaka badala ya tani 400,000 kwa mwaka).Mbinu hii itasaidia
kupunguza msongamano wa bandari ya Dar kama ambavyo nchi Jirani ya Kenya
wamefanya kwa kuipanua bandari ya Lamu ili kupunguza msongamano bandari ya
mombasa.
4. Hoja
nyingine ni ya kihistoria,Tangu tupate uhuru watu wa kusini wamesota katika
janga la kukosa nishati ya umeme kwa
muda mrefu na hawakuunganishwa na gridi ya taifa kwa sababu lukuki ingawa
iliwezekana kuvusha umeme baharini kwenda Zanzibar ilishindikana kuuleta
Mtwara.Kama wameweza kusahauliwa kwa miaka 51 katika swala la nishati,hofu ni
kuwa gesi itakapoisha vizazi vyao vitasahauliwa tena kwa kubaki na bomba
tupu,na hakuna atakayekumbuka tena kuunganisha mikoa hii na Gridi ya Taifa ili
kuwa na umeme wa uhakika ambao ndio hitaji kubwa mojawapo la wawekezaji.Hoja ya
gesi kuwa nyingi sana na itachukua muda mrefu kuisha haina mashiko kwani hata dhahabu tuiyokuwa
tunajivunia kuwa ni nyingi sana katika mgodi wa Nzega uliokuwa unachimbwa na
kampuni ya Resolute umefungwa mwaka jana august,dhahabu imeisha,hivyo hata gesi
itaisha tu,tufanye maamuzi ya busara.
5. Ilani ya
chama cha mapinduzi(2010) katika ibara ya 63(h) na (k) ilianisha miradi ya kinyerezi(240MW)
na mradi wa Mnazi bay(300MW) kama miradi miwili tofauti inayojitegemea.Hivyo
tunashangaa leo inapoonekana kuwa ni mradi mmoja.Tunataka kila mmoja uendelee
kama ulivyopangwa na si vinginevyo.Hii ndiyo itawezesha ahadi ya ujenzi wa
kiwanda cha UREA kilichopangwa kujengwa Mtwara kama inavyoainishwa katika Ibara
ya 49(e) kufanikiwa.Lakini hii pia itawezesha uhakika wa uanzishwaji wa kiwanda
cha kubangulia korosho kama makubaliano(Memorandam of understanding)
yaliyoingiwa kati ya TIB(80% Tanzania Investiment bank) na Tandahimba Newala
Cooperative union(20%TANECU) kukamilika.Nadhani Kuyatekeleza tuliyoahid ndio
njia bora ya kutimiza ahadi na kuboresha maisha ya watanzania.
6. Kwa kuwa
kipaumbele cha watu wa Mtwara si kuwa na umeme majumbani ambao ni ongezeko la
gharama la maisha kiuchumi(na kwa kuzingatia kuwa nyumba nyingi za mji wa
Mtwara hazina sifa ya kuunganishiwa umeme kwani ni za nyasi,udongo na makuti na
kipato chao cha sasa kinawanyima uwezo wa kuipa bili za kila mwezi)Kipaumbele
kinabaki ni kupunguza makali ya maisha kwa kuwa na uhakika wa kipato kwa njia
ya ajira kwa shughuli za uzalishaji viwandani na shughuli zitakazoambatana na
hizo,Ni vema serikali ikazingatia kauli ya
Mkurugenzi mkuu wa Wentworthy
resource Limited Inayochimba gesi ya Mnazi Bay Bwana Bob Mcbean iliyoripotiwa
tarehe 6 December London mwaka 2012 kuwa watapata faida kubwa
kwa kuwekeza katika kiwanda cha mbolea na kemikali nyingine,hivyo ni vyema
mkazo ukawa katika kuhimiza uwekezaji
zaidi kupitia gesi hii na uhakika wa nishati ya umeme kutokana na mtambo wa
kufua umeme utakaojengwa Mtwara.
TUJIFUNZE
KWA WENZETU.
Tanzania
si nchi ya kwanza kuchimba gesi katika dunia wala Afrika.Katika bara la afrika
tunazo nchi kama Algeria,Misri na Nigeria ambazo husafirisha gesi nje ya nchi.Tukiwa
nchi ya 66 duniani tukizalisha 658,000,000cubic metres,jirani zetu msumbiji ni
wa 50 wakizalisha 3,600,000,000cubic metres(takwimu za mwaka 2012).
Tanzania
kwa sasa inasadikika kuwa na kiasi cha 43 Trillion Cubic feet (TCF)
ukilinganisha na kiasi cha 2.8Trillioni cubic Metres(98.896Trillion cubic feet)
za msumbiji ambazo ni zaidi ya mara mbili ya kiwango tulichonacho hivyo si
vibaya tukijifunza kwao.
Kwa
sababu ya mipango mizuri ya kiuchumi ya Msumbiji haikuwa lazima kujenga kila
kitu Maputo/beira ambayo ni miji ya biashara lakini mtambo wa kuzalisha gesi ya
107.5MW umejengwa na kampuni ya Aggreko katika mji wa pembeni wa Ressano Garcia
utakaopeleka umeme Maputo na miji
mingine ya Afrika kusini ambako katika miji hii umeme huu utasafirishwa na kutumika kwani ndio miji mikubwa ya
kibiashara kama ilivyo Dar Es Salaam .
Ingawa umbali wa Maputo na Ressano Garcia
ni 1/5 ya umbali wa Dar-Mtwara,tunaweza kujifunza kwao katika hili.
Akizindua mradi huo mwezi July 2012 Rais wa
msumbiji Mh.Armando Guebuza alieleza kuwa wanakusudia kujenga mitambo ya kuweka
gesi katika hali ya kimiminika ipatayo 10(liquefied
natural gas (LNG) plants) katika maeneo mbalimbali ya msumbiji.Hii yote ni
kutawanya uchumi na kutengeneza fursa mbalimbali kwa wananchi wa kawaida wa Msumbiji.Hili
nalo linaweza kufanyika Tanzania.
NINI
KIFANYIKE?
1. Kwa
sababu bomba hili halisafirishi chakula cha dharura kwamba likisitishwa watu
watakufa katika jiji la Dar Es Salaam,Serikali itangaze rasmi kusitishwa kwa
mradi huu wa ujenzi wa bomba mara moja kutokana na kilio cha wananchi na
izijibu hoja 9 za wananchi zilizotolewa katika maandamano ya tarehe 27 december
2012.
2. Mkuu wa
mkoa na waziri wa nishati na madini wawaombe radhi wananchi wa Mtwara kwa
maneno yao ya kuudhi kwa kuita maandamano yao kuwa ni ya kipuuzi,wahaini na
wasioelewa ili kuonyesha kuwa walikosea.
Wasipofanya hivyo ni kusema walikusudia
kuyasema hayo na kwa jinsi hiyo ni kuchochea mikutano na maandamano
yanayoendelea,hivyo kwa lolote litakotokea watastahili kuwajibishwa.
3. Uwekwe
mpango maalumu wa viongozi waandamizi wa serikali kuja mtwara na kukutana na
wananchi wa mtwara Haraka ndani ya siku 14 zijazo.Nia sio kuwaambia gesi lazima
itoke bali ni kuwasikiliza na kufanyia kazi hoja zao.
4. Wabunge
wa mkoa wa Mtwara na Lindi waache malumbano kati yao bali wajitokeze hadharani
na kueleza msimamao wao wa pamoja kuhusiana na jambo hili.
ANGALIZO
Swala la
gesi linalenga kuwafaidisha wananchi wote wa Tanzania kama vile sera ya
serikali inavyosema.
Wananchi wa Mtwara ni sehemu ya Taifa hili nao wanahaki ya
kuhoji na kutathmini utekelezwaji wa
yale waliyoahidiwa na viongozi wao.Kuwanyima fursa hiyo ni kuwatenga na
utajiri wa Taifa lao.
Ningependa
kurudia kwa kusema kuwa,wananchi wa Mtwara hawasemi wananchi wa maeneo mengine
ya Tanzania hawapaswi kufaidika na gesi inayozalishwa Mtwara,hoja yao ni kuhusu
faida zilizozungumzwa na viongozi hapo kabla kuhusiana na viwanda na umeme.Hili
ndilo linalotakiwa kufanyiwa kazi kwa sasa.
Ingawa ni kweli kwamba sio serikali
inayojenga viwanda hivi lakini ndiyo yenye dhamana ya kufanya hivyo kama
ilivyoahidi.
Ikumbukwe
kuwa kufanikiwa kwa ujenzi wa mtambo wa kufua umeme Mtwara utatoa mwongozo wa
utekelezaji wa miradi kama hii katika maeneo mengine ya Nchi yetu ambako gesi
inaendelea kugundulika.
Mungu
Ibariki Tanzania,
Mungu
Ibariki Mtwara,
Mungu
Ibariki Gesi Asilia isaidie kuinua maisha ya watanzania Maskini,
Ahsanteni
Sana.
JOEL
NANAUKA
0713-243
244
MDAU WA
MAENDELEO.
No comments:
Post a Comment