Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga amesema hatagombea tena wadhifa huo katika uchaguzi uliopangwa kufanyika Februari 24 mwaka huu.
Akizungumza na Waandishi wa Habari kwenye ofisi za TFF leo, Rais Tenga amesema wakati anaingia kwenye uongozi mwaka 2004 ajenda ilikuwa na kuijenga TFF kama taasisi kwa kuweka mifumo ya uendeshaji ikiwemo kutengeneza katiba na kanuni, jambo ambalo limefanyika.
“Wajumbe wamekuwa wakiniuliza Rais vipi? Mimi hapana. Nilishafika pale pa kufika. Tulipoanza wakati ule ilikuwa ni kujenga taasisi. Na kazi hiyo tumeifanya. Tulipoingia mwaka 2004 hiyo ndiyo ilikuwa ajenda,” amesema Rais Tenga.
Amesema walitengeneza Katiba, vyombo huru vya kufanya uamuzi, kuongeza wigo wa wapiga kura ambapo hivi sasa kwenye mpira wa miguu hakuwezi kutokea migogoro, hata ikitokea kuna mfumo wa kuidhibiti.
Rais Tenga ameishukuru Sekretarieti ya TFF, Kamati ya Uchaguzi ya TFF, kamati za uchaguzi za wanachama wa TFF na vyama wanachama wa TFF kwa hatua iliyofikiwa katika uchaguzi ambapo mikoa yote imekamilisha uchaguzi na kubaki vyama shiriki pekee.
Ametoa mwito kwa wadau kujitokeza kugombea uongozi TFF, kwani baada ya kujenga taasisi ajenda iliyobaki ni mpira wa miguu wenyewe ikiwemo nini kifanyika ili mpira uchezwe katika maeneo mbalimbali.
“Tumeshatengeza mfumo, sasa ni kuangalia jinsi ya kuendeleza mpira. Changamoto ni tufanye nini ili mpira uendelee. Tunataka watu wengine wabebe hiyo ajenda ili tuangalie tunakwendaje mbele,” amesema.
Pia amesema ushirikiano ambao amepata kwa wapenzi na wadau wa mpira wa miguu ni wa ajabu. Vilevile ameishukuru vyombo vya habari, Serikali, klabu, wadhamini na wafadhili kwa mchango wao katika uendeshaji wa mpira wa miguu nchini.
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF),LEODEGAR TENGA |
Wadau 19 wamechukua fomu kuwania nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) unaotarajiwa kufanyika Februari 24 mwaka huu.
Fomu hizo zimeanza kutolewa leo (Januari 14 mwaka huu) ambapo wawili wamechukua nafasi ya Makamu wa Rais wakati waliobaki wanaomba ujumbe wa Kamati ya Utendaji wakiwakilisha kanda mbalimbali.
Waliochukua fomu za umakamu wa rais ni Wallace Karia na Ramadhan Nassib. Wote ni wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF inayomaliza muda wake.
Waliochukua fomu za ujumbe ni Shaffih Dauda, Athuman Kambi, Hussein Mwamba, Stewart Masima, Yusuph Kitumbo, Mugisha Galibona, Vedastus Lufano, Twahili Njoki, Charles Mugondo, Elley Mbise, Farid Nahdi, Ayubu Nyaulingo, Nazarius Kilungeja, Epaphra Swai, Khalid Abdallah, James Mhagama na Selemani Bandiho.
No comments:
Post a Comment