Sunday, April 21, 2013

dawa za kuongeza akili zaingia nchini.

akili 7a99a
John Haule akionesha moja ya dawa zenye virutubisho kutoka Afrika Kusini zilizoingia nchini.

Mtindo wa maisha, ulaji na msongo wa mawazo, vimewasababishia Watanzani wengi maradhi lukuki hata vifo.

Hata hivyo, wataalamu wa afya kutoka Afrika Kusini wamekuja na dawa maalumu, zilizo na uwezo wa kurudisha kumbukumbu, kuongeza upeo darasani, kuondoa sumu mwilini na kumfanya mzee kuonekana kijana.

Dawa hizo zinazotumia vitamini zilizomo kwenye vyakula vya kila siku, zina uwezo wa kuongeza kiwango cha uelewa kwa mwanafunzi au mfanyakazi.

Kiwango hicho cha uelewa kitaalamu unatambulika kama ‘IQ’.

Mratibu wa dawa hizo hapa nchini, John Haule anasema kuwa dawa hizo zina uwezo wa kufanya kazi kwa haraka.

“Virutubisho hivi ni vizuri kwa wale wanaokwenda katika mitihani au wanataka kufanya kazi inayohitaji umakini wa hali ya juu,” anasema Haule na kuongeza:

“Zimetengenezwa kwa vyakula tunavyotumia na siyo kemikali.”

Haule ambaye ni mtaalamu wa tiba asili na mimea anasema kwamba mtindo wa maisha na vyakula vinavyoliwa na watu mara kwa mara kwa sasa huufanya mwili kuhifadhi sumu nyingi mwilini.

Anasema kuwa dawa hizo pia zina uwezo kuondoa sumu mwilini na kuufanya mwili wa binadamu kurejesha rangi yake halisi na kumeng’enya vizuri chakula anachokula.

Haule anayefanya kazi pamoja na Shirika la Nativa linalotengeneza dawa hizo la nchini Afrika Kusini, anaeleza kuwa tangu kuingiza dawa hizo nchini watu wengi wamejitokeza kuzihitaji.

Ofisa Uhusiano wa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), Gaudensia Simwanza anasema kuwa mamlaka hiyo inazitambua dawa hizo kama virutubisho vya chakula, zimesajiliwa na ni salama kwa binadamu.

“Tuna taarifa kuwa bidhaa za ‘Go Woman’ na ‘Go Man’ zimesajiliwa na ni salama,” anasema.

Dawa nyingine zinazotengenezwa na kampuni hiyo zimetajwa kuwa na uwezo wa kuunda mifupa kwa watu wazima na majeraha ya wagonjwa wa kisukari.

“Ni vigumu kwa watu wazima wenye miaka 50 na kuendelea kupona haraka wanapopata ajali, lakini hizi dawa zinaponya majeraha na kuunga haraka mfupa,” anasema Haule.

Anasema kuwa kadri umri wa binadamu unavyoongezeka mwili wake unashindwa kuzalisha baadhi ya virutubisho vinavyoupa mwili uimara.

Dawa hizo zina mchanganyiko wa madini, vitamin, viondoa sumu pamoja na dawa za mitishamba.

Virutubisho vya chakula kwa kawaida hupungua ubora wake kwa sababu ya udongo, mionzi au kuweka vyakula hivyo katika majokofu.

Mambo mengine yanayofanya virutubisho vya chakula visifanye kazi yake sawasawa ni msongo wa mawazo na uchafu wa mazingira.

Ugonjwa wa kukosa raha na kusononeka kila wakati au sonona, pia unaweza kutibiwa kwa dawa hizo.

“Sonona inaua. Hata wataalamu wa afya wa nchi za Ulaya wamethibitisha, lakini dawa hii ina madini ya amino acidi ambayo hupatikana baada ya mtu kucheka,” anasema.

Anabainisha kwamba dawa hizo zina vitamin maalumu zinazoweza kuongeza kinga ya mwili na kuondoa sumu mwilini.

“Zina vitamin a, c na e, madini ya zinki na selenium na zina uwezo wa kuongeza nguvu ya mwili,” anasema.

Anadokeza kuwa kati ya dawa hizo, zipo pia dawa kwa ajili ya wanawake na wanaume pekee, zilizo na kazi maalumu.

Kwa mfano dawa ya wanawake ina uwezo wa kumsaidia mwanamke apate raha ya tendo la ndoa, inarutubisha nywele zake na kuzifanya zikue kwa haraka.

Vilevile, dawa hiyo inasaidia kuimarisha ngozi ya mwili kwa kuondoa sumu mwilini.

“Hii dawa kwa ajili ya wanawake ina Vitamini maalumu za kukuza nywele kama ‘Omega3 na Omega 6,’” anasema Haule.

Kwa upande wa wanaume, dawa hiyo itawasaidia kuongeza uwezo wa tendo la ndoa, kuimarisha mifupa pamoja na viungo.

Dawa zote mbili, yaani ile ya wanawake na ya wanaume zina uwezo wa kuimarisha ubongo na kumbukumbu.

Haule anaongeza kuwa ipo dawa kwa ajili ya wanawake wenye tatizo la kutokwa damu kwa wingi kunakosababishwa na hedhi au maradhi mengine.

Hata hivyo, Dk John Semkuya kutoka Hospitali ya Mwananyamala anasema kuwa ni vigumu mtu kupata tiba ya akili akiwa tayari ni mtu mzima, kwani uwezo wa kiakili unajengwa kuanzia utotoni.

“Lakini suala hili linahitaji utafiti zaidi kwa sababu kama hujafanya tafiti, huna haki ya kuzungumza,” anasema Dk Semkuya.

Anasema ikiwa virutubisho hivyo vya chakula vitatumiwa tangu utotoni basi vinakuwa na manufaa zaidi kuliko kutumiwa ukubwani.

Wagonjwa wa Ukimwi
Miongoni mwa dawa hizo ipo dawa ya ‘Life Gain’ mahususi kwa kufubaza makali ya Virusi vya Ukimwi.

Haule anasema kuwa kwa virutubisho vilivyo katika dawa hizo vina uwezo wa kupandisha kinga ya mwili kwa haraka, bila kumwathiri mgonjwa.

Mwananchi ilifanya mazungumzo na mwanamume mmoja mkazi wa Tandika (jina linahifadhiwa) anayeishi na VVU ambaye alitumia dawa ya Lifegain.

Mtu huyo alisema alikuwa hoi kwa maradhi, lakini baada ya kutumia dawa hiyo kwa muda wa wiki mbili, alinyanyuka na sasa anaendelea na shughuli zake za kawaida.

Haule anasema kampuni hiyo imefika baada ya kuona kuna upungufu mkubwa wa dawa zinazotumia virutubisho vya mimea huku watu wengi wakinywa dawa za kemikali.

“Dawa zenye kemikali zinasaidia, lakini zikitumika kwa muda mrefu huchosha ini, figo kwa sababu hutunza sumu,” anasema Haule.

Haule anasema amerithi elimu hiyo ya tiba mbadala kutoka kwa babu yake, Mzee Fungafunga.

Anasema alijifunza tiba kwa kutumia mimea, kutoka kwa babu yake, ambaye licha ya kuwa alikuwa mhunzi, alitibu kwa njia ya mimea.

Haule anasema aliamua kujikita zaidi katika tiba asilia baada kukosa ushirikiano katika fani aliyosomea ya ufundi makanika. Chanzo: www.mwananchi.co.tz


CHANZO/MjengwaBlogs.

No comments:

Post a Comment