Ugonjwa hatari unaoshambulia mahindi
na kusababisha saratani kwa binadamu umeingia nchini na wakulima sasa
wametahadharishwa kutokula mahindi hayo wala unga ambao haujakobolewa.
Mahindi yaliyoathiriwa na ugonjwa huo
huota 'fungus' ambao ina sumu inayoitwa 'Aflatoxin' ambayo inaweza
kusababisha madhara kwa wanyama na binadamu hususan ugonjwa wa saratani.
Mbali na kutikisa mikoa kadhaa na
kusababisha hasara kubwa kwa wakulima, ugonjwa huo ambao umeanzia nchini
Kenya unaendelea kusambaa kwa kasi na sasa umeingia pia nchini Uganda.
Awali ugonjwa huo uliripotiwa
kuzikumba wilaya za Babati mkoani Manyara na Meatu mkoani Shinyanga tu,
lakini sasa umesambaa hadi katika mikoa jirani ikiwamo Kilimanjaro
.
Mkuu wa Mkoa Kilimanjaro, Leonidas
Gama jana alilithibitishia gazeti hili kuwa mkoa wake umekumbwa na
ugonjwa huo na tayari umesambaa katika wilaya tatu; Moshi Vijijini, Siha
na Hai.
"Ni kweli baadhi ya wilaya zimekumbwa na ugonjwa huo, bahati
mbaya sana hauna tiba na unasambaa kwa kasi... Wataalamu wanaendelea
kuwaelimisha wakulima kutambua dalili zake," alisema Gama.
Gama alisema endapo mkulima atabaini
shamba lake kushambuliwa na ugonjwa huo katika hatua za awali,
anachotakiwa kufanya ni kung'oa mimea yote ya mahindi na kuichoma moto.
Mkuu wa Wilaya ya Hai, Novatus Makunga
alisema takriban hekari 14 zimeshambuliwa na ugonjwa huo katika shamba
la Watawa wa Kanisa Katoliki Mailisita na shamba la mkulima wa Lambo.
Alisema tayari wataalamu kutoka
Taasisi ya Utafiti wa Kilimo ya Selian (SARI) ya Jijini Arusha wamefika
wilayani humo na kutoa tahadhari kwa wakulima juu ya athari za ugonjwa
huo.
Mfanyabiashara mashuhuri wa mjini Moshi, John Bennett anayemiliki
mgahawa wa Golden Shower aliitaka Serikali kutoa elimu kwa wananchi na
wafanyabiashara na kuchukua tahadhari.
"Utajuaje unga wa dona haukutokana na
hayo mahindi au pumba ya chakula cha mifugo hayakutokana na hayo? Hili
jambo ni zito sana si la kufanyia utani hata kidogo"alisema Bennett.
Mkulima wa Kijiji cha Kikavu Chini
wilayani Hai, Justine Mvungi alisema wataalamu kutoka SARI wamewataka
kuchoma moto miche ya mahindi ambayo watagundua imeshambuliwa.
"Wametuambia takriban shamba
likishambuliwa, tung'oe mahindi hayo na kuyachoma moto, wametuambia kama
tulishavuna basi tukoboe mahindi hayo maana kiini chake kina
madhara,"alisema.
"Aliongeza kusema" hata tukikoboa
mahindi tumeambiwa zile pumba zake tusiipe mifugo kwa sababu
itaathirika... Ugonjwa huu wa mmea wa mahindi umeleta taharuki kubwa kwa
wakulima na wananchi."CHANZO MWANANCHI
CHANZO/MjengwaBlogs.
No comments:
Post a Comment