Wednesday, April 3, 2013

RAGE AMPA MKONO WA 'KWAHERI' KABURU, AAMUA KWENDA KUMPIGIA MAGOTI HANS POPPE ARUDI VITANI.



 
KIKAO cha Kamati ya Utendaji ya klabu ya Simba kilichofanyika jana mjini Dar es Salaam, kimeridhia kujiuzulu kwa aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’, imeelezwa. Hata hivyo, Kikao hicho kilichofanyika Dar es Salaam chini ya Mwenyekiti wa klabu hiyo, Alhaj Ismail Aden Rage kimekataa katakata kujiuzulu kwa aliyekuwa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili, Zacharia Hans Poppe.  
Akizungumza na Waandishi wa Habari mchana wa leo makao makuu ya klabu, Mtaa wa Msimbazi, Dar es Salaam, Ofisa Habari wa S.S.C., Ezekiel Kamwaga ‘Mr. Liverpool’ amesema kwamba kikao hicho pia kimemteua Mwenyekiti, Rage kuongoza kampeni za kwenda kumbembeleza Hans Poppe abatilishe uamuzi wake wa kujiuzulu na kuendelea kusukuma mbele gurudumu la maendeleo la Simba SC.   
“Na kama utakumbuka, hata Mwenyekiti wetu, Rage alijiuzulu Ujumbe wa 
Kamati ya Nidhamu ya TFF (Shirikisho la Soka Tanzania), lakini Kamati ya Utendaji ya TFF, chini ya rais wake, Leodegar Tenga ikamkatalia, hivyo si ajabu kwa Hans Poppe kukataliwa kujiuzulu,”alisema Kamwaga.  
“Na pia uamuzi huu wa Kamati ya Utendaji, umeendana na uamuzi wa 
 
Mkutano wa Matawi uliofanyika mwezi uliopita Dar es Salaam, ambao ulikubali kujiuzulu kwa Kaburu, ukakataa kwa Hans Poppe,”alisema Kamwaga.   
Mwandishi huyo wa safu ya “BET na Kamwaga” katika gazeti la michezo linaloongoza Tanzania, Mwanaspoti, amesema kikao cha jana pia kiliamua Mkutano Mkuu wa klabu hiyo ufanyike Julai mwaka huu.  
“Kamati imeamua Mkutano Mkuu ufanyike Julai na utatangazwa siku 30 kabla, hiyo ni kwa mujibu wa Katiba ya Simba, ambayo inaelekeza Mkutano Mkuu ufanyike mara moja kwa mwaka, hivyo Kamati imeona hakuna sababu ya kuitisha Mkutano wa dharula kwa sasa,”alisema.  
Hamkani si shwari ndani ya Simba SC kwa sasa kutokana na kufanya vibaya kwa timu katika mashindano mbalimbali na baadhi ya wanachama kushinikiza uongozi ujiuzulu.  
Mwezi uliopita Kaburu na Hans Poppe walijiuzulu, wakati huo Rage alikuwa India kwa matibabu ya mgongo.  
Akiwa India, baadhi ya wanachama walikutana katika ukumbi wa Star Light Cinema, Dar es Salaam na kufikia uamuzi wa kuung’oa uongozi mzima na kuunda Kamati ya Muda chini ya Hans Poppe.  
Hata hivyo, Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji ya TFF chini ya Mwenyekiti wake, Wakili Alex Mgongolwa ilisema mapinduzi hayo ni batili na uongozi wa Rage bado halali.     
Hans Poppe, Kapteni wa zamani wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) amekuwa mwanachama wa Simba anayekubalika na wengi, kwani katika mgogoro huu pande zote zinampendekeza.  
Mwezi uliopita, Simba SC ilitolewa katika Raundi ya Kwanza tu ya Ligi ya 
 
Mabingwa Afrika kwa kufungwa jumla ya mabao 5-0 na Recreativo de Libolo ya Angola, ikifungwa 1-0 nyumbani Dar es Salaam na baadaye 4-0 ugenini.  
Aidha, kwa sasa Simba SC ambao ndio mabingwa watetezi wa Ligi Kuu, wameporomoka hadi nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi, wakiwa wana pointi 35, nyuma ya Kagera Sugar yenye pointi 37, Azam FC 43 na Yanga SC iliyo kileleni kwa pointi zake 49.  
Klabu pia inakabiliwa na madeni mengi kiasi cha kufikia kudhalilishwa kwa wachezaji na wadai hao. Mfano mwezi uliopita wachezaji wa Simba walizuiwa kutoka hotelini kwenda kumenyana na Coastal Union ya Tanga katika Ligi Kuu hadi uongozi ulipe deni la Sh. Milioni 28 la hoteli ya Sapphire Court, Kariakoo.  
Lakini baada ya uongozi kubembeleza na kuahidi kwa maandishi kulipa deni hilo, waliruhusiwa kuondoka, ingawa walichelewa kufika uwanjani na kujikuta wanashuka dimbani bila hata kupasha misuli moto.  
Katika mwezi huo huo, gari mbili za klabu zilikamatwa na wamiliki wa hoteli ya Spice, Kariakoo pia kwa sababu ya deni la Sh. Milioni 27 na wakati huo huo, inadaiwa kuna kigogo anaidai Simba SC zaidi ya Sh. Milioni 200 alizokuwa anaikopesha kwa matumizi tofauti.     
Simba SC inategemea fedha za mauzo ya mshambuliaji wake Mganda, Emannuel Okwi kwenda Etoile du Sahel ya Tunisia dola za Kimarekani 300,000 zaidi ya Sh. Milioni 470,000 za Tanzania izitumie kulipa madeni hayo.  
Na pia mustakabli wa malipo hayo haueleweki hadi sasa ikiwa ni miezi miwili tangu biashara hiyo ifanyike, kiasi cha kuibua hofu nyingine, labda Simba SC ‘imepigwa changa la macho’.
 
 
Chanzo/BinZubeiryBlogs.

No comments:

Post a Comment