Waziri mkuu wa zamani wa Uingereza, Margaret Thatcher, maarufu kama
"Iron Lady" kutokana na ujasiri na ukakamavu wake katika medani za
uongozi, amefariki dunia baada ya kuugua ugonjwa wa kiharusi akiwa na
miaka 87.
Malkia Elizabeth wa Pili wa Uingereza na Waziri Mkuu
David Cameron wameongoza katika salamu za rambi rambi kwa waziri mkuu
huyo wa kwanza mwanamke nchini Uingereza, muumini mashuhuri kabisa wa
sera za mrengo wa kulia na mtu muhimu wakati wa Vita Baridi.
Msemaji wa familia ya Thatcher amekaririwa akisema "kwa
masikitiko makubwa Mark na Carol Thatcher (watoto wa marehemu)
wanatangaza kwamba mama yao Bi. Thatcher amefariki kwa utulivu baada ya
kupigwa na kiharusi leo asubuhi."
Waziri Mkuu huyo wa zamani ambaye aliiongoza Uingereza
kuanzia mwaka 1979 hadi mwaka 1990 alikuwa akikabiliwa na maradhi ya
kupoteza kumbukumbu na mara chache amekuwa akionekana hadharani katika
miaka ya hivi karibuni.
Thatcher alikatazwa kuhutubia hadharani
Mara ya mwisho alilazwa hospitalini hapo
mwezi wa Disemba mwaka jana kwa ajili ya operesheni ndogo ya kuondowa
uvimbe kwenye nyonga yake.Kiongozi huyo wa zamani wa chama cha
Conservative amebakia kuwa waziri mkuu pekee mwanamke katika historia ya
Uingereza na kiongozi aliekaa mfululizo kwa muda mrefu kabisa katika
makaazi ya waziri mkuu ya Downing Street katika karne ya 20.
Binti yake wakati fulani aliwahi kusema kwamba waziri
mkuu huyo wa zamani inabidi akumbushwe mara kwa mara kwamba mume wake
Denis amefariki mwaka 2003.Thatcher alitakiwa na madaktari kuacha
kuhutubia hadharani muongo mmoja uliopita baada ya kukumbwa na kiharusi
mara kadhaa.
Kasri la Kifalme la Uingereza Buckingham Palace limetowa
taarifa ikisema kwamba Malkia amesikitishwa kusikia habari za kifo cha
Thatcher na kwamba atatuma ujumbe binafsi wa masikitiko kwa
familia.Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron amekatisha ziara yake
katika nchi kadhaa za Ulaya na amesema kwamba kwa huzuni kubwa amepokea
habari za kifo cha Bibie huyo na kwamba wamempoteza kiongozi
adhimu,waziri mkuu adhimu na Muingereza adhimu.
Thatcher aiokowa Uingereza
Waziri Mkuu wa zamani Margaret Thatcher akiwa pamoja na Waziri Mkuu wa sasa David Cameron hapo mwaka 2010.
Ameongeza kusema kwamba Thatcher
"ameitumikia nchi yake vizuri sana, ameiokoa nchi yake na ameonyesha
ushujaa mkubwa sana katika kufanya hivyo.Watu watakuwa wanajifunza juu
ya kile alichokifanya na mafanikio yake kwa miongo kadhaa inayokuja na
yumkini hata kwa karne kadhaa.Hiyo dio haiba yake."
Michael Howard kiongozi wa chama cha Conservative kuanzia
mwaka 2003 hadi mwaka 2005 amekiambia kituo cha televisheni cha Sky
kwamba ni habari za kuhuzunisha sana kwani alikuwa ni mashuhuri sana
katika siasa za Uingereza.Howard anaamini kwamba Thatcher ameiokoa nchi
yao, ameubadili uchumi wa nchi hiyo na anaamini kwamba ataingia katika
historia akiwa kama mmojwapo wa mawaziri wao wakuu walio adhimu kabisa.
Wafuasi wa sera za mrengo wa kulia wanampongeza mama huyo
kwa kuitowa Uingereza kwenye msononeko wa kiuchumi lakini wafuasi wa
mrengo wa shoto wanamshutumu kwa kuving'owa viwanda vilivyokuwepo tokea
enzi za jadi na kuvunja kiini cha mshikamano wa jamii.
Alielewana vyema na Reagan
Waziri Mkuu Margaret Thatcher akifurahia jambo na Rais Ronald Reagan wa Marekani katika Mkutano wa Kilele wa Ottawa mwaka 1981
Katika jukwaa la kimataifa alijenga
uhusiano maalum na Rais Ronald Reagan wa Marekani jambo ambalo
limesaidia kuuangusha ukomunisti katika Muungano wa
Kisovieti.Alimwelezea aliekuwa kiongozi wa Muungano wa Kisovieti wakati
huo Mikhail Gorbachov kuwa ni mtu anayeweza kushirikiana naye.Pia
alikuwa akipinga vikali uhusiano wa karibu wa Ulaya.
Thatcher alizaliwa akiwa anajulikana kwa jina la Margaret
Hilda Roberts hapo tarehe 13 Oktoba mwaka 1925 katika mji wa soko wa
Grantham mashariki ya Uingereza akiwa ni binti wa muuza duka la vyakula
na bidhaa ndogo ndogo.Baada ya kumaliza shule na kujipatia shahada yake
ya Kemia katika Chuo Kikuu cha Oxford alifunga ndoa na mfanyabiashara
Denis hapo mwaka 1951 na miaka miwili baade walibarikiwa watoto mapacha
Carol na Mark.
Mara ya kwanza alichaguliwa katika bunge hapo mwaka 1959
na alichukuwa nafasi ya waziri mkuu wa zamani Edward Heath kama kiongozi
wa chama cha upinzani cha Conservative hapo mwaka 1975 kabla ya kuwa
waziri mkuu miaka minne baadae.
Haiba aliyoiwacha
Haiba yake ya kudumu inaweza kuelezwa kwa
muhtasari kuwa ya "Thatcherism " yaani mkusanyiko wa sera ambapo
wafuasi wake wanasema zimeendeleza uhuru wa mtu binafsi na
kusambaratisha mgawanyiko wa kitabaka ambao ulikuwa umeipasuwa Uingereza
kwa karne kadhaa.Hata hivyo kushinikiza sera zake kuliiweka serikali
yake katika mapambano kadhaa magumu ndani na nje ya nchi.
Alipambana na migomo ya mara kwa mara ya vyama vya
wafanyakazi ambapo alifanikiwa kuzima nguvu za vyama hivyo na kuondowa
ruzuku kwa makampuni kadhaa yaliokuwa yakiendeshwa kwa
hasara.Itakumbukwa wakati Argentina ilipovivamia visiwa vya Falklands
vilivyoko chini ya himaya ya Uingereza hapo mwaka 1982, Thatcher alituma
vikosi na meli za kivita na kuvikombowa katika kipindi cha miezi
miwili.
Mwandishi: Mohamed Dahman/AFP
Mhariri: Mohammed Khelef
No comments:
Post a Comment