MWANAFUNZI
wa kidato cha pili Shule ya Sekondari Komnyang’anyo, Mwenjuma Magalu
(16) amejikuta akibeba mzigo wa kulea familia baada ya familia hiyo
kutelekezwa na babayake.
*Imeandaliwa na www.thehabari.com kwa kushirikiana na TAMWA
Mwanafunzi
huyo anayeishi katika Kijini cha Msasa amejikuta katika hali hiyo ngumu
baada ya mama yake mzazi, Hadija Magalu kufariki dunia ambaye ndiye
aliyekuwa akiihudumia familia hiyo baada ya mzazi mwenzake (mumewe)
kuitelekeza miaka minne iliyopita.
Mama huyo (Hadija Magalu) alifariki
dunia Agosti, 2013 kwa matatizo ya uzazi na kuiacha familia hiyo ya
watoto watatu aliyokuwa akiihudumia chini ya ulezi wa mamayake mzazi,
Bibi Amina Mohamed.
Akizungumza na
mwandishi wa habari hizi hivi karibuni kijijini Msasa, mwanafunzi
Magalu alisema amelazimika kuilea familia hiyo baada ya bibi yake
aliyeachiwa familia hiyo kuugua ugonjwa wa TB na kushindwa kuendesha
shughuli za kilimo na nyinginezo kuisaidia familia hiyo.
“Bibi
ndiye aliyekuwa akitupikia, tutafutia chakula na tulikuwa
tukishirikiana naye hata kulima…lakini kazi hizo zote kutokana na afya
yake hawezi kuzifanya, ninalazimika kuzifanya mwenyewe.
Japokuwa nipo
shuleni lakini natakiwa kujua tutakula nini tunapata wapi pesa ya
chakula na shughuli nyingine za familia,” alisema Magalu akizungumza na
mwandishi wa habari hizi.
Alisema
familia yao hutegemea kilimo lakini wakati mwingine hulazimika kwenda
kutafuta vibarua vya kufanya ili kupata pesa ya kula yeye pamoja na bibi
yake. Aidha aliongeza kuwa wadogo zake wawili ambao awali alikuwa
akikaa nao amelazimika kuwapeleka kwa mjomba wake baada ya kuona hali ni
ngumu.
Hata hivyo alisema wajomba zake nao hali yao ni ngumu hivyo
wanashindwa kuhudumia familia hiyo.
Akizungumzia
hali ya maisha ya familia hiyo Bibi. Amina Mohamed ambaye kwa sasa ni
mgonjwa wa TB alikiri mwanafunzi huyo kuwa na majukumu mazito ya familia
ambayo awali alikuwa ameyabeba yeye baada ya mwanaye kufariki dunia.
“Kweli
mtoto huyu anaelemewa na malezi ya familia hii lakini sina cha kufanya
kwa kuwa mimi ni mgonjwa wa TB na nimeshauriwa nisifanye kazi kwa sasa,
hivyo kuanzia kupika, kulima shambani na hata kutafuta cha kula anafanya
yeye baada ya kurudi shuleni,” alisema bibi huyo.
Mwanafunzi
huyo ambaye anasomeshwa na msamaria mmoja aliyejitokeza baada ya
familia yao kushindwa kumlipia ada amewaomba watu walioguswa na maisha
ya familia hiyo kumsaidia.
Akizungumza
hivi karibuni Kaimu Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Komnyang’anyo,
Nadhiru Kinyama alikiri hali ngumu kwa kijana huyo kutokana na mazingira
ya familia yao na kuongeza anahitaji kusaidiwa hata fedha za kujikimu
na gharama zingine za masomo.
Chanzo/MjengwaBlogs
No comments:
Post a Comment