Mpatanishi; Zacharia Hans Poppe amerudisha amani Simba SC |
Na Mahmoud Zubeiry
SASA ni shwari Simba SC. Hivyo ndivyo unavyoweza kusema, kufuatia pande mbili zilizokuwa zinavutana, uongozi chini ya Mwenyekiti Alhaj Ismail Aden Rage na wapinzani wake kumaliza tofauti zao.
Pongezi
kubwa ziende kwake, Kapteni wa zamani wa Jeshi la Wananchi Tanzania
(JWTZ), Zacharia Hans Poppe aliyefanikisha kumaliza mgogoro wa chini kwa
chini baina ya Rage na wapinzani wake.
Akizungumza
na BIN ZUBEIRY jioni hii, mpatanishi huyo wa mgogoro uliorejesha amani
na umoja Simba SC, amesema; “Tofauti zilizokuwapo tumekwishazimaliza na
sasa Simba SC ni shwari, tunaanza upya kazi,”alisema.
Poppe
aliyepigana vita dhidi ya Nduli Iddi Amin Dada kuokoa ardhi ya Tanzania
na Watanzania waliokuwa wakinyanyswa na askari na rais huyo wa zamani
wa Uganda, aliongeza; “Na kwa maana hiyo, natamka rasmi, nami nimerejea
ndani ya Simba SC kwa nafasi zangu zote kama nilivyoombwa baada ya
kujiuzulu,”alisema.
Poppe
alikuwa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji na Mwenyekiti wa Kamati ya
Usajili- wakati huo huo Mwenyekiti wa Friends Of Simba na aliamua kukaa
kando kabisa wakati mgogoro kutofungana na upande wowote, akishughulikia
amani ya klabu.
Poppe
alisema kwa sasa wanalekeza nguvu zao katika kumalizia Ligi Kuu ya
Vodacom Tanzania Bara kwa heshima na baada ya hapo watatengeneza timu
mpya itakayoiteka soka ya nchi hii msimu ujao.
“Tumevuna
matunda ya ugomvi na migogoro katika klabu, tulianza msimu vizuri na
tukawa juu kwa muda mrefu, lakini baada ya hapo naona tukalewa mafanikio
tukaanza kugombana bila sababu,”.
“Matokeo
yake ndiyo haya, tumepoteza mwelekeo, lakini madhali tumemaliza tofauti
baina yetu, na tumefikia makubaliano ya msingi ya kudumisha umoja na
amani ndani ya klabu, ambavyo ndivyo chimbuko la mafanikio, hakuna shaka
wana Simba watafurahi tena,”alisema Hans Poppe.
Mambo
yalitibuka Simba SC miezi kadhaa iliyopita kufuatia mgogoro wa chini
kwa chini baina ya Rage na wapinzani wake, uliosababisha mgawanyiko hadi
ndani ya uongozi.
Makamu
Mwenyekiti, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ alijiuzulu sambamba na Hans Poppe
na tangu hapo, Simba imekuwa ikienda kama jahazi liso na Nahodha na
matokeo yake ni kutaka kuzama kwa kupoteza mwelekeo.
Matokeo
yake, timu imepoteza ubingwa wa Ligi Kuu na kukosa hata nafasi ya pili,
ambayo ingewawezesha kucheza Kombe la Shirikisho Afrika mwakani.
Amani
inarejea Simba SC zikiwa zimebaki takriban wiki tatu kabla ya kumenyana
na wapinzani wa jadi, Yanga SC katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom
Tanzania Bara, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Yanga
SC walitaka sana kutumia mwanya wa mgogoro ndani ya Simba SC kulipa
kisasi cha kufungwa 5-0 mwaka jana, lakini sasa inaonekana shughuli
itakuwa pevu Mei 18 Uwanja wa Taifa.
CHANZO/BinZubeiryBlogs.
No comments:
Post a Comment