Viongozi kutoka mataifa kadhaa ya Afrika wamewasili jijini Nairobi
kuungana na Wakenya kwenye sherehe za kuapishwa kwa rais mpya wa Kenya,
Uhuru Kenyatta, kwenye uwanja wa mpira uliojaa maelfu ya wafuasi wake.
Kenyatta mwenye umri wa miaka 51 ni mtoto wa rais wa
kwanza wa Kenya, Jomo Kenyatta. Ushindi wake wa asilimia 50.07 katika
uchaguzi wa tarehe 4 Machi ulihalalishwa na Mahakama ya Juu baada ya
pingamizi lililowekwa na Waziri Mkuu anayemaliza muda wake, Raila
Odinga, kutupiliwa mbali na mahakama hiyo.
Kenyatta anayekuwa rais wa nne wa taifa hilo la Afrika ya
Mashariki tangu lilipopata uhuru wake kutoka Uingereza mwaka 1963,
anakuwa rais wa pili barani Afrika kuwa madarakani hali anakabiliwa na
mashitaka kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) kwa tuhuma za
kusaidia kuchochea ghasia za kikabila zilizoukumba uchaguzi wa urais wa
Kenya wa mwaka 2007.
Kesi hiyo imepangwa kusikilizwa mwezi Julai, ambapo
Kenyatta na naibu wake, William Ruto, wanakabiliwa na mashitaka ya aina
moja.
Hata hivyo, uchaguzi wa mara hii ulikuwa wa amani na kwa
mujibu wa shirika la habari la Reuters, Wakenya wengi wanatarajia kwamba
Uhuru atatimiza ahadi yake ya kuwa kiongozi wa watu wote na hatakuwa
rais wa kabila lake tu, jambo ambalo limekuwa kawaida kwa wanasiasa wa
huko.
Utata unaoyakumba mataifa ya Magharibi
Kwa mataifa ya Magharibi, ambao ni
wafadhili wakubwa wa nchi hiyo yenye uchumi mkubwa zaidi kwenye eneo la
la mashariki mwa Afrika, Kenya ni mshirika muhimu katika mapambano dhidi
ya makundi ya kidini yenye siasa kali kwenye eneo hilo.
Lakini sasa mataifa hayo yanakabiliwa na uchaguzi wa ama
kuendelea kuimarisha mahusiano au kujitenga na kiongozi ambaye
anakabiliwa na mashitaka kwenye mahakama ya ICC mjini The Hague.
Marekani na mataifa makubwa ya Ulaya yalisema yangelituma
mabalozi wao kwenye sherehe za kuapishwa kwa Kenyatta, kiwango cha
uwakilishi ambacho wanasema bado kinakwenda sambamba na msimamo wao wa
kuwa na mahusiano ya lazima tu na watuhumiwa hao.
Mtaalamu wa masuala ya Kenya katika Chuo Kikuu cha
Warwick, Daniel Branch, ameiambia Reuters kuwa mataifa ya Magharibi
yamejikuta kwenye hali ngumu sana, lakini huenda kila nchi ikatafuta
njia yake yenyewe na mahusiano na Kenya.
China huenda ikapata fursa mpya
Wakati kwenye sherehe hizo, viongozi wakuu wa Afrika watajikuta wamewekwa pamoja na mabalozi tu wa nchi za Magharibi, Kenya na India - ambazo zote mbili hazijasaini Mkataba wa Rome ulioanzisha ICC - zimetuma maafisa wao wa ngazi za juu.
Hata hivyo, mabalozi wa Kimagharibi wataepuka matusi mengine, baada ya maafisa wa Kenya kusema kuwa Rais Omar Hassan al-Bashir wa Sudan asingelihudhuria sherehe hiyo.
Chanzo/DW SWAHILI.
No comments:
Post a Comment