Wiki hii magazeti ya Ujerumani yameandika juu ya Baba Mtakatifu mstaafu
Benedikt wa 16 na juu ya mwendesha mashtaka mkuu wa Mahakama
inayopambana na uhalifu ya mjini The Hague,ICC. Pia yameandika juu ya
Kongo
Gazeti la"Süddeutsche"limeandika juu ya msimamo wa Baba Mtakatifu mstaafu Benedikt wa 16 juu ya Afrika. Katika makala yake gazeti hilo linasema kwamba alipokuwa kiongozi wa Kanisa Katoliki, Benedikt wa16 aliyataja matatizo ya barani Afrika lakini hakuwa na masuluhisho.
Gazeti hilo linaeleza kwamba Benedikt wa16 alikuwa kiongozi wa Kanisa Katoliki kwa muda wa miaka minane.Aliyataja matatizo ya Afrika lakini jee aliweza kuondokana na mtazamo wa kiulaya juu ya Afrika.?
Ziara ya barani Afrika:
Nyota ilimsimamia vibaya Benedikt wa16 alipofanya ziara barani Afrika mnamo mwaka wa 2009.Waandishi wa habari waliripoti kwa mapana na marefu juu ya msimamo wake wa kupinga matumizi ya kondomu na msimamo wake wa kutetea kupiga marufuku kutoa ujauzito.
Gazeti la "Süddeutsche"limeandika katika makala yake kuwa jawabu la Benedikt wa 16 lilikuwa kutoa mwito wa kuliimarisha kanisa barani Afrika.
Aliwataka wa Wakatoliki wa Afrika wasimame wima na waitetee Injili na wafanye juhudi za kuleta mdahalo baina ya dini, tamaduni na jamii zote.
"Mimi nawatumikia watu wanaodhulumiwa barani Afrika".
Mwendesha Mashitaka Mkuu wa ICC Fatou Bensouda
Gazeti la "Der Tagesspiegel" limeikariri kauli hiyo ya Fatou Bensouda, Mwendesha mashtaka mkuu wa Mahakama Kuu ya mjini The Hague,ICC inayopambana na uhalifu.
Katika muktadha wa uchaguzi mkuu nchini Kenya,gazeti la "Der Tagesspiegel" linakumbusha aliyoyasema
Mwendesha mashtaka mkuu huyo alipofanya ziara nchini Ujerumani.
Fatou Bensouda alisema katika ziara hiyo kwamba amani bila ya haki haiwezi kuleta maridhiano ya dhati.
Gazeti la"Tagesspiegel"limemnukuu mwanasheria huyo akisema kuwa anawatumikia watu wanaodhulumiwa barani Afrika.
Gazeti hilo limetilia maanani kwamba Umoja wa Afrika unamuunga mkono Mwendesha mashtaka mkuu huyo wa Mahakama ya kimataifa, ICC licha ya malalamiko kwamba Mahakama hiyo inawaandama Waafrika tu.!
Mgogoro wa Mashariki mwa Kongo:
Waasi wa M23 Mashariki mwa Kongo
Gazeti la"Die Zeit" linauliza katika makala yake,jee Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo itakuwa na amani?
Gazeti hilo limeuliza swali hilo kuhusiana na mkataba wa amani uliotiwa saini mjini Addis Ababa Jumapili iliyopita na viongozi wa nchi za maziwa makuu.
Gazeti la"Die Welt" linaeleza kuwa hatua ya viongozi kutoka nchi 11 za maziwa makuu kutia saini mkataba wa kuleta amani katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, inapaswa kuzingatiwa kuwa tukio muhimu la kisiasa na kidiplomasia.
Gazeti la "Die Zeit" limemnukuu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon akisema kwamba kutiwa saini kwa mkataba huo ni mwanzo tu wa mchakato wa muda mrefu wa kuleta amani nchini Kongo.Lakini gazeti la"Die Welt" linauliuza katika makala yake,jee nani atauendeleza mchakato huo ?
Waasi wa Mali wakimbilia Sudan:
Gazeti la"die tageszeitung limearifu kwamba waasi waliotimuliwa nchini Mali wamekimbilia Sudan.Gazeti hilo limesema kwa mujibu wa wapinzani wa serikali nchini Sudan,wapiganaji wa kiislamu wenye itikadi kali kutoka Mali wamekimbilia katika jimbo la Darfur la magharibi mwa Sudan.Waasi hao walikimbia Mali baada ya majeshi ya Ufaransa kuingilia kati kijeshi ili kuuzima uasi nchini humo.
Kwa mujibu wa gazeti la"die tageszeitung" wapiganaji hao wa kiislamu watawaunga mkono wanamgambo wanaoshirikiana na serikali ya Sudan,katika mapambano ya kugombea malighafi.
Gazeti la"die tageszeitung" limesema kuwa habari juu ya waasi wa Mali kuijipenyeza ndani ya Darfur zimethibitishwa na mwakilishi maarufu wa chama cha "Haki na Usawa" bwana Tahir al- Faki alipozungumza na jarida la "Sudan Tribune"
No comments:
Post a Comment