Tuesday, March 5, 2013

waziri muhongo alipokutana na watanzania uingereza.

1. Kadamnasi ikimsikiliza Waziri© 2013 Urban Pulse Creative_96
Kadamnasi ikimsikiliza Waziri kwa makini, ukumbi wa Ubalozi wetu London.Wapo waliokuja kuuliza maswali. Au waliotaka tu kufahamishwa. Wapo waliojaribu kumbana Waziri wakijibishana naye masuala ya kisiasa. Wote walipewa nafasi katika hizo saa nne. Muhimu ilikua kuithamini nchi yako.

2. Evans Mela akiuliza swali© 2013 Urban Pulse Creative
Evans Mela akiuliza swali.
Balozi wetu London, Mheshimiwa Peter Kallaghe alipomkaribisha mgeni alisema hawa ni Watanzania wanaoipenda nchi yao. Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo mwenye miaka 58 ni mwanataaluma aliyebobea kielimu. Mbali na tuzo saba za kitaifa na kimataifa alizoshapewa ni mhariri wa jarida la kisayansi Afrika (Africa Earth Science Journal). Anaheshimika kiulimwengu na si ajabu anao wadhifa wa Makamu Rais wa Tume ya Ramani ya Madini duniani iliyoundwa 1881 Ufaransa. Lengo lake ni kuendeleza masuala ya mazingira, madini na hali ya hewa. Mtanzania huyu ni pia mwanachama wa Jumuiya mbalimbali za jiolojia, Tanzania, Marekani, China na Uingereza.
3. Balozi Kallaghe akimkaribisha Waziri kuongea na Watz UK© 2013 Urban Pulse Creative
Balozi Kallaghe akimkaribisha Waziri kuzungumza na wananchi.
Tunavyokuja kumsikiliza tunataka ukweli, maana wanayansi hawaropoki ovyo.
Lakini…
Mtanzania hahitaji usomi na taaluma pekee; anatalilia kutatuliwa matatizo ya mgao wa umeme, nyumba, chakula, kusomesha watoto wetu nk…
Na hayo sasa ndiyo ya kutafakari kuhusu makutano na Waziri Muhongo Jumanne iliyopita tarehe 26 ukumbi wa Ubalozi wa Tanzania, Uingereza.

4. Prof Muhongo akiongea na Watanzania, kulia Balozi P Kallaghe © 2013 Urban Pulse Creative_99
Maongezi ya saa nne bila kupumzika. Waziri Sospeter Muhongo akiwa kazini na mwenyeji wake kando.
Waziri aligawa maongezi mafungu matatu.
1. Umeme
2. Madini
3. Maswali na majibu.
Kiwajihi na kisaikolojia hakuna hata nukta moja Mbunge huyu wa kuteuliwa alipopepesa pembeni kutazama kijikaratasi au kumwomba Katibu wake aliyeongozana naye (Bw Sosthenes Massola) amkumbushe kitu. Ni kiongozi anayefaham anachokisema. Kwa saa nne nzima takwimu, mahesabu na maelezo vilimbubujika kinywani bila kusita.

1. SUALA LA UMEME
Alisisitiza nchi yetu haiwezi kondokana na umaskini bila kuendeleza umeme. Wastani wa kipato chetu kitaifa (“Gross National Income”) ni dola 23 hadi 24 bilioni. Hizo zikigawanywa kwa kila Mtanzania ni dola 500 (takiban shilingi laki nane na nusu) na yathibitisha sisi taifa maskini. Lengo ni kufikisha dola 1,250 hadi 1,300 mwaka 2025.
Asilimia 18.4 ya Watanzania tu ndiyo wanaotumia umeme. Kati yao asilimia 6.6 wako vijijini.
BILA KUTUMIA UMEME HATUWEZI KUONDOKANA NA UMASKINI.
Sababu kibao. Mabwawa ya maji ya kizamani. Muundo wa shirika la Umeme (TANESCO) wenye mfumo wa kizamani, nk.

6. Ellly Njau-Benichou aliyeuliza swali kuh gesi na elimu© 2013 Urban Pulse Creative
Mjasiria mali, Elly Njau-Benichou aliyeuliza swali kuhusu gesi na elimu.
Lengo la Wizara yake ni kufikisha umeme kufikia asilimia 30 mwaka 2015. Moja ya masuluhisho yaliyoshaanza ni bei ya kuunganisha umeme kushushwa toka laki 4 au 5 hadi laki 1.7.
WATANZANIA TULIO NJE TULIKUMBUSHWA KUJENGA NYUMBANI.
Kuunganisha umeme shule ya msingi ya kijijini kwako ni shilingi milioni nne; “ukitaka kujenga zahanati ni milioni kumi”. CHANGIA MAENDELEO KWENU.
LAKINI TATIZO HILI SI LA BONGO TU.
Nchi zilizoendelea ki uchumi Afrika zina umeme kila sehemu. Asilimia 99 ya wananchi wa Mauritius wanao, ilhali Afrika Kusini ni 75%.
WAZIRI ALIKUMBUSHA TWAHITAJI KUWA NA NJIA NYINGI KUPATA UMEME.
Gesi inapatikana kwa wingi. Kwa sasa tunatumia kidogo sana (toka Songo Songo); akatoa takwimu akasema nyingine zimegunduliwa Mtwara na maeneo hayo yote.
Hivyo matumizi ya gesi ndiyo yatakayotuondoa choo cha umaskini. Kila siku magunia 40,000 ya mkaa yanatumika Dar es Salaam. Tunaweza pia kutumia mimea (“bio-energy”); nchi nyingi duniani hutumia mimea; mathalan miwa na sukari kupata petroli, Brazil.
WATANZANIA TUNATAKIWA TUWE WATU WA KARNE YA 21 SIO WA KUNI NA MIKAA.

5. Andy Mkwavi akiuliza swali© 2013 Urban Pulse Creative_4
Andy Mkwavi aliyetaka ufafanuzi juu ya Uzalendo wa viongozi wetu.

2. SUALA LA MADINI
Hapa Profesa Muhongo alisisitiza azma yake si kupoteza muda kwa kelele za malumbano. Alisema iko migodi sita ya dhahabu, Tanzania. Akagusia juu ya sheria ya Madini ya mwaka 2010 ambayo imepandisha mrabaha kutoka asilimia 2 kwenda asilimia 3 na kodi ya mamlaka kufikia asilimia 30. Umuhimu wa misingi ya Sheria hiyo ni kuwapa kipaumbele wamiliki migodi wa Kitanzania (hata wakishirikiana na wageni) usipungue asilimia 50. Alikumbusha juu ya faida za migodi kama kutoa ajira na kuwafariji wananchi wanaoizunguka.
Hapa tukirukia baadaye wakati wa maswali kuna aliyetaka kujua iweje kuna watu binafsi wanafaidi. Waziri akafafanua madini yote ni mali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
HUWEZI UKAUZA DHAHABU YAKO POPOTE. KUNA SOKO LA KIMATAIFA NA SHERIA ZAKE.
Dhahabu ni pato kubwa la kitaifa. Akatoa mfano wa serikali ya Marekani inayomiliki tani 10,000 za dhahabu. Si ajabu Marekani taifa tajiri.

Waziri akiongea Ukumbi wa Ubalozi Uingereza© 2013 Urban Pulse Creative_98
Akagusa mengi lakini moja muhimu la kukumbuka ni kuwa dunia ya leo pia ina madini mpya ambazo zamani hazikuangaliwa. Madini zinazotumika kujenga tarakilishi, ndege na simu za mkononi mathalan.
CHINA INAONGOZA DUNIA KWA MADINI HIZI MPYA KWA ASILIMIA 95.
Ndiyo maana kila nchi (ikiwemo Tanzania) zinatafuta migodi. Tunayo madini. Lindi kuna mawe. Singida yapo matale (“granite”). Matale tunavyojua hutumika kujenga madaraja, majumba, maeneo ya juu ya fenisha nk.
3.MASWALI NA MAJIBU- TUBADILI MTAZAMO
Kila muulizaji alipoanza swali na “serikali inafanya au itafanya nini” alikumbushwa huo ni “mtazamo wa kizamani.”
SERIKALI SI SAYARI NYINGINE. TUSIWE TUNASEMA SERIKALI, SERIKALI. SISI WENYEWE NDIYO SERIKALI.
Aliposema hivyo alinikumbusha Rais wa zamani Marekani hayati John Kennedy aliyemtaka kila mwananchi kujiuliza utalifanyia “nini taifa lako badala ya taifa litakufanyia nini.”
Waziri alitoa mfano wa Wakenya walipokuwa wakichangiana kumtuma mtoto wa mwenzao kusoma India au Marekani. Sisi tukitoa michango ni kufanya arusi. Mantiki yake Waziri hapa ni moja.
WATANZANIA TUJITUME NA TUPENDANE.
Yupo dada aliyejuza vipi serikali itaelemisha watu kuhusu matumizi ya gesi. Waziri alisisimama hapo kwamba sisi wenyewe tuelemishana na kusaidiana, badala ya kutegemea sana serikali. Watanzania hatuna tabia ya kusoma.
YALIKUWEPO MADUKA MENGI YA VITABU MIAKA YA SITINI NA SABINI MIJINI. LEO YAMEGEUZWA MADUKA YA NGUO.
Watanzania wavivu kusoma kiasi ambacho unaweza kutoa vijikaratasi vya kuelezea matumizi ya gesi, mtu akayatumia kufungia vitumbua.
Asilimia 60 ya magazeti ni ya udaku, starehe kuliko kuelemisha.
Kuna uvivu wa kusoma kiasi ambacho kuna mtu yuko radhi kununua shahada za udokta ilhali kamaliza darasa la saba.
IKIWA BAADHI YA VIONGOZI WANANUNUA SHAHADA ZA BANDIA JE, WATOTO WATAMWIGA NANI?
Ndani ya mada hii liliamka tena nyigu la tafrani za Mtwara, ambazo Waziri alitoa maelezo marefu. Sababu si tu za kicuhumi alisisitiza Waziri. KUNA MENGINE.
Akasema alipolihutubia Bunge mwaka jana alitawanya maelezo DHAHIRI ya mabomba na uchimbaji gesi. Akasema anakumbuka suala la mabomba lilikua ukurasa wa 79. Wabunge walisoma kisha wakapitisha hoja yake. Baadaye “wakamgeuka.”
Akaendelea kusema Wizara iligharimu kuwapeleka madiwani na viongozi waliochaguliwa toka Lindi, Mtwara na Kilwa kujisomea ughaibuni : Trinidad, Tobago na Norway. Lakini waliporudi hawakutekeleza walichokisoma.

Habari na Picha na Urban Pulse.
ChanzoMjengwaBlogs.

No comments:

Post a Comment