Sunday, March 3, 2013

Maalbino kuandamana nchini kudai haki zao.

Watu wenye ulemavu wa ngozi (albino) wanakusudia kufanya maandamano makubwa nchini kudai haki zao za kulindwa na kuishi kama Watanzania wengine.

Wamedai ikishindikana watafikisha kilio chao mataifa ya nje kulaani mauaji yanayofanywa dhidi yao kwa njia za kishirikina.

Hayo yalielezwa na mwanaharakati wa haki za walemavu nchini, Josphat Tonner, aliyefuatana na viongozi wa Chama cha Wazazi wa watoto wenye ulemavu Tanzania katika mkutano na waandishi wa habari uliyofanyika jijini hapa.

Tonner alisema suala la mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi, albino haliwezi kupatiwa ufumbuzi na kumalizika kwa sababu kuna dalili zinazoonyesha kuwa watu wakubwa wenye nafasi zao wanahusika na mauaji hayo.

Alidai kuwa wanaohusika na matukio hayo ni viongozi wakubwa wanaotaka madaraka kwa njia za kishirikina.

Alidai wahusika wakubwa wa mauaji hayo ni vigogo wanasiasa wenye imani za kishirikina ambao wanawatumia waganga wa tiba asilia kwa kudhani kwamba wanaweza kupata madaraka kupitia kiungo cha albino.

“Huu ndio ukweli watu wakubwa wenye madaraka ndani ya nchi hii ndiyo waasisi wakubwa wa mauaji haya, ndiyo maana hakuna kiongozi yeyote mwenye utashi wa kulishughulikia suala hili…wao ndio wahusika wakuu kwa kusaka vyeo vya kisiasa,” alisema Tonner.

Alitaja miongoni mwa sababu za kuwahusisha wakubwa na mauaji hayo kuwa ni pamoja na kutumia njia zisizo sahihi katika kushughulikia tatizo hilo ikiwamo uundwaji wa tume zisizo na mashiko na ambazo zipo kama danganya toto.

Aidha alidai zaidi ya watu 200 waliohusishwa na kesi za mauaji ya albino ni kesi tatu tu zilizofikishwa mahakamani ambazo mpaka sasa alieleza kuwa hazifahamiki hatima yake pamoja na usiri mkubwa uliopo katika kupata taarifa za matukio hayo.

Naye Mwenyekiti wa Chama hicho taifa, Omari Tuwa alieleza kuwa wimbi la ukatili na mauaji ya albino limeongezeka na kwamba mpaka sasa zaidi ya watu 70 wenye ulemavu wa ngozi wameuawa, 28 kujeruhiwa na 19 makaburi yao kufukuliwa.

Tuwa alilaani vitendo hivyo na kumuomba Rais Jakaya Kikwete kuingilia kati na kuchukua hatua za makusudi kutokomeza vitendo hivyo kwa kuwa wanaouawa ni Watanzania na wapigakura ambao kura zao ni miongoni mwa zilizomweka madarakani.
 
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

No comments:

Post a Comment