RAIS Jakaya Kkikwete. |
Utangulizi
Ndugu wananchi;
Namshukuru
Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehma, kwa kutujalia uzima na kutuwezesha
kuwasiliana kupitia utaratibu wetu mzuri tuliojiwekea wa kufanya hivyo
kila mwisho wa mwezi. Leo nimepanga kuzungumza nanyi mambo
matatu; yaani Mpango wa Amani, Usalama na Ushirikiano wa Jamhuri ya
Kidemokrasi ya Kongo, Uhusiano wa Waislamu na Wakristo na Matokeo ya
Mtihani wa Kidato cha Nne.
Mpango wa Amani, Usalama na Ushirikiano wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo
Ndugu Wananchi;
Tarehe
8 Februari, 2013 kule Addis Ababa, Ethiopia niliungana na Katibu Mkuu
wa Umoja wa Mataifa, Mhe. Ban Ki-Moon, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja
wa Afrika, Mhe. Nkosozana Dlamini Zuma na viongozi wa nchi 12 za Afrika
Mashariki, Kati na Kusini kutia saini Mpango wa Amani, Usalama na
Ushirikiano wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo na jirani zake. Pamoja
na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo zilikuwepo nchi za Burundi, Rwanda,
Uganda, Sudani Kusini, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Jamhuri ya Kongo,
Angola, Zambia na Tanzania ambazo ni jirani ya Kongo. Nchi za Ethiopia,
Msumbiji na Afrika ya Kusini pamoja na Umoja wa Mataifa na Umoja wa
Afrika zilitia saini kama wadhamini. Ethiopia kwa nafasi yake ya kuwa
Mwenyekiti wa sasa wa Umoja wa Afrika na Msumbiji kwa kuwa Mwenyekiti wa
Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC). Nchi wanachama wa
Mkutano wa Ukanda wa Maziwa Makuu ziliwakilishwa na Uganda ambayo ni
Mwenyekiti wake wa sasa. Afrika ya Kusini ilishirikishwa kwa kuwa taifa
kubwa na linalotegemewa katika ukanda wetu.
Mpango
huu ni jitihada nyingine ya kusaidia Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo
ipate amani ya kudumu. Kama tujuavyo, tangu mwaka 1997 wakati wa vita
vilivyosababisha kuondolewa kwa Rais Mobutu Seseseko mpaka sasa nchi
hiyo rafiki na jirani haijapata amani na utulivu wa kudumu. Kumekuwepo
jitihada na mipango kadhaa ya kuleta amani ambayo hata hivyo baada ya
muda fulani machafuko hutokea tena na mipango hiyo kuvurugika.
Inakadiriwa kuwa takriban watu milioni 5.4 wamepoteza maisha na watu
wengi kuwa wakimbizi ndani na nje ya nchi yao. Pia kumekuwepo na
vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto pamoja na mali nyingi
kuharibiwa au kuporwa.
Ndugu Wananchi;
Machafuko
yaliyoanzishwa na waasi wa Kundi la M23 mapema mwaka wa jana ndiyo
sababu ya kuwepo kwa Mpango huu wa sasa tuliotia saini kule Addis Ababa,
Ethiopia tarehe 8 Februari, 2013. Katika Mpango huo Jamhuri ya
Kidemokrasi ya Kongo na jirani zake, Tanzania ikiwemo, tumekubaliana
kutokufanyiana vitendo vinavyohatarisha amani na usalama wa nchi zetu.
Tumeazimia tusifanye hivyo ama moja kwa moja kama nchi au kwa kutumia
watu wengine. Aidha, tumekubaliana tusiruhusu watu au vikundi vya watu
kutumia nchi zetu kuhatarisha usalama wa nchi nyingine. Kimsingi
tumekubaliana kuwa majirani wema. Katika Mkataba huo, majukumu ya kila
nchi yameainishwa vizuri pamoja na yale ya Umoja wa Mataifa, Umoja wa
Afrika na Mashirika ya Kikanda hususan SADC na ICGLR.
Ndugu Wananchi;
Niliamua
kukubali kushiriki na kutia saini Mpango ule kwa kutambua ukweli kwamba
sisi majirani wa nchi ya Kongo tunao wajibu wa kusaidia kwa kile
tunachoweza. Wananchi wa Kongo wameteseka kwa muda mrefu mno hivyo kama
Mpango huu utawasaidia kupata amani na usalama hatuna budi kuunga
mkono. Ni kwa misingi hiyo hiyo, tulikubali kuchangia kikosi kimoja
katika Jeshi la Kimataifa la kulinda amani huko Mashariki ya Kongo kama
ilivyoamuliwa na Mkutano wa Nchi za Maziwa Makuu mwezi Julai, 2012.
Uamuzi huo umeungwa mkono na Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika na
Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika. Umoja wa Mataifa umeamua
Jeshi hilo liwe sehemu ya Jeshi la Umoja wa Mataifa la Kulinda Amani
nchini Kongo (MONUSCO) jambo ambalo sote tumeliafiki. Tumepeleka
walinzi wa amani Darfur, Sudan na Lebanon, kwa nini tusipeleke Kingo.
Miaka ya nyuma tulishapeleka walinzi wa amani Liberia, Siera Leon na
Eritrea.
Ni
matumaini yetu kuwa Mpango huu mpya utatekelezwa kwa ukamilifu na kuzaa
matunda yaliyokusudiwa. Kama nchi jirani, Jamhuri ya Kidemokrasi ya
Kongo yenye amani, usalama na utulivu ni jambo lenye maslahi makubwa
kwetu. Ina maana ya kutokuwa na wakimbizi kutoka nchi hiyo, uharamia
katika Ziwa Tanganyika kutokuwepo na ustawi wa shughuli za kiuchumi na
kibiashara kwa upande wetu na wao. Ni chachu muhimu ya maendeleo ya
Mikoa ya pembeni mwa Ziwa Tanganyika na Tanzania kwa jumla.
Uhusiano wa Waislamu na Wakristo
Ndugu wananchi;
Jambo la pili ninalopanga kulizungumzia siku ya leo ni uhusiano wa
Wakristo na Waislamu hapa nchini. Kwa miezi kadhaa sasa tangu mwaka wa
jana kumekuwepo na matukio kadhaa yanayosababisha mifarakano na
kupandikiza chuki baina ya waumini wa dini ya Kikristo na Kiislamu.
Matukio ya kauli na vitendo vya kudharau dini za wengine, kunajisi
vitabu vitakatifu vya dini hizo, kuchoma moto nyumba za ibada na mzozo
kuhusu nani achinje. Kumekuwepo na matumizi mabaya ya radio na simu
za mkononi na mifumo mingine ya mawasiliano iliyoeneza maneno na ujumbe
wa chuki na vitisho kwa waumini na viongozi wa dini zetu hizi kubwa
hapa nchini. Kauli na matendo hayo, katika baadhi ya maeneo yamekuwa
chanzo cha uhasama na magomvi baina ya waumini na hatimaye kusababisha
vifo kama ilivyotokea Buseresere Mkoani Geita na Beit-el-Ras, Zanzibar.
Ndugu zangu;
Watanzania
hatujawahi kuwa hivi, kumetokea nini? Miaka yote Watanzania ni watu
tunaotambua na kuheshimu tofauti za dini zetu mbalimbali tunazoabudu.
Watanzania ni waelewa na kwa ajili hiyo tumekuwa tunavumiliana kwa
tofauti zetu na ndiyo maana tumekuwa tunaishi pamoja kidugu, kwa umoja
na kushirikiana kwa mambo yote yanayotuhusu maishani isipokuwa wakati
kila mmoja anapoingia kwenye nyumba ya ibada kumuomba Mola kwa misingi
na taratibu ya dini yake.
Watanzania
wa dini zote na makabila tofauti wanaishi nyumba moja, wanasoma pamoja,
wanafanya kazi pamoja kwa udugu, upendo, umoja na ushirikiano. Kuna
koo na familia zenye watu wa dini tofauti, wengine Waislamu na wengine
Wakristo. Wapo Waislamu na Wakristo wameoana, wamezaa na wamejukuu na
kila mmoja amebakia kuwa mfuasi wa dini yake. Wapo pia ambao hawakuoa
lakini wamezaa watoto na wanashirikiana kulea watoto wao. Hayo ndiyo
maisha ya Watanzania na hiyo ndiyo Tanzania yenye amani na utulivu
tuliyozaliwa, kukua na kuishi. Nawasihi sana Watanzania wenzangu,
tuienzi na kuidumisha tunu hii waliyotujengea mababu zetu.
Ndugu Wananchi;
Kuna
wenzetu kwa sababu wanazozijua wao na kwa manufaa wanayoyajua wao
wanataka kutuvurugia nchi yetu hii nzuri. Tusiwape nafasi wachochezi
hawa kwani hawatutakii mema na wala hawazitakii mema dini zetu na nchi
yetu. Sisi katika Serikali hatutasita kuwachukulia hatua wale wote
wanaochochea chuki za kidini, wanaodharau vitabu vitakatifu vya dini
nyingine na wanaokejeli dini nyingine.
Nimewakumbusha
Polisi na mamlaka husika kote nchini wasifanye ajizi kwenye matukio ya
namna hiyo. Wawachukulie hatua stahiki wale wote wanaohusika.
Nimewataka wazingatie msemo wa Kiswahili usemao “ajizi nyumba ya njaa”.
Wachochezi wa mifarakano na chuki za kidini wasipodhibitiwa ipasavyo
wataleta maafa kwa Watanzania wasiokuwa na hatia. Nimewakumbusha Wakuu
wa Wilaya na Mikoa kama walinzi wa amani wa maeneo yao ya uongozi,
watimize ipasavyo wajibu wao. Pia nimewataka Polisi wakamilishe mapema
upelelezi wa makosa ya vurugu za kidini na wahusika wafikishwe haraka
kwenye vyombo vya sheria ili iwe fundisho kwa wengine.
Ndugu Wananchi;
Naendelea
kuwasiliana na viongozi wa dini kuzungumza nao juu ya wajibu wao maalum
wa kuhakikisha kuwa wafuasi wao hawawi chanzo au sehemu ya tatizo na
mifarakano miongoni mwa waumini wa dini mbalimbali nchini. Hali
kadhalika naitumia nafasi hiyo kuwakumbusha umuhimu wa kuzungumza na
wenzao wa upande mwingine kutatua tofauti au matatizo yanayoathiri
uhusiano mwema baina yao.
Ndugu Wananchi;
Kuna
msemo maarufu usemao “mjenga nchi ni mwananchi na mbomoa nchi ni
mwananchi”. Naomba tuwe wajenga nchi na kamwe tusikubali kuwa wabomoa
nchi. Hivi tukiibomoa nchi yetu tutakwenda wapi? Tutaishi wapi?
Tusikubali kugeuka wakimbizi ndani ya nchi au nje ya nchi yetu.
Kwa
mara nyingine tena, napenda kutumia nafasi hii kuwapa mkono wa pole
makanisa, familia, ndugu na jamaa wote wa Mchungaji Kachila na Padri
Mushi. Sote tunafahamu machungu waliyonayo kwa kuondokewa na wapendwa
wao. Serikali na wapenda amani wote nchini wapo pamoja nanyi katika
kipindi hiki kugumu. Vile vile natoa rambirambi zangu nyingi kwa
waumini wote wa Kanisa la Pentekoste Assemblies of God na Kanisa
Katoliki Tanzania kwa kuondolewa ghafla na viongozi wao. Tuzidi kumwomba
Mwenyezi Mungu azipumzishe kwa amani roho za viongozi wetu. Amin.
Matokeo ya Mtihani wa Kidato cha Nne Mwaka 2012
Ndugu wananchi;
Tarehe
18 Februari, 2013 Baraza la Mitihani la Taifa lilitangaza matokeo ya
Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Nne ya mwaka 2012. Wanafunzi 397,132
walifanya mtihani huo na kati ya hao, waliofaulu ni 126,851 yaani sawa
na asilimia 34.5. Wanafunzi 240,903 ambao ni sawa na asilimia 65.5
hawakufaulu mtihani huo. Kwa ulinganifu, matokeo hayo ni mabaya kuliko
matokeo mengine ya mtihani huo ya miaka ya hivi karibuni.
Mwaka
2011, jumla ya wanafunzi 336,782 walifanya mtihani huo na waliofaulu
walikuwa asilimia 53.6 na ambao hawakufaulu kabisa walikuwa asilimia
46.4. Mwaka 2010 jumla ya wanafunzi 352,045 walifanya Mtihani wa Taifa
wa Kidato cha Nne, asilimia 50.4 ya wanafunzi hao walifaulu na asilimia
49.6 ya wanafunzi hawakufaulu.
Ndugu Wananchi;
Matokeo
ya mitihani ya kidato cha nne mwaka 2012, yameshtua na kufadhaisha watu
wengi nchini na kwa sababu stahiki kabisa. Kwanza, kwamba kiwango cha
kufaulu kimeporomoka sana, tena ghafla, kutoka asilimia 53.6 mwaka 2011
hadi asilimia 34.5 mwaka 2012. Hili ni anguko la asilimia 19.1 ambalo,
kwa kila hali, ni kubwa sana. Pili, kwamba hata shule zinazofahamika
kuwa na historia ya kufaulisha vizuri kama vile seminari, shule za watu
binafsi, za mashirika ya dini na sekondari kongwe za Serikali ambazo
hazina matatizo kama ilivyo kwa zile sekondari za Kata, nazo safari hii
hazikupata mafanikio kama ilivyo kawaida yao. Nazo zimejikuta zikiwa na
idadi ya vijana waliopata daraja la kwanza, la pili na la tatu
ikipungua wakati waliopata daraja la nne na waliofeli wakiongezeka.
Isitoshe
na kiwango cha ufaulu wa vijana umepungua pia. Mwaka 2010 wanafunzi 10
bora wote walikuwa wamefaulu daraja la kwanza la alama au pointi 7.
Mwaka 2011 katika wanafunzi 10 bora wanane walipata daraja la kwanza kwa
alama 7 na wawili alama 8. Mwaka 2012 katika wanafunzi 10 bora,
watatu walipata daraja la kwanza kwa alama 9, watatu alama 10 na wawili
alama 11.
Ndugu Wananchi;
Haya
ndiyo mambo yanayozua maswali kwa watu wengi yanayohitaji kupatiwa
majawabu ya uhakika. Kulikoni mwaka 2012? Ndiyo msingi wa uamuzi wa
Waziri Mkuu, Mhe. Mizengo Pinda, kuamua kuunda Tume ya kuliangalia suala
zima la mitihani ya mwaka 2012 na matokeo yake. Hali hii haijawahi
kutokea katika miaka ya hivi karibuni. Ni suala muhimu sana kwa
maendeleo ya nchi yetu, hivyo lazima ukweli wake ujulikane kwa uhakika.
Hii itawezesha Serikali na wadau wengine kuchukua hatua stahiki
kurekebisha mambo mapema iwezekanavyo ili hatimaye mambo yawe mazuri
siku za usoni. Tusipofanya hivyo mambo yanaweza kuwa mabaya zaidi na
lawama zinaweza kuwa kubwa zaidi kwa Serikali.
Ndugu Wananchi;
Hivi
sasa kunatolewa mawazo lukuki kuhusu sababu za kwa nini matokeo
yamekuwa mabaya. Wapo wanaodhani kuwa lipo tatizo katika utungaji wa
mitihani, usahihishaji wake au kutoa maksi kwa watahiniwa. Wapo
wanaodhani walimu hawawajibiki ipasavyo au baadhi yao kutokumudu masomo
wanayofundisha. Wapo wanaofikiria kuwa wanafunzi hawako makini katika
kufuatilia masomo na wazazi hawajali kufuatilia maendeleo ya watoto wao
shuleni. Wapo wanaoinyooshea kidole Serikali kwa sera, mitaala na
uwekezaji usiokidhi mahitaji ya maendeleo ya elimu. Wapo wanaofikiria
kuwa Serikali kushindwa kuongeza mishahara ya walimu kwa asilimia 100
kama walivyotaka imechangia. Orodha ni ndefu, ali mradi kila mtu ana
mawazo yake. Na sisi katika Serikali hatuwezi kuwa tunadhani kwa sababu
tunayo dhamana maalum. Lazima tujue ukweli kwa uhakika na ndiyo maana
kuna umuhimu wa Tume. Naomba kila mtu mwenye mawazo yake ayafikishe
kwenye Tume hiyo hapo itakapoundwa ili tupate jawabu muafaka la tatizo
hili.
Ndugu Wananchi;
Napenda
kuwahakikishia kuwa sisi katika Serikali tumetoa kipaumbele cha juu
sana kwa elimu na kwamba hakuna upungufu wa utashi kwa upande wangu na
wenzangu wote Serikalini. Ndiyo maana tumeguswa sana na matokeo haya.
Bajeti ya elimu ya shilingi trilioni 3.6 ambayo ni sawa na asilimia 24
ya bajeti yote ya Serikali ndiyo kubwa kuliko zote. Kwa ajili hiyo
imetuwezesha kuendelea kukabili mahitaji na changamoto za upanuzi mkubwa
wa elimu ya sekondari na elimu ya juu. Bado hatujazimaliza changamoto
zote na kwamba bado tuna kazi kubwa mbele yetu, lakini mafanikio
yanaendelea kupatikana. Tutaendelea kutoa kipaumbele cha juu kwa elimu
mpaka hapo itakapofikia mahali kwamba matatizo makubwa yatakapokuwa
yamepungua sana.
Hitimisho
Ndugu Wananchi;
Mungu Ibariki Tanzania!
Mungu Ibariki Afrika!
Nashukuru kwa kunisikiliza!
No comments:
Post a Comment