Waziri wa Fedha Dr.William Mgimwa. |
Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa, ameliambia gazeti la Mtanzania Jumapili kuwa wizara yake imekopa fedha hizo Benki ya Dunia ili iweze kulisaidia Shirika la Ugavi wa Umeme (TANESCO) linalokabiliwa na ukata mkali.
Jana Waziri Mgimwa alieleza TANESCO inakabiliwa na ukata wa kutisha unatokana na mzigo mkubwa wa madeni ya kampuni za ufuaji wa umeme zinazofanya biashara ya kuliuzia umeme Shirika hilo.
Alisema Wizara yake imekuwa na utaratibu ya kutenga fedha kila mwezi kwa ajili ya kulisaidia kusambaza umeme na mwezi huu inategemea kupata mkopo huo wa Shilingi bilioni 160 kutoka benki ya dunia ambazo zitapelekwa moja kwa moja TANESCO ili kulisaidia liweze kujiendesha na kulipa sehemu ya madeni yake.
Hata hivyo, taarifa kutoka ndani ya shirika hilo zimeeleza kuwa mkopo huo umeombwa mahususi kwa ajili ya kununulia mafuta mazito ya kuendeshea mitambo ya kufua umeme kutokana na tishio la nchi kuingia gizani baada ya kampuni zinazoiuzia umeme TANESCO kutishia kusitisha kwa kutolipwa malimbikizo ya madeni yake kwa muda mrefu.
Moja ya kampuni zinazotajwa kutishia kusitisha kuiuzia TANESCO umeme ni Songas ambayo zipo taarifa zinazoeleza kuwa imeshatoa taarifa kwa TANESCO ya kusudio la kufunga mitambo yake baada ya kutolipwa malimbikizo ya deni lake la Sh. bilioni 80.
Tayari mgawo wa umeme umeshaanza kuyaadhili baadhi ya maene mbalimbali hapa nchini kutokana na uhaba wa Nishati ya umeme ingawa Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo na TANESCO wamekuwa wakikwepa kueleza ukweli iwapo mgawo upo au la.
Taarifa za kuwepo mgawo wa umeme wa kimya kimya zinaonekana kumuumbua Waziri Muhongo na wasaidizi wake ambao wamepata kukaririwa mara kadhaa wakieleza kuwa wizara ya Nishati na Madini ikiwa chini ya usimamizi wao hakutakuwa na mgawo wa umeme.
via gazeti la Mtanzania
No comments:
Post a Comment