Sunday, March 3, 2013

SIMBA SC INAWEZA KUFANYA KILE AMBACHO WENGI HATUTARAJII HII LEO.

WAWAKILISHI wa Tanzania Bara katika Ligi ya Mabingwa Afrika, leo wanashuka kwenye Uwanja wa Manispaa mjini Calulo, kumenyana na wenyeji Recreativo de Libolo katika mchezo wa marudiano, Raundi ya Kwanza Ligi ya Mabingwa Afrika.
 

Katika mchezo huo, wenyeji wanapewa nafasi kubwa ya kusonga mbele kutokana na ushindi wa ugenini wa 1-0 katika mchezo wa kwanza uliofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
 

Ili kusonga mbele, Simba watatakiwa kuifunga Libolo mabao 2-0, au kushinda 1-0 na mchezo uhamie kwenye mikwaju ya penalti, ambako bila shaka Juma Kaseja, mlinda bora nchini anaweza kufanya maajabu. Mashabiki wengi wa Simba SC wanaonekana kukatishwa tamaa na timu yao si tu kutokana na matokeo ya awali, bali matokeo ya hivi karibuni ya timu hiyo kwa ujumla yamekuwa si mazuri.
 

Benchi la Ufundi la Simba SC, chini ya kocha Mkuu, Mfaransa Patrick Liewig lina matumaini ya kufanya vizuri katika mchezo huo, baada ya kufanyia makosa yaliyojitokeza katika mchezo wa awali. 
 

Sahau kuhusu aina ya timu ya sasa ya Simba SC na matokeo yake, rejea kwenye historia ya timu hiyo, je itaweza kuupanda mlima kinyumenyume? Historia inasema Simba SC inaweza kushinda ugenini, hata ikitoka kufungwa nyumbani na kusonga mbele kwenye michuano ya Afrika. 
MAAJABU YA SIMBA SC MECHI ZA UGENINI AFRIKA MWAKA 1974: 
 

Ilikuwa ni katika Raundi ya Kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika, wakati Simba ilipoanzia ugenini na Linare ya Lesotho na katika mchezo huo ilishinda mabao 3-1 ugenini, kabla ya kuja kushinda tena 2-1 nyumbani na kusonga mbele.
 

Simba iliendelea kufanya vizuri katika michuano hiyo, katika Raundi ya Pili ilianzia tena ugenini na kuanza na ushindi wa 2-1 dhidi ya timu ya jeshi la Zambia, kabla ya kuja kushinda tena 1-0 nyumbani, hivyo kukata tiketi ya kutinga Robo Fainali ya michuano hiyo.
 

Katika Robo Fainali, Wekundu hao wa Msimbazi waliangukia kwa timu ngumu na tishio wakati huo barani, Hearts Of Oak ya Ghana na wakapangiwa kuanzia ugenini tena. Mabao ya Adam Sabu (sasa marehemu) na Abdallah Kibadeni yaliipa Simba SC ushindi wa 2-1 mjini Accra.
 

Katika mchezo wa marudiano, Simba ilitoka sare ya bila kufungana na waghana hao, hivyo kutinga Nusu Fainali, ambako safari yao ilikoma, baada ya kutolewa na Mehallal El Kubra ya Misri. 
 

Simba ilishinda 1-0 kwenye mchezo wa kwanza Dar es Salaam, nayo ikaenda kufungwa 1-0 katika mchezo wa marudiano Misri, kabla ya Mehallal kushinda kwa penalti 3-0, ingawa kuna habari za kipa wa Simba wakati huo, Athumani Mambosasa (sasa marehemu) kufanyiwa fujo, wakati wa upigwaji wa penalti na kutishiwa kwa bastola.
Kikosi cha Simba.
                                                              MWAKA 1979: 
 

Ilikuwa ni katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, wakati Simba ilipopangwa kuanza na Mufulira Wanderers ya Zambia na  mchezo wa kwanza ulifanyika Dar es Salaam. Katika mastaajabu ya wengi, Simba SC ilitandikwa mabao 4-0 Uwanja wa Taifa na wengi kukata tamaa ya timu hiyo kusonga mbele.
 

Hata hivyo, katika mchezo wa marudiano mjini Lusaka, Wekundu wa Msimbazi waliibuka na ushindi wa mabao 5-0 na kusonga mbele kwenye michuano hiyo, ambako hata hivyo safari yao iliishia, baada ya kutolewa na Racca Rovers ya Nigeria. Simba ilianza kwa kulazimishwa sare ya bila kufungana Dar es Salaam, kabla ya kwenda kuchapwa mabao 2-0 na Racca Rovers nchini Nigeria.
MWAKA 1993:
 

Ilikuwa ni katika michuano ya Kombe la CAF, ambayo wakati huo ilikuwa ikishirikisha washindi wa tatu wa Ligi barani. Simba ilianza vibaya, baada ya kulazimishwa sare ya bila kufungana Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na Ferroviario de Maputo ya Msumbiji. 

Mashabiki wengi wa Simba walijua safari imeiva, lakini katika mchezo wa marudiano, Simba ilitoa sare ya  1-1 ugenini hivyo kusonga mbele kwa faidfa ya bao la ugenini.
 

Huu ndio mwaka ambao Simba ilipata mafanikio makubwa zaidi katika ushiriki wake wa michuano ya Afrika, kwani ilifika hadi fainali ya michuano hiyo. Katika 

Raundi ya Pili, pia Simba ilishinda mechi zote mbili, dhidi ya Manzini Wanderers ya Swaziland, 1-0 nyumbani na 1-0 ugenini, hivyo kuingia Robo Fainali, ambako ilikutana na timu ngumu kutoka Algeria, USM El Harrach.
 

Simba ilianza kwa ushindi wa mabao 3-0 Dar es Salaam, kabla ya kwenda kufungwa 2-0 ugenini hivyo kusonga mbele. 

Kabla ya mchezo wa marudiano, Simba iliweka kambi ya wiki moja mjini Nice, Ufaransa, chini ya ufadhili wa Azim Dewji enzi hizo.
 

Katika Nusu Fainali, Wekundu hao wa Msimbazi walikutana na timu ngumu kutoka Angola, Atletico Sports Aviacao na katika mchezo wa kwanza Dar es Salaam walishinda 3-1 na marudiano, wakalazimisha sare ya bila kufungana.
 

Simba SC ikaandika historia ambayo hadi leo haijafutwa, kuwa timu ya kwanza kufika fainali ya Kombe la Afrika, ambako hata hivyo ilikwenda kufungwa na Stella Abidjan ya Ivory Coast. 

Mchezo wa kwanza ugenini, Simba ilianza vema tu kwa kulazimisha sare ya bila kufungana, lakini katika marudiano, ikafungwa 2-0, mabao ya Boli Zozo.   
MWAKA 1996:
 

Ilikuwa ni katika michuano ya Kombe la Washindi, ambayo wakati huo ilikuwa ikishirikisha washindi wa pili wa Ligi za Afrika na ambayo kwa sasa imeunganishwa na Kombe la CAF na kuwa Kombe la Shirikisho. 

Simba SC ilipangwa kuanzia ugenini na Chapungu Rangers ya Zimbabwe na katika mchezo wa kwanza tu ugenini, ikaibuka na ushindi wa 1-0 ugenini.
 

Wapinzani wao wakakata tamaa na kujitoa kwenye mashindano, hawakuja kwenye mechi ya marudiano Dar es Salaam na Simba ikasonga mbele katika Raundi ya Pili, ambako ilikutana na Al Mokaoulun ya Misri.
 

Mchezo wa kwanza, Wekundu wa Msimbazi walishinda 3-1 na marudiano wakafungwa 2-0, hivyo wapinzani wao wakasonga mbele kwa faida ya bao la ugenini.
MWAKA 2003:
 

Ilikuwa ni katika Ligi ya Mabingwa Afrika, wakati Simba ilipoanza na ushindi mwembamba wa bao 1-0 dhidi ya timu ya Jeshi la Ulinzi la Botswana (BDF) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kwa jinsi ilivyobanwa kwenye mechi hiyo, wengi miongoni mwa mashabiki wa timu hiyo walikata tamaa.
 

Hata hivyo, katika mchezo wa marudiano, Wekundu hao wa Msimbazi waliibuka na ushindi wa mabao 3-1 na kurejea nyumbani kishujaa. Simba SC iliendelea kufanya vema katika michuano hiyo, baada ya kuitoa pia Santos ya Afrika Kusini katika Raundi ya Pili.
 

Mechi ya kwanza nchini Afrika Kusini, timu hizo zilitoka sare ya bila kufungana na katika mchezo wa marudiano mjini Dar es Salaam, baada ya dakika 120 matokeo yalibaki kuwa 0-0 ndipo mikwaju ya penalti ikaamua mshindi. 
 

Kipa Juma Kaseja alipangua mkwaju wa penalti wa Nahodha wa timu hiyo wakati huo, Mussa Otieno na Simba SC ikashinda kwa penalti 9-8 hivyo kuingia Raundi ya tatu na ya mwisho ya mchujo, ambako ilikutana na Zamalek ya Misri, waliokuwa mabingwa watetezi.
 

Mchezo wa kwanza Dar es Salaam, Simba SC ilishinda 1-0 na katika mchezo wa marudiano ugenini, ikaenda kufungwa 1-0, hivyo baada ya dakika 210 za kuumana kwa miamba hao, matokeo yalikuwa 1-1.
 

Ndipo mchezo ukahamia kwenye mikwaju ya penalti na huko, kipa Kaseja kwa mara nyingine aliibuka shujaa kwa kupangua penalti mbili za Waarabu na kuiwezesha Simba SC kuivua ubingwa Zamalek na kukata tiketi ya kucheza hatua ya makundi ya michuano hiyo kwa mara ya kwanza na ya mwisho kwao.  
MWAKA 2010:
 

Ilikuwa ni katika michuano ya Kombe la Shirikisho, wakati Simba SC ilipowashitua wengi baada ya kuanzia ugenini Zimbabwe dhidi ya wenyeji Lengthens FC na kufanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 3-0. Katika mchezo wa marudiano, Simba SC ‘ilimsukuma mlevi’ baada ya kushinda tena 2-1 na kusonga mbele.
 

Katika Raundi ya Pili, Simba haikufurukuta mbele ya Haras El Hodoud ya Misri baada ya kutolewa kwa jumla ya mabao 6-3. Simba SC ilishinda nyumbani 2-1, ikaenda kufungwa ugenini 5-1, hicho kikiwa ni kipigo kikubwa cha kwanza kihistoria na pekee kwa Simba SC katika mechi zake za Kaskazini mwa Afrika. 
Awali ya hapo, na hata baada ya hapo nyavu za Simba hazijawahi kutikiswa zaidi ya mara tatu za timu za Waarabu.
MWAKA 2013:
 

Simba SC inaingia kwenye mchezo wa marudiano wa Raundi ya Kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ikiwa nyuma kwa bao 1-0 ili isonge mbele. Hakuna njia nyingine ya kuifanya Simba iendelee kuwamo kwenye michuano hiyo zaidi ya ushindi.
 

Watu wanaidharau timu ya sasa, wanasema ni mbovu na haina washambuliaji, lakini kwa vyovyote ili isonge mbele inatakiwa kushinda 2-0, au 1-0 kisha ijaribu bahati yake kwenye mikwaju ya penalti. Simba SC inahukumiwa haina washambuliaji kwa sababu ilifungwa 1-0 nyumbani na Libolo, bila shaka hata jioni ile ambayo Simba ilifungwa 4-0 na Mufulira, washambuliaji wake hawakuwa vizuri kama walivyokuwa kwenye mchezo wa marudiano waliposhinda 5-0.
 

Felix Sunzu hakucheza mechi ya kwanza. Mrisho Ngassa hakuwa vizuri sana katika mchezo wa kwanza- na kwa ujumla Simba SC ilitengeneza nafasi kadhaa nzuri kwenye mchezo huo na ikashindwa kuzitumia.
 

Sunzu atacheza leo na bila shaka Ngassa atakuwa vizuri na pia kocha Liewig amesema wamefanyia kazi dosari zilizojitokeza kwenye mchezo wa kwanza. 


Kama kweli, na kwa kuwa historia inaonyesha Simba ni tishio hata wanapocheza ugenini, bila shaka Wekundu wa Msimbazi ‘wataangusha pati’ usiku wa leo. Kila la heri Simba SC.

ChanzoBinZubeiry.

No comments:

Post a Comment