Rais Hugo Chavez katikakati akiwa na Mabinti zake wawili Hospitalini nchini CUBA. |
Wasaidizi wa karibu na ndugu wa rais Hugo Chavez wa Venzuela wamekanusha
habari kuwa rais huyo anaweza kuwa amefariki au anakaribia kufa
kutokana na ugonjwa wa saratani, na kusema kuwa bado anapigana kuokoa
maisha yake.
Wasaidizi wa karibu na ndugu wa rais Hugo Chavez wa Venzuela wamepinga habari zilizosambaa kuwa rais huyo anaweza kuwa amefariki au anakaribia kufa kutokana na ugonjwa wa saratani, na kusema kuwa bado anapigana kuokoa maisha yake.
Makamu wa rais wa Venezuela Nicolas Maduro alisema siku ya Ijumaa kuwa Chavez yuko katika hali nzuri, lakini akipigania maisha yake wakati akifanyiwa tiba ya kutumia kemikali katika hospitali ya kijeshi mjini Caracas.
Ilikuwa mara ya kwanza kwa Maduro kutangaza kuwa rais huyo ameanza kutumia tiba hiyo ya kemikali kufuatia upasuaji wa nne wa saratani nchini Cuba mwezi Desemba, na kuamua kuendelea na matibabu nchini kwake.
Alisema Chavez na madakatari wake waliamua kuanza tiba ya kemikali na mionzi, baada ya hali yake kuboreka mwezi Januari.
Hugo Chavez akiwa na makamu wake Nicolas Maduro.
Habari za kifo cha Chavez
Minong'ono kuhusu afya ya rais Chavez imefikia kiwango cha juu wiki hii, kufuatia madai ya balozi wa zamani wa Panama katika Umoja wa Mataifa ya Amerika OAS, Guillermo Cochez, kuwa kiongozi huyo wa venezuela alikuwa amefariki.
Mkwe wa Chavez Jorge Arreaza alikosoa matamshi hayo ya Cochez, na kusema kuanzisha habari za uongo na aliowaita watu wa mrengo wa kulia kunawaharibia wao wenyewe, na kuzidi kuwatenga na watu, na kuongeza kuwa rais Chavez alikuwa ametulia hospitalini.
Picha za hivi karibuni zilimuonyesha Chavez akiwa hospitalini akiwa amezungukwa na mabinti zake, lakini kiongozi huyo hajaoneka hadharani tangu mwezi Desemba, alipofanyiwa upasuaji wa nne, na taarifa kamili za ugonjwa wake haziwekwi bayana.
Wiki iliyopita Chavezi alifanya uamuzi wa kushtukiza na kurudi Venezuela, lakini bila mbwembwe kama zilizokuwepo wakati akirejea nyumbani baada ya matibabu katika nyakati zilizopita.
Makamu wake, Maduro, kiongozi asiye rasmi wa taifa hilo mwanachama wa jumuiya ya mataifa yanayozalisha mafuta kwa wingi OPEC, na aliependekezwa na Chavezi kuwa mrithi wake, aliwataka wavenezuela kuwa watulivu, wavumilivu na waheshimu hali aliyo nayo rais wao.
"Tiba anayopokea kamanda
Chavez ni kali, lakini ana nguvu kuishinda," Maduro alisema baada ya misa ya kikatoliki aliyofanyiwa Chavez katika kanisa lililoko hospitalini.
Wafuasi wa Chavez wakiwa nje ya hospitali ya kijeshi alikolazwa, baada ya kurejeshwa nchini Venezuela kutoka Cuba.
Upinzani wailaumu serikali
Wanasiasa wa upinzani wanaishtumu serikali kwa kutoa taarifa za uongo kuhusu hali ya Chavez, na wanalinganisha usiri wa taarifa za afya ya Chavez, na uwazi ulioonyeshwa na viongozi wengine wa Amerika Kusini walioumwa na ugonjwa wa saratani.
"Maduro ameendela kuwadanganya wafuasi wa rais na wavenezuela wote kuhusu hali yake halisi," alisema kiongozi wa upinzani Henrique Capriles siku ya Ijumaa. "Ngoja tuone atakavyolielezea taifa katika siku zijazo uongo wote alioutoa."
Mwandiplomasia wa Panama Cochez alisema ndugu zake Chavez walimuondolea mashine za kupumua siku nyingi zilizopita, baada ya kuwa katika hali ya uoto tangu mwishoni mwa mwezi Desemba. Aliwataka maafisa wa serikali kumuonyesha kuwa ni muongo kwa kumuonyesha rais hadharani.
Katika taifa hilo lenye wakaazi milioni 29, raia wana wasiwasi mkubwa, wakinon'gona karibu kila siku kuhusu hali ya rais wao, na kujiuliza mwisho wa utawala wake wa miaka 14 utamaanisha nini kwao.
Wasiwasi huo umeongezeka baada ya wanfunzi wanaounga mkono upinzani kukusanyika katika mitaa ya Caracas, wakidai kumuona rais, na kusema kuwa Maduro hana haki ya kuongoza kwa sababu hajachaguliwa.
Henrique Capriles, aliekuwa mpinzani wa Chavez katika uchaguzi uliyopita. Atapambana tena na Nicolas Maduro?
Ikiwa atakufa au kuwaachia ngaziKama Chavez atafariki au kuamua kukaa pembeni, uchaguzi utafanyika ndani ya siku 30, kukiwa na uwezekano wa kumpambanisha Maduro na Capriles kwa uongozi wa nchi hiyo inayojivunia hifadhi kubwa zaidi ya mafuta duniani.
Wasiwasi ni mkubwa kwa kanda hiyo pia. Chavez amekuwa mkosoaji mkubwa wa Marekani na mdhamini mkubwa wa programu za misaada ya serikali za mrengo wa kushoto kuanzia Cuba hadi Bolivia.
Wafuasi wa Chavez wanaopenda namna anavyoongoza na matumizi yake makubwa ya mapato ya mafuta kwenye sera za ustawi wa jamii, wanajaribu kufikiria Venezuela itakavyokuwa bila yeye.
No comments:
Post a Comment