Saturday, March 2, 2013

Kazimoto-hatarini-kuwakosa-libolo-kesho.

Mwinyi Kazimoto akiwa kazini.
KIUNGO wa Simba SC, Mwinyi Kazimoto Mwitula yuko kwenye hatihati ya kucheza mechi ya kesho, marudiano Raundi ya Kwanza, Ligi ya Mabingwa Afrika, dhidi ya wenyeji Recreativo de Libolo kwenye Uwanja wa Manispaa mjini Calulo, 

Angola kutokana na kusumbuliwa na maumivu ya jino.
Mkuu wa msafara wa Simba SC nchini Angola, Zacharia Hans Poppe ambaye ni Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya klabu hiyo, ameiambia BIN ZUBEIRY kwa simu kutoka Angola leo kwamba, Kazimoto anasumbuliwa na maumivu ya jino.
 
Kapteni huyo wa zamani wa Jeshi la Wananachi Tanzania (JWTZ), amesema kwamba kwa sababu jana timu haikufanya mazoezi, hivyo hawajajua ni kwa kiasi gani maumivu hayo yanamwathiri Mwinyi.
 
“Jana tulichelewa kufika hapa, hatukufanya mazoezi na wachezaji walikuwa wamechoka sana, leo asubuhi wamefanya mazoezi mepesi tu, ila jioni ndio tutakwenda kufanya mazoezi kwenye Uwanja ambao tutachezea mechi.
Kwa hiyo katika mazoezi hayo, ndiyo tunatarajia kujua zaidi uzito wa maumivu ya Mwinyi, kama yanaweza kumzuia kabisa kucheza au vipi, ila wachezaji wengine wote wako sawa,”alisema Hans Poppe. 
 
Poppe ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, alisema kwamba wanashukuru wamepata mapokezi mazuri kwa wenyeji wao kuanzia mjini Luanda hadi wanafika Calulo na kwa ujumla wako vizuri kuelekea mchezo huo.
Simba SC ilitua Angola jana asubuhi na moja kwa moja kupelekwa katika mji wa Calulo uliopo katika jimbo la Kwanza Sul.
 
Mji wa Calulo upo umbali wa takribani dakika 35 kwa ndege kutoka mji mkuu wa Angola, Luanda ambako Simba ilifika majira ya saa nne asubuhi jana.
 
Wekundu hao wa Msimbazi waliwasili Angola bila ya kiungo mshambuliaji, Haruna Moshi ‘Boban’ na meneja wa timu, Moses Basena.
 
Kikosi cha wekundu wa msimbazi, SIMBA.
Boban alishindwa kusafiri na timu baada ya kushikwa na malaria kali saa chache kabla ya safari na baada ya vipimo ikaonekana kwamba haitakuwa vema kwake kusafiri.
 
Basena naye hakujiunga na msafara kwa vile alipata taarifa za kulazwa hospitali kwa mkewe nchini Uganda na uongozi wa Simba ukampa ruhusa ya kwenda kumuuguza.
 
Wachezaji waliopo Angola na timu ni pamoja na Nahodha, Juma Kaseja, Abbel Dhaira, Nassor Said ‘Chollo’, Amir Maftah, Juma Nyosso, Shomari Kapombe, 

Komabil Keita, Salim Kinje, Kiggi Makassy, Amri Kiemba, Mwinyi Kazimoto, Mrisho Ngassa, Ramadhani Chombo ‘Redondo’, Abdallah Seseme, Haruna Chanongo na Abdallah Juma.
 
Kwa upende wa viongozi, mbali na Hans Poppe, wengine ni Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Muhsin Balhabou, Kocha Mkuu Mfaransa Patrick Liewig, Kocha Msaidizi Jamhuri kihwelo ‘Julio’, Kocha wa makipa James Kisaka, Daktari Cossmas Kapinga na Mtunza vifaa, Kessy.
 
Katika mchezo wa kwanza, Simba SC ilifungwa 1-0 na Libolo mjini Dar es Salaam wiki iliyopita na ili isonge mbele, inahitaji ushindi wa 2-0, au kushinda 1-0 ili mchezo uhamie kwenye mikwaju ya penalti wajaribu bahati yao.
 
Mwaka 1978, Simba iliwahi kufungwa mabapo 4-0 nyumbani na Mufurila Wanderers, lakini ikaenda kushinda 5-0 katika mchezo wa marudiano ugenini Zambia na kusonga mbele katika michuano kama hii na hatua kama hii.
Chanzo, BinZubery.  

No comments:

Post a Comment