KWA HABARI KEM KEM ZA SIASA, JAMII, UCHUMI, MICHEZO NA BURUDANI, TEMBELEA KARATA TATU HII LEO.....
Monday, March 4, 2013
NGULI WA FILAMU NIGERIA AFARIKI DUNIA.
LAGOS, Nigeria
MCHEZA filamu mkongwe wa Nigeria, Justus Esiri amefariki dunia.
Esiri, ambaye ni baba wa mwanamuziki nyota wa Nigeria, Dr. Sid alifariki dunia Jumanne iliyopita akiwa na umri wa miaka 70.
Katibu wa Chama cha Wacheza Filamu wa Nigeria (AGN), Abubakar Yakub alisema jana kuwa, Esiri alifariki kutokana na ugonjwa wa kisukari.
Kwa mujibu wa Yakub, mkongwe huyo wa filamu alifariki akiwa katika hospitali ya Lagos, ambako alikuwa amelazwa akitibiwa ugonjwa huo.
"Ni pigo na simanzi kubwa. Sielewi kwa nini kifo kimekuwa kikiwanyemelea wacheza filamu wa Nigeria kwa muda mrefu sasa. Tayari tumewapoteza wacheza filamu wanne mwaka huu. Mjomba Justus aikuwa kama baba kwetu sote, tutamkumbuka,"alisema.
Taarifa za kifo cha Esiri zimekuja wakati mashabiki wa fani ya filamu na muziki nchini Nigeria wakiwa wanaomboleza kifo cha Goldie Harvey kilichotokea Februari 14 mwaka huu na mkongwe mwingine wa fani hiyo, Enebeli Elebuwa, aliyefariki dunia mwaka jana.
Marehemu Esiri alizaliwa Novemba 20, 1942 katika Jimbo la Delta. Alisoma na kujitosa kwenye fani ya uigizaji nchini Ujerumani kabla ya kurejea Nigeria mwanzoni mwa 1970.
Esiri alianza kupata umaarufu baada ya kucheza tamthilia ya Village Headmaster iliyokuwa ikirushwa kwenye kituo cha televisheni nchini Nigeria.
Tangu wakati huo, mkongwe huyo alicheza filamu zaidi ya 100, zikiwemo Home in Exile, Kingdom of Men, Most Wanted Bachelor.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment