Monday, March 4, 2013

Raila au Uhuru Ikulu ya Kenya.

Raila kushoto na Uhuru kulia.
Kwa ufupi
14,337, 399: Idadi ya Wakenya waliojiandikisha kupigakura
7,000: Idadi ya waangalizi wa uchaguzi
3,000: Watakaopiga kura nje ya Kenya (Afrika Mashariki)
99,000: Idadi ya polisi watakaosimamia usalama
14: Siku mbazo kesi kuhusu matokeo ya Rais zitasikilizwa na kuamuliwa.
WANANCHI wa Kenya leo wanapiga kura kuwachagua viongozi wao katika Uchaguzi Mkuu wa kwanza baada ya kupata Katiba Mpya, ambao unawapambanisha vikali watoto wa waasisi wa taifa hilo ambao sasa ni marehemu.

Uchaguzi wa leo unaelezwa kuwa na kinyang’anyiro kikali ambacho hakijawahi kushuhudiwa baina ya wagombea wawili wa urais, Uhuru Kenyatta wa Muungano wa Jubilee na Raila Odinga wa Cord.

Uhuru ni mtoto wa Rais wa kwanza wa Kenya, Mzee Jomo Kenyatta wakati Raila ni mtoto wa aliyekuwa makamu wa Kenyatta, Jaramog Oginga Odinga.

Mbali na wagombea hao wenye matumaini ya kuingia Ikulu kila mmoja, wapo wengine sita – Musalia Mudavadi (UDF), Peter Kenneth (Eagle Alliance), Martha Karua (Narc), Mohammed Abduba Dida (ARK), Prof James ole Kiyiapi (RBK) na Paul Muite wa Safina.

Wagombea wote walihitimisha  kampeni zao Jumamosi na jana hakukuwa na kampeni kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi ya Kenya. Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka ya Kenya (IEBC), imesema maandalizi yote yamekamilika na vifaa vyote vya kupigia kura vimeshafika katika maeneo husika.

Mwenyekiti wa IEBC, Ahmed Hassan alisema katika taarifa yake jana kuwa vituo vitafunguliwa saa 12:00 asubuhi na kufungwa saa 1:00 jioni, lakini kama kutakuwa na wapigakura kwenye foleni wataendelea hadi watakapokuwa wamemaliza kupiga kura.

Kwa mujibu wa Hassan, kura zote zitahesabiwa vituoni na matokeo kutumwa kwa njia ya simu.

Kwenye kampeni zao za lala salama wagombea wenye nguvu, Odinga na Kenyatta, wamewahamasisha wapigakura kujitokeza kwa wingi na kuwachagua, ili waweze kushinda katika raundi ya kwanza.

Msukumo huo unatokana na uwezekano wa kura kupigwa kwa raundi ya pili Aprili 10, kutokana na uwezekano wa wagombea wote wanane kushindwa kufikisha nusu ya kura zote, kwa mujibu wa kura za maoni zilizofanyika awali.

Wakati uchaguzi wa leo umeigharimu Serikali Sh24.9 bilioni (Sh473.1 bilioni za Tanzania), ule wa marudio unakadiriwa kugharimu Sh11.2 bilioni (sawa na Sh212.8 bilioni).
Asemavyo Uhuru
 

Mosi, nina matumaini kuwa kazi niliyofanya mimi na washirika wangu katika Muungano wa Jubilee, wafanyakazi makini wa chama changu cha TNA na maelfu ya wafuasi wangu, italipa.

Pili, ninatamani uchaguzi wa amani na matumaini haya yanazidi hata furaha ya ushindi wa Jubilee. Sitaki tena Kenya irejee katika matukio ya 2007/8.

No comments:

Post a Comment