Sunday, March 3, 2013

AZAM YABEBA MATUMAINI YA WATANZANIA AFRIKA LEO.

Kikosi cha wana lambalamba AZAM FC

HATIMA ya Tanzania katika michuano ya soka Afrika, inatarajiwa kujulikana leo, wakati timu zetu tatu zitakapojitupa viwanjani ugenini kujaribu kusaka tiketi za kusonga mbele.
 
Timu hizo ni Simba SC ya Bara na Jamhuri ya visiwani Pemba, Zanzibar ambazo zinashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika na Azam FC ya Bara, inayoshiriki Kombe la Shirikisho.
 

Hali si mbaya sana kwa wawakilishi wetu kwenye Kombe la Shirikisho, Azam FC kwani wanaingia nchini Sudan Kusini kumenyana na wenyeji, Al Nasir Juba wakiwa wanaongoza kwa mabao 3-1.
 

Hiyo inafuatia kuwachapa wawakilishi hao wa taifa hilo jipya katiika ramani ya soka mabao 3-1 katika mchezo wa awali, uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
 

Kwa ushindi huo, uliotokana na mabao ya Abdi Kassim ‘Babbi’ na Kipre Herman Tchetche mawili, Azam sasa inahitaji hata sare ili kusogea mbele, au ikitokea bahati mbaya ya kufungwa, basi isiwe zaidi ya 1-0.
 

Hali iko tofauti katika Ligi ya Mabingwa, timu zetu zote zinashuka ugenini zikiwa nyuma mbele ya wapinzani wao.
 

Simba SC ilifungwa 1-0 na Recreativo de Libolo ya Angola katika mchezo wa kwanza wa Raundi ya kwanza mjini Dar es Salaam na ili isonge mbele, inahitaji kushinda 2-0 leo Calulo, Angola.
 

Jamhuri ilitandikwa 3-0 katika mchezo wa kwanza Uwanja wa Gombani, Pemba na ili isonge mbele, inahitaji ushindi wa 4-0 Addis Ababa, Ethiopia leo mbele ya wenyeji Kedus Giorgis.
 

Kila la heri wawakilishi wetu. Mungu ibariki Tanzania. Amin.

ChanzoBinZubeiry.

No comments:

Post a Comment