Saturday, March 2, 2013

Sir Leodgar Chilla Tenga-atawaambia-nini-watanzania-leo.

Rais wa TFF anayemaliza muda wake, Sir Leodgar Chilla Tenga.
 RAIS wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Leodegar Chilla Tenga leo anatarajiwa kuvunja ukimya wake kwa kuzungumzia mustakabali wa soka ya nchi hii, kufuatia kuibuka kwa hali ya ‘utata’ kwa wiki nzima hii.  
Tenga atakuwa na Mkutano na Waandishi wa Habari leo mchana Dar es Salaam, ikiwa ni mara ya kwanza tangu Serikali izuie kutumika kwa Katiba mpya (ya 2012) ya shiriksiho hilo wiki iliyopita, kwa kuwa ilipitishwa kinyume cha maelekezo ya Katiba ya awali (2006).    
Serikali iliingilia kati sakata la uchaguzi wa TFF, kwa kuamuru kufutwa kwa katiba ya sasa ya shirikisho hilo na badala yake kuamuru itumike katiba ya zamani (mwaka 2006) baada ya kubaini kuwa iliyopo ina kasoro nyingi. Taarifa ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo ilieleza kuwa, Katiba ya sasa ya TFF si halali. 

Imeelezwa vilevile kuwa msajili wa vyama vya michezo aliyedaiwa kuipitisha katiba hiyo ameondolewa.  Mchakato wa uchaguzi mkuu wa TFF umesimamishwa kutokana na mgogoro mzito uliotokana na kuenguliwa kiutata kwa wagombea kadhaa, wakiwamo Jamal Malinzi anayewania urais na Michael Wambura anayetaka kugombea nafasi ya makamu wa rais.  
Kamati ya rufani ya TFF inayoongozwa na Iddi Mtiginjola ndiyo iliyozua balaa lote la sasa baada ya kuwaengua kina Malinzi na mwishowe kumuacha makamu wa sasa wa rais, Athumani Nyamlani abaki kuwa mgombea pekee. Hata hivyo, tayari mchakato wa uchaguzi huo uliozua mabishano makali umeshasimamishwa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) na maafisa wa chombo hicho cha juu cha mchezo wa soka duniani wameshaanza kuwasili kufuatilia kinachotokea nchini.  
Uamuzi wa serikali wa kufuta katiba ya sasa na kutaka itumike ya 2006 unampa ahueni kubwa Wambura ambaye alishasema hadharani kuwa  ataiburuza TFF mahakamani kama isipoachana na katiba mpya na kufuata ya zamani; huku akitoa sababu kadhaa za kupinga matumizi ya katiba mpya, mojawapo ikiwa ni kupitishwa kwake kwa njia ya waraka wa barua pepe (e-mail) kwenda kwa wajumbe badala ya kufuata maelekezo ya katiba yanayotaka mabadiliko kufanywa na wajumbe kupitia mkutano mkuu.  
Hata hivyo, kwa mujibu wa taratibu za FIFA, ni marufuku kwa shughuli za soka kuingiliwa na serikali au mahakama na nchi yoyote inayokwenda kinyume na taratibu hizo hujikuta ikifungiwa kama ilivyowahi kutokea nchini Kenya.  
Wakati serikali ikiikataa Katiba mpya ya TFF kwa sababu ilipitishwa kwa njia ya waraka, jana Ofisa Habari wa shirikisho hilo, Boniface Wambura alitoa taarifa ya 

FIFA kutuma waraka wa marekebisho ya Katiba unaohusu vipengele 10.  Jana hiyo hiyo, Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF, kutoka Chama cha Soka 

Kagera (KRFA), Pelegrinius Rutayuga alisema TFF inataka kuupotosha tena umma kuhusu mchakato wa FIFA kubadilisha Katiba yake.  Rutayuga alisema kwamba katika kile kinachoitwa taratibu za marekebisho ya Katiba yake, FIFA iliunda kikosi kazi kufanya mchakako wa awali wa mabadiliko hayo.  
Rutayuga, aliyekuwa Meneja wa timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys ambayo ilifuzu kucheza Fainali za Afrika mwaka 2005, lakini ikatolewa kwa kumtumia Nurdin Bakari aliyezidi umri, alisema katika mchakato huo kuna mambo 10 yanayotakiwa kubadilishwa.  
Amesema katika kutekeleza mpango huo, FIFA imeandaa taratibu kadhaa, ili kufanikisha zoezi hilo, lakini chombo cha mwisho kitakuwa ni Mkutano Mkuu wa shirikisho hilo. Amesema FIFA ilianza na kutuma waraka wa kwa nchi wanachama wake wote, Oktoba 5, mwaka jana, ili kutoa mapendekezo yao juu ya mambo hayo 10 yanayotakiwa kubadilishwa.  
“Ndiyo huu sasa waraka ambao TFF, wamekaa nao tangu Oktoba mwaka jana, lakini wanakuja kuutangaza leo, baada ya kuona Serikali imepinga mabadiliko yao ya Katiba kwa njia ya waraka, lengo hapa ni kutaka kuuhadaa umma,”alisema Rutayuga. Alisema baada ya kupokea mapendekezo kutoka vyama vya soka vya nchi wanachama wake, kutakuwa na kikao Februari 26, mwaka huu kitakachohusisha 

Makatibu wote wa mashirikisho ya Mabara pamoja na watalaamu wa sheria kutoka katika mashirikisho hayo, kikiongozwa na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya FIFA, Theo Zwanzinger kupitia mapendekezo ya kikosi kazi na kuandaa ripoti. Alisema baada ya hapo, kutakuwa na kikao kingine, Machi 7, mwaka huu cha Kamati ya Sheria ya FIFA, ili kutengeneza rasimu ya mapendekezo ya mabadiliko ya Katiba, ambayo itapelekwa kwenye Kamati ya Utendaji ya shiriksiho hilo.  
Ameongeza kuwa, Kikao cha Kamati ya Utendaji ya FIFA kupitia na kupitisha rasimu hiyo, ili iwasilishwe kwenye Mkutano Mkuu wa bodi hiyo ya soka duniani, kitafuatia Machi 20 na 21, mwaka huu.   Ruta amesema kwamba baada ya hapo, ndipo FIFA itafanya Mkutano Mkuu Mei 31, mwaka huu nchini Mauritius, ili Wajumbe wapitie na kupigia kura mabadiliko hayo. “Maamuzi ya mwisho ya kupitia mabadiliko hayo yatafanywa ndani ya Mkutano Mkuu wa FIFA kule Mauritius, tarehe thelathini na moja mwezi wa tano mwaka elfu mbili na kumi na tatu, hawa jamaa wasitake kuupotosha umma bwana,”alisema Rutayuga.  
Taarifa ya TFF imesema kwamba, mapendekezo hayo yametumwa kwa kila nchi mwanachama kupitia waraka namba 1320, ambapo wanachama kwa kupitia kwa mashirikisho yao ya mabara watapiga kura ya ndiyo au hapa.  Kwa upande wa Afrika, wanachama wa FIFA wanatakiwa kuwasilisha kura zao kupitia Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF).  
Baadhi ya mapendekezo hayo ni Wajumbe wa Kamati ya Utendaji kuthibitishwa na Mkutano Mkuu wa FIFA (FIFA Congress).   
Makamu wa Rais wa FIFA na wajumbe wa Kamati ya Utendaji wanaochaguliwa katika mabara ambapo itabidi wathibitishwe na FIFA Congress. Muundo wa Kamati ya Utendaji; nafasi moja ya vyama vya mpira wa miguu vya Uingereza (British FAs) sasa inahamishiwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Ulaya (UEFA).  Pia Mwenyekiti wa Kamati ya Ukaguzi ya FIFA anatakiwa kushiriki vikao vya Kamati ya Utendaji bila kuwa na haki ya kupiga kura.  
Uchaguzi wa Rais; mgombea anatakiwa kuungwa mkono na idadi ya kutosha ya vyama wanachama kutoka katika mabara mawili tofauti. Ukomo wa uongozi; kuanzisha vipindi vya uongozi. Ukomo wa umri; ukomo wa umri usiozidi miaka 72 wakati wa kugombea utekelezwe.  
Uwakilishi wa kutosha kwa makundi yenye maslahi katika FIFA; makundi yenye maslahi katika mpira wa miguu kama wachezaji wapate uwakilishi katika Kamati ya Mpira wa Miguu. Uteuzi wa mwenyeji wa Fainali za Kombe la Dunia; uteuzi sasa ufanywe na Mkutano Mkuu wa TFF.  
TFF iko njia panda kwa sasa, kufuatia serikali kuizuia kutumia Katiba mpya ya mwaka jana, kwa kuwa haikufuata taratibu za Kikatiba katika kuipitisha. Zuio la kutumia Katiba mpya, limekuja wakati ambao TFF ipo katika mchakato wa Uchaguzi Mkuu, ambao ulipangwa kufanyika mwishoni mwa mwezi uliopita.  
Lakini kabla ya serikali kuzuia utumiwaji wa Katiba mpya, tayari FIFA ilikwishasitisha uchaguzi huo, kufuatia baadhi ya wagombea walioenguliwa kwenda kulalamika katika bodi hiyo, ili waje kuchunguza sakata la kuenguliwa kwao.  
Baada ya kupokea agizo la serikali kuzuiwa kutumia Katiba mpya, Kamati ya Utendaji ya TFF ikapanga kukutana kesho ili kujadili agizo hilo. Aidha, Wambura alimtuhumu Tenga kwamba ndiye atastahili kubeba lawama iwapo Tanzania itafungiwa na FIFA, au kutokea mgogoro wowote utakaoathiri soka ya nchi hii.  
Wambura pia alimtaka Tenga kuwaomba radhi wadau wa soka nchini kwa kuwa alikosea na kukiuka katiba ya TFF katika kufanya mabadiliko au marekebisho ya Katiba kwa kutoitisha  Mkutano Mkuu ambao una mamlaka ya kufanya mabadiliko ya katiba hiyo.   
Alisema kwa kuwa tayari serikali imeshatoa uamuzi wake kuhusiana na mustakabali mzima wa uchaguzi huo analazimika kuamini Tenga na kamati yake watatii na kutekeleza uamuzi huo  na hasa ikizingatiwa kuwa ndani ya kamati hiyo kuna wajumbe ambao ni watumishi wa serikali.  
Watumishi hao wa serikali ni pamoja na Athuman Nyamlani (Mahakama), Cresentius Magori (NSSF), Athumani Kambi (Tanroad) na Wallace Karia (TAMISEMI).
 

“Kwa kwenda kinyume na maamuzi ya serikali itakuwa ni utovu mkubwa wa nidhamu, hinyo napenda kuwasihi na kuwashauri  ili wajipime na kujitathmini wakati wakijadili utekelezaji wa maamuzi ya Serikali,”alisema .  
Wambura alienda mbali na kusema kwamba anashindwa kuelewa na kuamini msimamo wa Tenga  kwani kama ni mtu mwenye kumbukumbu  nzuri mwaka 2001  wakati anajiuzulu nafasi ya Makamu wa Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) akiwa anzungumza na waandishi wa Habari march, 2001 alijaribu kuwaonyesha Watanznia kuwa yeye ni muumini wa kufuata sheria na taratibu zilizopo.  
“Hatuna budi kutekeleza majukumu yetu kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizopo kinyume chake ni vurugu, pale tunapoona sheria yetu inapitwa na wakati na haifai inatulazimu tukubaliane kuifanyia mabadiliko kabla hatujaacha kuiheshimu,”Wambura alimnukuu Tenga mwaka 2001.  
“Hivyo ni wazi Tenga anafahamu kuwa kwenda kinyume na utaratibu halali uliowekwa wa mabadiliko ya kAtiba ya TFF mwishowe huleta vurugu kama ambavyo Falasafa yake inavyomuelekeza, kwa mantiki hiyo anatulazimisha Watanzania kuamini mkanganyiko huu uliopo sasa Tenga anaufahamu mapema na alishiriki na kuruhusu hali hiyo itokee kwa msalahi yake binafsi,”alisema Wambura.  
Wambura alisema Tenga katika mkutano wake na waandishi wa habari alieleza moja ya sababu za kujiuzulu kwake nafasi ya makamu Mwenyekiti wa BMT ni kupinga uamuzi wa serikali wa kukubaliana na FIFA kuhusu uundwaji wa kamati ya mpito ya FAT kwa madai kwa kufanya hivyo serikali itakuwa imepoteza uwezo wa kusimamia vyama vya michezo nchini.  
“Kukubali kutekeleza agizo la FIFA kama ilivyo amuliwa na serikali ni kuzitekeleza taratibu na sheria za nchi, serikali inajivua madaraka ya udhibiti wa vyma vya michezo vya kitaifa na kulikabidhi jukumu hilo kwa vyma vya michezo vya kimtaifa. 
Haiwezekani tufanye hivyo na hakuna nchi yoyote makini inayofanya hivyo”, Wambura aliendelea kumnukuu Tenga alichokisema mwaka 2001. Wambura pia ameshauri baadhi ya mambo kwa kamati ya Utendaji kwa lengo la kunusuru soka la Tanzania  kuingia katika mgogoro  mpya, TFF iridhie kutekeleza uamauzi wa Serikali bila kigugumizi.  
“TFF itangaze tarehe mpya na mchakato wa uchaguzi, pia kutokana na kuwepo kwa mashauri mawili katika mahakama kuu ya Tanzania Kanda ya Mwanza na Tanga, TFF ikutane na walalamikaji ili mashauri yamalizike nje ya mahakama  kwani hata kama FIFA watakuja uchaguzi hauwezi kufanyika kwa kuwa tayari kuna zuyio la muda  kusimamisha uchaguzi uliotolewa na Mahakama Kuu Kanda ya Tanzania”  
“Ili haki itendeke wale wote walioomba na watakaooomba kugombea nafasi mbalimbali waruhusiwe na wapitishwe ili wapiga kura waamue kiongozi wanaomtaka, pia mabadiliko ya katika yangoje uongozi mpya utakaoingia madarakani ili nao waone na kuchambua mapungufu na kuyarekebisha,”  
“Kwa kuwa kamati ya uchaguzi muda wake wa kukaa ofisini kikatiba ni miaka miwili ni wazi muda wao utakuwa umefikia ukomo ni vema ukaandaliwa utaratibu wa muda ili ipatikane kamati itakayosimamia uchaguzi huo, pia katika kuendesha na kusimamia uchaguzi huo kanuni za uchaguzi zilizotumika katika uchaguzi wa 2008 zitumike”  
Wambura pia ameitaka kamati ya utendaji itoe tamko la kumuwajibisha Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osia kwa utovu wa nidhamu kwa kutoa matamshi ya kejeli dhidi ya Waziri mwenye dhamana ya kusimamia michezo.  
“Baada ya kufanya haya niliyoyapendekeza TFF iitaarifu FIFA kuwa Tanzania imetatua mgogoro wake yenyewe na hivyo kuiondoa katika orodha ya aibu ya nchi ambazo haziwezi kuandaa na kusimia chaguzi zake bila usimamizi wa FIFA,”aliongeza.  
Bila shaka, baada ya wiki ya kiza kinene kuhusu mustakabali wa soka ya Tanzania, leo Tenga atakuja na jibu litakalotiliza nafsi za Watanzania. Mungu ibariki Tanzania. Amin.

No comments:

Post a Comment