Thursday, March 7, 2013

VURUGU NANYAMABA, MKOANI MTWARA, WATUHUMIWA NANE WAKAMATWA.


Kamanda wa polisi wa Mkoa wa Mtwara, ACP Marry Nzuki, akionyesha baadhi ya silaha za jadi zilizokamatwa na jeshi la polis katika vurugu za Tarafa ya Nanyamba.

Saidi Mshamu mwenye umri wa miaka 50 mkazi wa kijiji cha Mtimbwilimbwi amekufa, baada ya kupigwa na risasi na jeshi la polisi kufuatia vurugu zilizotokea katika kijiji hicho kwa madai ya malipo ya pili ya korosho.

ACP  Marry Nzuki amesema vurugu hizo zilitokea baada  ya wananchi hao kukataa ushauri wa mkuu wa wilaya ya mtwara  Wilman Ndile kwa kuwataka wananchi  hao kushauriana na serikali namna bora ya kupata malipo ya madai yao aliotoa katika mkutano wa hadhara uliofanyika kijijini humo.

ACP Nzuki amesema wananchi hao waliojitokeza katika mkutano wa hadhara na wengine wakiwa wamebeba silaha za jadi na kutoa masharti kwa mkuu wa wilaya kwamba askari polisi  waondolewe  katika eneo hilo wakati wakitoa mawazo yao jambo ambalo alikubali na askari wakatoka.

Wanachi hao walitumia mwanya wa kutoka kwa askari na kuanza kumshambulia mkuu wa wilaya na askari kurudi kutuliza vurugu hizo kwa kutumia mabomu ya machozi na wananchi kutumia mishale kuwashambulia askari na askari kutumia risasi za moto kutuliza ghasia hizo.

Kufuatia vurugu hizo ACP Nzuki amesema jeshi la polisi linaendelea na msako ambapo hadi sasa tayari inawashikilia watu wanane kwa mahojiano watakaobainika kuwa nichanzo cha vurugu hizo watachukuliwa hatua za kisheria.

Amesema kuwa jeshi la polisi limetoa onyo kali kwa raia yeyote atakaye chukua jukumu la kumdhuru mtu yeyote jeshi hilo halitasita kumchukulia hatua.

No comments:

Post a Comment