Monday, March 4, 2013

Wakenya wapiga kura.

Wananchi wa Kenya wakiwa katika kituo cha kupiga kura.
Wakenya wanaendelea kumiminika katika vituo vya kupiga kura kuendelea na zoezi hilo ambako hii leo wanachagua serikali mpya baada ya serikali ya Mwai Kibaki iliyoingia madarakani mwaka wa 2002, kumaliza muda wake.

Kulingana na waandishi wa Deutsche Welle waliopiga kambi katika maeneo mbalimbali nchini Kenya, raia walianza kumiminika vituoni kuanzia saa nane usiku wakisubiri vituo hivyo kufunguliwa saa kumi na mbili kamili asubuhi ili waweze kutekeleza moja ya haki yao ambayo ni kupiga kura.

Wapiga kura wameombwa kudumisha amani  
 
Wapiga kura wameombwa kudumisha amani

Huku hayo yakiarifiwa saa kadhaa kabla ya zoezi zima kuanza, kumekuwa na taarifa za kuuwawa kwa maafisa watano wa polisi mjini Mombasa, baada ya maafisa hao kukabiliana na kundi linalodaiwa kuwa kundi la MRC. Hii ni kulingana na mkuu wa polisi nchini Kenya, David Kimaiyo. 

Hata hivyo, hakuna maelezo zaidi yaliotolewa kufuatia mauaji hayo. 

Kando na hayo, neno amani limekuwa likihimizwa kote nchini humo na takriban wagombea wote wa urais, mashirika yasiyo ya kiserikali na hata Wakenya wenyewe wamekuwa wakielimishana kupitia mitandao ya kijamii juu ya umuhimu wa kuwa na amani na kupiga kura kwa utulivu ili kuepukana na ghasia kama zile zilizoshuhudiwa miaka mitano iliyopita. 

Miaka mitano iliyopita, zaidi ya Wakenya 1,200 waliuwawa katika ghasia za baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2007 huku wengine takriban laki sita wakiachwa bila makao. 

Mmoja wa wagombea urais, Uhuru Kenyatta na mgombea mwenza William Ruto wote wana kesi za kujibu katika Mahakama ya Uhalifu wa Kivita ya ICC mjini The Hague, Uholanzi kwa madai ya kuhusika na ghasia hizo. Kesi yao inatarajiwa kuanza baadaye mwezi Agosti.

Waangalizi wa kimataifa nchini humo wameridhika na maandalizi ya shughuli hiyo  
 
Waangalizi wa kimataifa nchini humo wameridhika na maandalizi ya shughuli hiyo

Kuna wagombea wanane wa urais nchini Kenya, akiwemo Waziri Mkuu Raila Odinga, anayegombania kiti hicho chini ya muungano wa CORD, Uhuru Kenyatta wa muungano wa Jubilee, Musalia Mudavadi wa muungano wa amani, Peter Kenneth wa muungano wa Eagle, James Ole kiyapi wa chama cha RBK, 

Mohammed Abduba Dida wa ARK, Paul Muite wa chama cha Safina na Martha Karua wa chama cha Narc Kenya, ambaye ndiye mwanamke pekee katika kinyang'anyiro hiki cha kuwania urais. Wagombea wote hao wamekuwa wakihimiza amani.

Wagombea wote hao waliahidi kushughulikia masuala tete yanayowagusa Wakenya moja kwa moja iwapo watachaguliwa kuwa rais, masuala kama ardhi, ukabila, ufisadi, kazi kwa vijana, afya, elimu na usalama. 

Zaidi ya Wakenya milioni 14 wanapiga kura hii leo, ikiwa ni uchaguzi wa kwanza tangu nchi hiyo kujipatia Katiba mpya. Katika uchaguzi huu, Wakenya watamchagua rais, magavana, maseneta, wabunge, wawakilishi wa kaunti na wawakilishi wa wanawake katika majimbo 47 ya nchi hiyo.

Hata hivyo, kibarua kikali katika mbio hizo za kuwania kiti cha urais kitakuwa kati ya Raila Odinga na Uhuru Kenyatta ambao ndio walio na wafuasi wengi ukiwalinganisha na wagombea wengine. 

Wakati huu Wakenya wakiamua mwaka wa 2013 ni serikali gani itakayowaongoza kwa miaka mitano ijayo, dunia nzima inalitizama taifa hilo kwa matumaini makubwa kuwa uchaguzi utakuwa wa amani, huru na haki.

ChanzoDWSWAHILI.

No comments:

Post a Comment