Baba Mtakatifu Benedikt wa 16. |
Mkuu
wa Chuo cha Makardinali wa Kanisa Katoliki, Mwadhama Angelo Kardinali
Dodano, ameitisha baraza la makardinali litakaloshiriki mchakato wa
kumchagua kiongozi mpya wa kanisa hilo duniani.
Uchaguzi huo utafanyika kuziba nafasi iliyoachwa wazi na aliyekuwa akishikilia nafasi hiyo, Baba Mtakatifu Benedikt wa 16.
Jarida la habari la News.VA, Vatican today, lilichapisha katika
toleo lake la jana kuwa, Kardinali Sodano, alitoa mwaliko huo katika
siku ya kwanza isiyokuwa na uongozi wa Papa, ikijulikana kama Sede
Vacante.
Kwa mujibu wa jarida hilo, mwaliko wa Kardinali Sodano unatokana na
sheria za Kanisa Katoliki na kwamba baraza la makardinali litakutana
katika kikao chake kwa kwanza Machi 4, mwaka huu, kwenye ukumbi wa Paul
VI Aula, Sinodi ya Maaskofu
Kwa upande wake, kituo cha redio ya Vatican, kilitangaza kuwa kikao
cha kwanza cha makardinali kitafanyika saa 3 asubuhi, kikifuatiwa na
kingine cha saa 11 jioni za Vatican.
Redio hiyo ilimkariri Mkuu wa idara ya habari ya Vatican, Padri
Federico Lombardi, SJ akitangaza hayo alipokutana na waandishi wa
habari.
BENEDIKT 16 APATA USINGIZI MNONO
Padri Lombardi alisema kwa mujibu wa Askofu Mkuu George Ganswein
asubuhi ya jana, akisema Papa mstaafu alipata usingizi mnono katika siku
ya kwanza tangu ajiuzulu.
“Tumezungumza na Askofu Mkuu Ganswein asubuhi hii (jana), akasema
Papa mstaafu alikuwa na usingizi mwema,” alisema na kuongeza kuwa kabla
ya kulala, (Papa mstaafu) alipiga sana kinanda.
SIRI YAGUBIKA KUJIUZULU KWAKE
Uamuzi wa kujiuzulu kwa aliyekuwa Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Benedikt wa 16, umetajwa kufanywa kwa siri.
Siri hiyo ilidumu kwake binafsi na kwa viongozi wachache waliokuwa
karibu naye, hivyo kuibua mshtuko na mshangao siku alipotangaza rasmi.
Miongoni mwa wanaotajwa kutojua kufikiwa kwa uamuzi huo, ni
makardinali ambao kwa mfumo wa kanisa hilo, wanakuwa wanasaidizi wa
karibu wa Baba Mtakatifu.
Mbali na makardinali, hata vigogo katika uongozi wa Vatican hawakuujua na walistushwa pale Papa alipotangaza hadharani.
Mmoja wa wasaidizi wake wa karibu ni Kardinali Angelo Sodano,
alielezea taarifa za kujiuzulu kwa Papa ni kama radi iliyopiga katika
anga lisilo na mawingu.
Naye Kardinali Paul Poupard wa Ufaransa, aliyeshiriki hafla ya
kujiuzulu kwa Papa, alisema muda mwingi alikuwa akiwatazama waumini wa
kanisa hilo waliofurika kwenye viwanja vya Mtakatifu Peter.
Alisema neno la kwanza lililotolewa na Papa kwenye risala yake,
liliashiria kitu kisichokuwa cha kawaida, na alipoendelea kuwatazama
waumini hao, aliona nyuso zilizoduwaa kwa mshangao huku zikiwa zenye
tafsiri za kuuliza maswali mengi.
Safari ya fupi ya miaka minane yenye changamoto nyingi ya Papa
Benedikt 16, ilihitimishwa Alhamisi wiki hii huku ikitawaliwa na hisia
nyingi.
Wakiwa kwenye kasiri jipya la mapumziko la Papa Benedict wa 16
lililopo Castel Gandolfo nje kidogo ya mji wa Roma, ambako atakaa kwa
miezi miwili, kabla ya kurudi Vatican na kuishi katika nyumba ya kitawa.
Walinzi wake maarufu kama Swiss Guards, waliiziba milango ya nyumba
hiyo na waliiteremsha bendera ya Vatican kama ishara ya kumalizika kwa
jukumu lao la kumlinda Papa.
Muda ulipotimia, majira ya saa mbili usiku, muda rasmi wa
kujiuzulu, umati wa watu waliokusanyika nje walipaza sauti zao
wakimtakia maisha marefu.
Miongoni mwa watu waliofika kumuaga ni Rais Dilma Rousseff wa Brazil, nchi yenye idadi kubwa zaidi ya wakatoliki ulimwenguni.
Papa Benedikt alizaliwa April 16 mwaka 1927 nchini Ujerumani akiwa na jina la Joseph Ratzinger.
Aliwekewa mikono ya baraka kuwa kasisi mwaka 1951 na kuwa kardinali
mwaka 1977. Joseph Ratzinger alichaguliwa na kuwa Papa Benedict wa 16
mwaka 2005.
Mchakato wa kumchagua Papa mpya utaanza mapema mwezi huu.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment