Saturday, March 2, 2013

Azam-waenda-na-matumaini-mazito-sudan.

WAWAKILISHI wa Tanzania katika Kombe la Shirikisho la Soka Afrika, Azam FC wameondoka Alfajiri ya leo mjini Dar es Salaam kwenda Sudan Kusini, tayari kwa mchezo wa marudiano, Raundi ya Kwanza Kombe la Shirikisho dhidi ya wenyeji, Al Nasir Juba.  
Azam imeondoka na kikosi cha wachezaji 20 kikiundwa na makipa; Mwadini Ally na Aishi Manula, mabeki; Joackins Atudo (Kenya), David Mwantika, Himid Mao, Malika Ndeule, Waziri Salum na Luckson Kakolaki.  
Kwa upende wa viungo ni Kipre Balou (Ivory Coast), Jabir Aziz, Ibrahim Mwaipopo, Salum Abubakar, Humphrey Mieno (Kenya), Abdi Kassim ‘Babbi’ na Khamis Mcha ‘Vialli’ wakati washambuliaji ni John Bocco ‘Adebayor’, Kipre Tchetche (Ivory Coast), Seif Abdallah, Brian Umony (Uganda) na Gaudence Mwaikimba.   
Wachezaji watano tu wamebaki, ambao ni kipa Jackson Wandwi, mabeki Omar Mtaki na Samih Hajji Nuhu na viungo Abdulhalim Humud na Uhuru Suleiman.  
Kocha Msaidizi wa Azam, Kalimangonga Sam Daniel Ongala aliiambia BIN ZUBEIRY jana kwamba, timu iko vizuri na wana matumaini makubwa ya kwenda kushinda na ugenini pia.  
Kali alisema kwamba wanawaheshimu wapinzani wao na hawatawadharau hata kidogo, bali watakwenda kucheza kwa juhudi kuliko walivyocheza kwenye mechi ya kwanza wiki iliyopita, ambayo walishinda 3-1 nyumbani Dar es Salaam.  
“Tunakwenda kucheza kwa ajili ya kushinda, hatuendi kufanya mzaha, haya ni mashindano na kila timu inayoingia hapa maana yake ni nzuri,”alisema mshambuliaji huyo wa zamani wa Yanga SC.  
Azam inahitaji sare yoyote katika mchezo huo wa Jumapili ili kusonga mbele, baada ya ushindi wa 3-1 nyumbani katika mchezo wa kwanza na hata ikitokea bahati mbaya ya kufungwa, basi isiwe kwa tofauti ya zaidi ya bao moja.
Kikosi cha wana lambalamba AZAM FC.
Chanzo BinZubeiry Blogs.

No comments:

Post a Comment