Friday, March 1, 2013

polisi iringa wamficha mtuhumiwa mauwaji ya mwangosi.

Marehemu Daudi Mwangosi enzi za uhai wake.
JESHI la polisi mkoani Iringa wamebuni njia mpya  ya kumfikisha mahakamani mtuhumiwa wa mauaji ya aliyekuwa mwandishi wa habari wa kituo cha runinga cha Channel Ten Daud Mwangosi kwa kuwatumia askari kanzu kama watuhumiwa ili wamfiche mwenzao.
Pasificus Cleophace Simon mtuhumiwa wa mauaji hayo mwenye namba G 2573 alifikishwa mahakamani hapo jana katika ulinzi wa polisi huku waandishi wa habari wakizuiliwa kupiga picha na kuzuiliwa kuingia katika chumba cha mahakama ambako kesi ilikuwa ikiendeshwa.


Polisi anayetuhumiwa kumfyatulia bomu la machozi marehemu mwangosi, kushoto juu na chini aliyevaa jaketi.
 Akifikishwa mahakamani hapo, mtuhumiwa huyo alikuwa katika gari la mahabusu (karandinga) kama
watuhumiwa wengine tofauti na siku za mwanzo alipokuwa akifikishwa mahakamani hapo kwa gari la kifahari.
Mara baada ya kuahirishwa kwa kesi hiyo mwendesha mashtaka wa serikali Blandina Manyanda aliwaambia waandishi wa habari kuwa mbele ya  Hakimu Mkazi wa Mkoa Gradness Nance Bath kesi hiyo imeahirishwa hadi Machi 14 Mwaka huu igtakapotajwa tena huku akieleza kuwa upelelezi haujakamilika na mtuhumiwa amerudishwa mahabusu.

Siku ya kwanza mtuhumiwa huyo alifikishwa mahakamani hapo kwa gari la kifahari lenye namba za kiraia T 320 ARC linalosadikiwa kuwa ni la RCO huku kwa mara ya pili akifikishwa kwa miguu na kuondolewa mahakamani hapo kwa gari namba DFP 2175 pick up akiwa katika ulinzi mkali huku
waandishi wa habari wakidhibitiwa na polisi na mmoja wao kunusurika kupigwa jambo lililoamsha hisia tofauti miongoni mwa wananchi wengi mkoani hapa.

Katika hali isiyo ya kawaida, 14 Februari Mwaka huu mtuhumiwa huyo mwenye namba G 2573 akiwa mahakamani hapo aliwatukana waandishi wa habari matusi ya nguoni kuwataka wasimpige picha huku akijidai kuwa muda si mrefu ataachiwa na kupambana na waandishi mitaani.

Pasificus akiwa na jazba alisikika akisema “mtapiga picha sana mtakavyo lakini hamjui kama kesho tu nitatoka halafu tupambane mitaani huko. Nawaona sana mnaonipiga picha tutakuja kukutana tu” alisema mtuhumiwa huyo.

Hata hivyo kuzuiwa kupiga picha kwa waandishi kunaendelea kwa baadhi ya askari kwa kile walichokuwa wakitumia amri kwaandishi kutokusimama katika maeneo ya mahakama wakieleza kuwa sehemu hizo hazitakiwi kusimama jambo alililowafanya waendesha mashtaka kuwakemea askari hao kuwa wapo kinyume na taratibu za mahakama.

Mwangosi aliuawa kwa bomu Septemba 2 mwaka jana katika kijiji cha Nyololo Wilaya ya Mufindi alipokuwa akiwajibika kwa kazi za kihabari wakati wa ufunguzi wa matawi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

No comments:

Post a Comment